Dodoma. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo Jumatatu, Novemba 17, 2025 Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma ameunda wizara 27 na kuteua mawaziri 27 na naibu mawaziri 29.
Katika wizara hizo, Rais Samia ameirejesha tena Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mwaka 2015, Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli alipounda Baraza lake la mawaziri kwa mara ya kwanza, aliitoa Tamisemi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwenda kuwa chini ya Ofisi ya Rais ambapo imekuwa hivyo kwa miaka 10.
Lakini leo Jumatatu, Rais Samia kwenye Baraza lake, ametangaza kuipeleka Tamisemi kuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo Waziri Mkuu kwa sasa ni Dk Mwigulu Nchemba.
“Tawala za mikoa ilikuwa chini ya Ofisi ya Rais, lakini kwa kuwa waziri mkuu ndiyo msimamizi wa shughuli zote za Serikali, tumeirudisha kwa Waziri Mkuu,” amesema Rais Samia.
Miongoni mwa mambo yaliyopo chini ya Tamisemi ni Wakuu wa Mikoa (RC), Wilaya (DC), Makatibu Tawala wa Mikoa (RAS), Wilaya (DAS), Wakurugenzi wa Halmashauri (DED), vituo vya afya na hospitali za wilaya.
Pia, Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) ipo Tamisemi.
Waziri wa Tamisemi aliyeteuliwa ni Profesa Riziki Shemdoe akiwa na naibu waziri, Reuben Kwangila atakayeshughulikia elimu na Dk Jafar Rajab Seif wa afya.
