Tabora. Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora linamshikilia Hadija Jimmy (39), mkazi wa Manispaa ya Tabora, kwa tuhuma za kujiteka ili kujipatia fedha za matumizi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Jumatatu, Novemba 17, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao, amesema kuwa mwanamke huyo anadaiwa kujiteka kutokana na kudai kuwa baba wa mtoto wake hampi fedha za matumizi, hatua inayoshukiwa kuwa na madhumuni ya kupata fedha kwa njia isiyo halali.
“Tunamshikilia mtuhumiwa huyu kwa sababu ya kutengeneza mazingira ya kwamba ametekwa ili baba mtoto wake atume hela ambazo ametaja ili aachiwe huru na kweli fedha zilitumwa na akarudi nyumbani,” amesema kamanda.
Kamanda Abwao amesema kuwa wengine wanaoshikiliwa ni Vitus Joseph na Ashura Swalehe, ambao wanatuhumiwa kuhusika katika kuunda mazingira yaliyopelekea tukio la utekaji.
“Wamefanikiwa kweli kudokeza au kupokea fedha zinazofikia zaidi ya Sh1 milioni, zilizotumwa na baba wa mtoto wa mtuhumiwa Hadija Jimmy,” amesema.
Aidha, Ashura, ambaye ndiye alimuhifadhi na kumtafutia mtekaji, amesema kuwa Hadija alifika nyumbani kwake na kumlalamikia kwamba baba wa mtoto wake hampi fedha za matumizi.
Kwa mujibu wa Ashura ni kwamba Hadija alitaka kudanganya kwamba ametekwa ili kupata fedha zinazohitajika ili aachiwe na watekaji.
“Mimi huyu dada ni wifi yangu, kwa hiyo alikuja kwangu akinishirikisha kuwa anataka kudanganya kwamba ametekwa ili kupata fedha za matumizi, kwa sababu baba wa mtoto wake hampi kiasi cha kutosha.
“Ndipo nikamtafutia kaka mmoja anayeitwa Vitus. Wakaongea naye na wakakubaliana, kisha walimpigia baba wa mtoto wake, ambaye aliweka malipo ya awali ya Sh500,000 na baadaye akamalizia Sh800,000,” amesema Ashura.
Kwa upande wake, Emmanuel Peter, baba wa mtoto wa Hadija Jimmy, aliyedaiwa kutekwa, amesema kuwa alifika nyumbani kwa mama wa mtoto wake lakini hakumkuta.
Hata hivyo, Peter amesema siku iliyofuata, mama wa mtoto wake alimpigia simu akidai kuwa ametekwa na kumtaka atume Sh2 milioni ili aachiwe huru. Peter alitafuta fedha hizo na akazituma, na baadaye mama wa mtoto wake alirudi nyumbani.
“Yaani mimi nilivyofika nyumbani kwake hayupo nikatulia tu lakini kesho yake akanipigia simu akasema ametekwa yupo kwenye jumba kubwa lililopauliwa tu halina milango wala madirisha, hivyo nitume hizo hela ili aachiwe huru, katika muda huohuo akanyang’anywa simu nikasikia mwanaume anasema atume fedha au tukumalize, sasa mimi ikabidi nitume hela kweli kwa sababu yule alikua na mtoto wangu mdogo, kumbe ni uongo tu,” ameeleza Peter.
