Waziri wa vijana ni nani na yapi yanamsubiri?

Dar es Salaam. Siku tatu baada ya Rais Samia Suluhu kuahidi kuunda wizara mahususi ya vijana, ametimiza hilo huku akimteua Joel Nanauka kuwa waziri wake wa kwanza.

Katika hotuba yake ya kuzindua Bunge la 13, Rais Samia Suluhu Hassan alisema kwa kuwa zaidi ya asilimia 60 ya watu nchini ni vijana, Serikali itaweka kipaumbele kwenye sera na programu zitakazopanua fursa za kiuchumi, kutengeneza kazi na ajira, kuongeza wigo wa hifadhi za jamii, na kuwajengea kesho iliyo bora zaidi.

Alisema lengo ni kuhakikisha vijana wanapata nafasi ya kushiriki katika kujenga mustakabali mwema wa Taifa letu. “Tutaweka kipaumbele kwenye ushirikishwaji wa vijana katika masuala ya maendeleo yao. Natambua kumekuwa na majukwaa mengi ya kuwafikia vijana, ila bado shughuli zao zinafifishwa na masuala ya kisiasa, na majukwaa hayo kupoteza malengo na mvuto kwa vijana.

“Mimi na wenzangu tumefikiria kuwa na wizara kamili itakayoshughulika na mambo ya vijana, badala ya kuwa na idara ndani ya wizara yenye mambo mengi,” alisema Rais Samia.

Aidha, alisema anafikiria kuwa na washauri wa masuala ya vijana ndani ya ofisi yake. Jambo jingine aliloliahidi kulitekeleza ndani ya siku 100 za awali za kazi ni kuongeza mitaji kwa ajili ya shughuli za kiuchumi za vijana na wanawake kwa kutenga Sh200 bilioni.

Kauli hizo, na hali ya mtanziko iliyokuwepo kutokana na maandamano yaliyoibua vurugu siku ya uchaguzi Oktoba 29 na siku zilizofuata, kundi la vijana likitajwa kuongoza, zilifanya wengi kusubiri kwa hamu kuundwa kwa wizara hiyo lakini pia kujua atakayeiongoza pamoja na majukumu yaliyoko mbele yake.

Akizungumzia uundwaji wa wizara hiyo, mchambuzi wa siasa na wakili Dk Onesmo Kyauke amesema tatizo kubwa la vijana ni ajira, kwani wanamaliza vyuo na hata wakiambiwa wajiajiri ni ngumu kwa sababu hawana mitaji na uzoefu.

“Kujiajiri si kitu rahisi, hili ndilo linapaswa kufanyika. Ilani ya CCM imezungumzia kupanua sekta ya kilimo, ufugaji, madini na viwanda, hivyo anapaswa kufanya kazi na wizara nyingine ili kuhakikisha sekta ya ajira inapanuka. Vijana wakibaki bila ajira, ikitokea kitu kama maandamano, hawana cha kupoteza,” amesema.

Pia amesema ni vyema kuwepo utamaduni wa kuandaa mijadala kwani suluhisho la vitu vingi linapatikana katika majadiliano.

“Tatizo kubwa ni kufunga wengine midomo na kuwazuia kutoa maoni yao na kuacha watu wachache bila suluhisho,” amesema.

Mtaalamu wa saikolojia na mwezeshaji, Charles Nduku amesema eneo kubwa ambalo Nanauka anapaswa kulishughulikia ni kubadili mtazamo wa vijana juu ya wanavyotazama fursa na kuwaonyesha vitu vya kufanya, kwani Tanzania ni tajiri, lakini vijana wanakosa maarifa.

“Huku utajiri upo, lakini mtazamo uliopo ni kuwa vijana wanatakiwa wakimaliza vyuo wavae suti waingie ofisini. Kwa sababu ni kijana na amekuwa akifanya kazi hii kwa muda mrefu, nadhani anajua namna ya kufanya, hususani kwa kubadili mitazamo yao,” amesema Nduku.

Uwezeshaji wa vijana na namna wanavyoweza kuifikia elimu ya vitendo ni jambo muhimu analopaswa kulisimamia ili kuhakikisha uwekezaji mkubwa unafanyika ili vijana wawezeshwe kujiajiri na kuajiri wengine.

Mtaalamu wa uchumi, Oscar Mkude amesema vijana sasa wako katika ari ya kupata mapinduzi, ikimaanisha yanahitajika mageuzi ya hali ya juu kwani yale yanayoendelea yanawafanya kuwa na kiu ya kupata mtu wa kuwasikiliza jambo ambalo wamekuwa hawalipati.

Hata hivyo, jambo kubwa kwa sasa ni vijana kuhitaji fursa za kiuchumi ili waweze kutumia muda wao vizuri lakini sasa wamejikuta katika kazi zisizokuwa na staha kwani fursa zinazopatikana katika kazi nzuri ni chache.

Amesema utengenezaji ajira ni suala pana na linagusa wizara mbalimbali ikiwemo kuwezesha uwekezaji, kuajiri wengine na kujiajiri kwani watu wenye njaa na wanaoona mambo yao hayaendi huwa ni hatari.

“Kundi la vijana ni kubwa na linaweza kuendelea kuwa hivi kwa kipindi kirefu kidogo, hivyo wizara inapaswa kuwa na majibu ya muda mfupi na mrefu ili kuhakikisha suluhisho linakuwa endelevu,” amesema.

Joel Nanauka (alizaliwa Mtwara, Julai 4, 1983) ni mhamasishaji maarufu, mwandishi wa vitabu, msomi aliyebobea katika masuala ya maendeleo na diplomasia ya uchumi.

Anasifika kwa kufundisha uongozi na kutoa hotuba na semina zinazolenga kuwawezesha watu binafsi na taasisi kufikia malengo yao.

Amejijengea sifa kama mmoja wa wazungumzaji mahiri kwenye majukwaa mbalimbali, akitoa maarifa kuhusu mafanikio, uongozi, na ukuaji binafsi. Kupitia majukwaa ya Youtube, Instagram na Facebook, Nanauka ni miongoni mwa vijana wenye ushawishi katika mitandao ya kijamii, akishiriki maudhui ya kuhamasisha na kuelimisha maelfu ya wafuasi wake.

Safari yake ya elimu ilianza Mtwara, ambako alihitimu darasa la saba mwaka 1992. Baadaye alichaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari ya Vipaji Maalumu Kibaha (Kibaha Secondary School), aliposoma kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita.

Mwaka 2002 alipata mafanikio makubwa katika mtihani wa kidato cha nne, akiwa miongoni mwa wanafunzi bora kitaifa kwa kupata Alama A katika masomo tisa kati ya 10, hatua iliyomwezesha kuendelea na masomo ya juu kwenye shule hiyo hiyo.

Mwaka 2005 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusomea Shahada ya Biashara na Uongozi. Baadaye alisomea Stashahada ya Juu ya Diplomasia ya Uchumi (Postgraduate Diploma in Economic Diplomacy) na kisha kupata Shahada ya Uzamili katika Maendeleo na Uhusiano wa Kimataifa (International Cooperation and Development).

Mwaka 2024, Nanauka alitunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu katika Uongozi na Usimamizi wa Biashara (Honorary PhD in Leadership and Business Management) na Chuo Kikuu cha Veridian, kilichopo Atlanta, Georgia, Marekani.

Katika utendaji wake, amewahi kutajwa miongoni mwa vijana 100 wenye ushawishi mkubwa barani Afrika, kutokana na mchango wake katika elimu ya uchumi na uongozi kupitia majukwaa mbalimbali, ikiwemo mitandao ya kijamii na machapisho ya vitabu.

 Aidha, amewahi kuajiriwa katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), akitoa mchango katika masuala ya maendeleo ya jamii.

Nanauka pia ni mshindi wa Tuzo ya I-Change Nations, inayotolewa na taasisi ya ICN ya Marekani, kutambua juhudi zake za kuleta mabadiliko chanya kwa watu nchini Tanzania.

Mbali na hilo, ni mwanzilishi wa Joel Nanauka Foundation, shirika lisilo la kiserikali lenye maono ya kuboresha ubora wa maisha kwa watu wasio na fursa, kupitia mipango endelevu. Shirika hilo limejikita katika kutekeleza miradi inayolenga kushughulikia mahitaji ya haraka ya jamii na kuinua ustawi wa makundi mbalimbali.