Morogoro. Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA), kwa ushirikiano na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, imeandaa maonyesho makubwa ya kibiashara yatakayofanyika kwa siku 10 kuanzia Novemba 20 hadi 30 mwaka huu katika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Maonyesho haya yatakutanisha wadau kutoka sekta za biashara, viwanda na kilimo, na yatatoa fursa maalumu kwa washiriki kuonyesha bidhaa zao, huduma, pamoja na ubunifu mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Novemba 17, 2025 mjini hapa, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amesema kuwa maonyesho hayo ni hatua muhimu katika kuchochea maendeleo jumuishi ya uchumi kwa kuwakutanisha wafanyabiashara, wawekezaji, taasisi za serikali na umma kwa ujumla.
Alibainisha kuwa kaulimbiu ya maonyesho hayo, “Kukuza Ujasiriamali, Ubunifu na Uwekezaji wa Kimkakati,” inaakisi dhamira ya kuhamasisha ujasiriamali, kuimarisha ubunifu, na kuendeleza ushirikiano miongoni mwa wadau wa maendeleo, ili kuongeza kasi ya ukuaji wa kiuchumi katika mkoa na Taifa kwa ujumla.
Malima ameongeza kuwa maonyesho haya yatachochea maendeleo ya uchumi wa mseto, na yatakuwa sehemu ya juhudi za Taifa kufikia lengo la kuwa na uchumi shindani na wa kipato cha kati.
Amesisitiza kuwa Tanzania inahitaji kujenga mazingira ya kuhamasisha uwekezaji na ubunifu ili kufikia malengo ya pato la Taifa la dola za Marekani trilioni moja na wastani wa pato la mtu mmoja la dola 7,000 kwa mwaka.
Amesisitiza kuwa maonyesho hayo ni hatua muhimu katika kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, ambayo inalenga kujenga uchumi wa kipato cha kati unaotegemea uzalishaji na mseto wa shughuli za kiuchumi.
Amesema kuwa ushiriki wa wadau mbalimbali ndio msingi wa kufanikisha mabadiliko hayo.
“Maonyesho haya ni sehemu ya mikakati ya mkoa wetu wa kukuza uchumi na kuongeza nafasi za ajira kwa vijana na wanawake. Ni nafasi ya kuonyesha maendeleo ya mkoa wetu katika sekta za biashara, viwanda, na kilimo,” amesema Malima.
Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Morogoro, Muadhini Mnyanza, amesema kuwa maonyesho hayo yatatoa fursa kwa wafanyabiashara, wakulima na wenye viwanda kuonyesha bidhaa zao, kubadilishana maarifa na kujenga mitandao madhubuti ya kibiashara.
Mnyanza ameongeza kuwa Mkoa wa Morogoro unajivunia kuwa na sekta muhimu za uchumi, ikiwemo kilimo, viwanda na biashara ambazo zimeendelea kuzalisha bidhaa zenye ubora wa kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Amesema hatua hiyo inaonyesha uwezo mkubwa wa mkoa huo katika kuchochea maendeleo ya viwanda na kuongeza thamani ya mazao.
“Haya maonyesho yatakuwa ya kipekee na endelevu, kwani tutakuwa tukifanya kila mwaka. Hii ni fursa ya kipekee kwa washiriki kupata ujuzi, kujitangaza, na kufungua fursa za kibiashara,” amesema Mnyanza.
Kwa upande Ofisa Mwandamizi wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Grace Makoye, amesema kuwa maonyesho hayo yatatoa fursa kwa wajasiriamali na viwanda vidogo kujifunza, kuonyesha bidhaa zao, na kujitangaza kwa umma.
Amesema kuwa washiriki watapata nafasi ya kujifunza kuhusu fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotolewa na taasisi za Serikali, ikiwemo Wakala wa Viwango Tanzania (TBS), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) pamoja na benki, ambazo zote zitashiriki katika maonesho hayo.
“Washiriki watapata fursa ya kujijenga kibiashara na kukuza biashara zao kwa kushirikiana na taasisi zinazowasaidia. Ni tukio muhimu ambalo litaimarisha ushirikiano miongoni mwa wadau wa maendeleo,” amesema Makoye.
