Dar es Salaam. Wanasiasa saba waliokuwa mawaziri katika muhula wa kwanza wa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, hawatakuwa sehemu ya Baraza la Mawaziri la sasa, baada ya kuwekwa kando.
Kati ya wanasiasa hao, wapo waliohudumu katika awamu mbalimbali za Serikali, huku wengine wakiwa na historia ya kumwagiwa sifa na mkuu huyo wa nchi, lakini hiyo haikutosha kuteuliwa tena.
Wanasiasa hao ni Jenista Mhagama, Dk Selemani Jafo, Dk Doto Biteko, Dk Damas Ndumbaro, Hussein Bashe, Dk Pindi Chana na Innocent Bashungwa.
Hatua hiyo inawafanya saba hao, kubaki na wadhifa wa ubunge baada ya kushinda nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.
Wachambuzi wa siasa wanasema kutemwa kwao ni ishara ya kushughulikiana ndani ya chama kwa upande mmoja, lakini kwa upande mwingine mkuu wa nchi ameamua kuleta sura mpya katika Serikali yake.
Kati ya saba hao, wapo wanasiasa waliohudumu kitambo katika wizara, akiwamo Jenista Mhagama, aliyeanza kuhudumu tangu enzi za Jakaya Kikwete na hakuwahi kutemwa hadi wakati wa kipindi cha kwanza cha awamu ya sita chini ya Samia.
Mbunge huyo wa Peramiho mkoani Ruvuma tangu mwaka 2005 akitokea ubunge wa viti maalumu mwaka 2000, kwa mara ya kwanza alipata uteuzi kwa mara ya kwanza na Kikwete kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Januari 2014.
Kwa mara ya kwanza, aliingia katika Baraza la Mwaziri akiwa waziri kamili Januari, 2015 alipoteuliwa tena na Kikwete kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu.
Alipoingia hayati Rais John Magufuli madarakani mwaka huohuo, Jenista alikuwa sehemu ya baraza lake la mawaziri akimteua kuendelea na wadhifa aliokuwa nao enzi za Kikwete.
Tangu enzi hizo, Jenista hakuwahi kutoka nje ya baraza la mawaziri, zaidi ya kuhamishwa katika wizara mbalimbali ikiwamo ya Sera, Bunge na Uratibu na baadaye Wizara ya Afya, wadhifa aliohudumu hadi kilipomalizika kipindi cha kwanza cha Rais Samia.
Ukiacha uandamizi wizarani, Jenista aliwahi kumwagiwa sifa hadharani na Rais Samia alipofanya ziara Peramiho mkoani Ruvuma Septemba mwaka 2024.
“Shukrani kubwa zaidi kwa tumbo lililomtoa Jenista Mhagama, nawashukuru wana Peramiho na tumbo lililomtoa Jenista. Huyu kwa lugha rahisi namwita kiraka changu. Pale kwenye upungufu, namtoa Jenista huku namuweka huku na kote nakumweka niwahakikishie anafanya kazi nzuri,” alisema Rais Samia.
Tofauti na Jenista, Jafo yeye alianza kuhudumu wizara kwa nafasi ya unaibu waziri katika Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), mwaka 2015 alipoteuliwa na hayati Magufuli.
Baadaye mwaka 2017 hayati Magufuli, alimteua kuwa waziri wa wizara hiyo, kabla ya mwaka 2021 kuhamishiwa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kwa wadhifa huohuo.
Alipoingia Rais Samia katika muhula wake wa kwanza Machi 19, 2021 baada ya kifo cha Magufuli, kwenye mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri, alimteua mbunge huyo wa Kisarawe, kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, wadhifa aliohudumu hadi mwishoni mwa muhula wa kwanza Samia na sasa ametemwa.
Bashe amehudumu katika nafasi ya ubunge wa Nzega Mjini, Mkoa wa Tabora tangu mwaka 2015 na mwaka 2017 hayati Magufuli alimteua kuwa Naibu Waziri wa Kilimo na baadaye mwaka 2019 alimpandisha hadi kuwa waziri kamili wa wizara hiyo.
Bashe naye ni miongoni mwa mawaziri waliokuwa machachari waliowahi kumwagiwa sifa na wakuu hao wa nchi.
Katika ukurasa wake wa Instagram, Bashe ameshukuru Rais Samia kwa kuaminiwa katika kipindi chote alichotumikia katika nafasi hiyo.
“Salaam ndugu zangu. Natumia nafasi hii kumshukuru Allah kwa kila jambo na kwa baraka zake katika safari yangu ya utumishi. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt @samia_suluhu_hassan kwa imani kubwa aliyonionyesha katika kipindi chake cha kwanza cha uongozi kama Naibu Waziri, na baadae kuniteua kama Waziri wa Kilimo.
“Ni heshima niliyothamini kwa moyo wangu wote, na ninaendelea kuwa mwenye shukrani kwa nafasi hiyo ya kuwatumikia Watanzania…Nawashukuru pia watumishi wote wa Wizara ya Kilimo kwa ushirikiano wa hali ya juu mlionipa katika kipindi cha miaka sita. Nawatakia heri na fanaka katika kuendelea kutekeleza majukumu yenu ya kuwatumikia Watanzania. Asanteni sana.”
Dk Biteko hana historia ndefu katika siasa, kwani ubunge aliupata mwaka 2015 katika Jimbo la Bukombe mkoani Geita na mwaka 2017 Magufuli alimteua kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini.
Miaka miwili baadaye, alimteua kuwa waziri kamili wa wizara hiyo hadi mwaka 2020. Katika kipindi chake cha pili, Magufuli alimteua tena Biteko kuwa Waziri wa Madini.
Alipoingia Rais Samia aliendelea kumwacha Dk Biteko katika wadhifa huo hadi mwaka 2023 alipomteua kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.
Hatua hiyo ya Dk Biteko inamfanya kuwa mwanasiasa wa tatu kushika nafasi ya Naibu Waziri Mkuu, tangu iliposhikwa na Dk Salim Ahmed Salim mwaka 1984 na baadaye mwaka 1991 ukashikwa na hayati Augustine Mrema.
Mbunge huyo wa Karagwe mkoani Kagera tangu mwaka 2015, alianza kwa kuteuliwa na Magufuli kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara mwaka 2019.
Baadaye mwaka 2020 alimteua kuwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo nafasi aliyoendelea kuhudumu hadi alipoingia madarakani Rais Samia.
Mwaka 2022, Rais Samia alimhamishia Tamisemi, kisha Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na baadaye Wizara ya Ujenzi na wadhifa wake ukatamatikia katika Wizara ya Mambo ya Ndani.
Bashungwa ndiye mwanasiasa mwenye rekodi ya kuwahi kuhudumu katika wizara nyingi na nyeti kwa muda mfupi.
Bashungwa amesema:“Ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kipindi tulichopata kuwatumikia Watanzania katika nafasi mbalimbali. Naomba kumshukuru Rais na Amiri Jeshi Mkuu, kwa fursa adimu uliyonipa katika vipindi mbalimbali kuwatumikia Watanzania.”
“Naomba pia, kuwashukuru wananchi na matajiri wangu wananchi wa Jimbo la Karagwe kwa ushirikiano na imani kwangu. Sasa nimepata muda wa ziada wa kukaa jimboni ili kazi iendelee na kwa kasi zaidi. Kazi na Utu, Tunasonga Mbele.”
Mbunge huyo wa Songea Mjini, kwa mara ya kwanza aliteuliwa na Magufuli mwaka 2018 kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na mwaka 2020 akateuliwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.
Mwaka 2022, aliteuliwa na Serikali ya Rais Samia kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na baadaye mwaka 2023 akateuliwa kuwa Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo kisha akarudishwa tena Wizara ya Katiba na Sheria wadhifa uliokoma sasa.
Dk Ndumbaro amemshukuru Rais Samia kwa kumuamini kwa nafasi hizo kwa kuwa zimempa heshima kubwa kwangu na nafasi ya kuwahudumia wananchi wetu kwa moyo, uadilifu na kujitolea.
“Nawashukuru sana wananchi wote, viongozi wenzangu, watumishi wa umma na wadau mbalimbali ambao tumefanya kazi kwa ukaribu. Tumeshirikiana kwa bidii kutekeleza majukumu ya kuwatumikia Watanzania na kuleta maendeleo katika sekta tulizokuwa tukisimamia.
“Ninaendelea kuwa mtumishi wa wananchi, mzalendo na mshiriki katika jitihada za kuijenga Tanzania tunayoitamani. Ninawapongeza na kuwatakia kila la heri wote walioaminiwa na kuteuliwa katika kuwahudumia Watanzania,” amesema kupitia Instagram.
Mwaka 2021, Dk Pindi aliteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na baadaye mwaka 2023 akateuliwa kuwa Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka 2024.
Dk Chana ni miongoni mwa makada waandamizi wa CCM na aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu miaka ya 2000. Pia, amewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Kenya.
Mwananchi, imezungumza na wadau mbalimbali juu ya vigogo hao kuwekwa kando. Mmchambuzi wa siasa Profesa Mohamed Makame amesema,”hakuna kiongozi mwenye hati maliki ya nafasi ya uongozi wa kuteuliwa, uteuzi huangalia nani anahitajika kwa wakati gani.”
Amesema aliyekuwa waziri awamu iliyopita si lazima aendelee kuwa na nafasi hiyo kwa kuwa, vipaumbele vya Serikali vinabadilika.
Mchambuzi huyo wa siasa amesema kuachwa kwao katika baraza jipya haimaanishi moja kwa moja kuwa vigogo hao hawakuwajibika vema awamu iliyopita bali hawajakidhi tu mwelekeo wa Serikali anayoitaka Rais Samia.
“Matamanio ya wananchi siku zote huwa ni kuona sura mpya kila mabadiliko ya Serikali yanapotokea, hivyo huenda Rais ameamua kufanya hivyo ili kuleta sura mpya ya Serikali yake,” amesema.
Kuenguliwa kwa wanasiasa hao, amesema kunawapa mtihani wateule wapya kukumbana nao bungeni katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Mtihani uliopo kwa waliopata nafasi hizo ni kwamba, wanakwenda kusimamiwa na hao wakongwe katika utekelezaji wa majukumu yao bungeni,” amesema.
Kwa upande wake, Dk Paul Loisulie amesema kuachwa kwa vigogo hao kuna maana nyingi katika siasa, mojawapo ikiwa ni ishara ya kuwepo kwa mpasuko ndani ya chama chao.
“Mchakato wa uchaguzi kwa kawaida huibua mambo mengi sana yakiwamo makundi ndani na nje ya chama, hii huenda ni ishara ya kushughulikiana ndani ya chama,” amesema.