Siri za kuijenga Tanzania ya teknolojia

Katika ulimwengu wa sasa unaotawaliwa na teknolojia na ubunifu, vijana wengi duniani wanazidi kuthubutu kuanzisha miradi inayobadili maisha yao na jamii kwa ujumla.

Katika orodha hiyo, yumoJumanne Mtambalike, Mkurugenzi Mtendaji wa Sahara Ventures, kampuni ya ubunifu, teknolojia na ujasiriamali yenye makao yake jijini Dar es Salaam.

Katika mahojiano haya maalumu, Mtambalike anafafanua changamoto, fursa na mustakabali wa maendeleo ya teknolojia nchini Tanzania.

Swali: Wewe ni kati ya vijana waliothubutu kujiajiri kwa kuanzisha kampuni m mahiri ya teknolojia. Kwa nini wahitimu wengi wanakosa uthubutu kama wako?

Jibu: Kwanza ni muhimu kuelewa kuwa sisi ni kizazi cha pili cha wafanyabiashara nchini, baada ya kizazi cha kwanza cha kina Mzee Mengi, Shirima na wengine waliothubutu kuingia kwenye biashara kubwa.

Wazazi wetu wengi walikuwa watumishi wa umma, wakulima au wanasiasa. Tulikosa mifano hai ya mjomba au baba ambaye alianza biashara na akaijenga hadi ikafanikiwa. Kwa hiyo vijana wengi wanajikuta wakifuata nyayo za wazazi, wakitamani kuajiriwa badala ya kujiajiri.

Changamoto nyingine ni hofu ya kushindwa. Jamii yetu inaona kushindwa kama doa, tofauti na mataifa mengine ambayo huchukulia kushindwa kama sehemu ya kujifunza. Hivyo vijana wengi wanahofia kujaribu kwa sababu wakifeli wanaogopa kuchekwa.

Pia mazingira ya kiuchumi hayajawasaidia vijana wengi kuanza biashara. Ukosefu wa mitaji, ugumu wa kupata mikopo, mazingira ya kodi yasiyowezesha biashara changa, na mfumo wa elimu usioandaa vijana kivitendo, yote haya yanapunguza ujasiri wa kuanza safari ya ujasiriamali.

Na zaidi, ukosefu wa watu wa mfano katika jamii zetu ni tatizo. Vijana wanahitaji kuona mfano wa mtu aliyefanikiwa katika mazingira magumu kama yao ili nao waamini kuwa inawezekana.

Swali: Unadhani aina ya elimu inayotolewa nchini ina mchango katika kuwakosesha wahitimu uthubutu wa kubuni mawazo mapya hasa ya kujiajiri?

Jibu: Kwa mtazamo wangu, tatizo si mtalaa pekee. Silabasi za vyuo vyetu hazina tofauti kubwa na zile za nje. Tatizo ni mazingira yanayozunguka mfumo wa elimu.

Katika nchi zilizoendelea, vyuo vinashirikiana kwa karibu na kampuni za teknolojia au viwanda. Wanafunzi wanapata fursa za vitendo kupitia ‘internship’ au miradi ya pamoja. Hapa kwetu vyuo vingi vimejitenga na sekta binafsi.

Mfano, ukienda Marekani chuoni Stanford, unakuta kampuni kubwa kama Microsoft au Google zikishirikiana na wanafunzi. Hapa (anataja jina la chuo maarufu nchini) hakuna hata kampuni kubwa jirani inayofanya kazi moja kwa moja na wanafunzi.

Kwa hiyo suluhisho ni kuunda mfumo wa elimu unaounganisha chuo, Serikali na sekta binafsi. Hapo ndipo kijana atapata ujuzi wa vitendo, ataweza kufikiri kwa ubunifu, na hatimaye kujiajiri. Mfumo mzima kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu lazima ubadilike.

Swali: Umekuwa kinara kwenye Tehama, nini kinakwamisha Tanzania kukosa wabunifu kama wale waliobuni mitandao ya kijamii na huduma nyingine za kiteknolojia zinazotamba duniani?

Jibu: Sidhani kama tunakosa wabunifu. Tuna vijana wengi wazuri kama Benjamin Fernandes, Anthony Mendes, Edwin Bruno, na wengine wengi. Wengine wameshauza kampuni zao kwa mamilioni ya dola. Mimi mwenyewe kupitia Sahara Ventures nimeweza kuajiri vijana wengi nchini.

Kinachotakiwa ni kujenga mfumo unaounga mkono ubunifu, sera, sheria, na mazingira ya kifedha yanayowezesha vijana kuanzisha na kukuza biashara zao.

Tunahitaji kuweka mkazo kwenye kuibua kampuni ndogondogo na za kati nyingi badala ya kungojea kampuni kubwa chache. Kama tukitengeneza kampuni 10,000 zinazoweza kuajiri watu 5,000 hadi 10,000, hapo tutaona matokeo makubwa zaidi.

Nafurahi kuona Serikali sasa inaandaa sera ya Startup Tanzania (kampuni changa) kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia, lakini bado tunapaswa kwenda mbali zaidi ili kufikia malengo ya mwaka 2040  kuwa na vijana 100 wenye kampuni za kati zinazoshindana kimataifa.

Swali: Unaridhika na utoaji wa elimu ya Tehama nchini?

Jibu: Kuna changamoto kubwa, hasa kutokana na idadi ya wanafunzi. Tanzania ina zaidi ya wanafunzi milioni 12, idadi inayokaribia watu wote wa Rwanda. Ukiamua kuwapa wote vitabu au kompyuta, ni mzigo mkubwa sana kwa Serikali, hivyo haiwezekani.

Lakini kuna hatua nzuri. Sasa kuna mtalaa unaoruhusu masomo ya Tehama kuanzia shule za sekondari, jambo ambalo sisi tulilikosa tulipokuwa shule.

Changamoto kubwa ipo vyuoni. Vyuo vingi ni vya “second generation” vimejikita katika tafiti na masomo ya nadharia, si ubunifu na ujasiriamali. Hivyo unakuta wanachofundisha ni historia ya kompyuta badala ya teknolojia mpya zinazotumika sasa.

Vyuo vikuu vinapaswa kushirikiana na sekta binafsi, kuhimiza ubunifu, na kuanzisha programu za kusaidia wanafunzi kubadilisha mawazo yao kuwa bidhaa halisi.

Swali: Ni kwa namna gani wabunifu wachache wanaojitokeza kwenye Tehama kama wewe wanaenziwa na hata kupewa nafasi nchini?

Jibu: Suala si kuenziwa kwa maneno, bali kupewa fursa. Tunahitaji sera na mifumo ya fedha ya kiserikali itakayowasaidia vijana wanaofanya kazi kwenye teknolojia.Serikali inapaswa kufungua masoko ya ndani na ya Afrika Mashariki kwa wabunifu wa Tanzania, kwa sababu matatizo yetu yanafanana na ya jirani zetu.

Lakini pia lazima mfumo wa ununuzi wa Serikali utoe kipaumbele kwa kampuni za vijana wazalendo. Na mwisho, mazingira ya kodi na kisheria lazima yawe rafiki kwa biashara changa.

Swali: Uliwahi kuwa sehemu ya Buni Hub, kituo cha kuendeleza wabunifu. Ni mafanikio gani unayajivunia?

Jibu: Ndiyo, nilijiunga na Buni Hub mwaka 2012 nikiwa sina wazo lolote la maana. Nilikaa pale hadi 2015, nikaajiriwa, na baadaye nikawa meneja. Tulisaidia vijana wengi kuanzisha kampuni ambazo leo zinaajiri Watanzania wengi.

Buni ilikuwa mfano bora wa kuonyesha namna Serikali inavyoweza kuanzisha kituo cha ubunifu kinachoweza kuleta matokeo makubwa. Hadi leo, kampuni nyingi za teknolojia zilizopo nchini zimetoka pale.

Kwa hiyo mafanikio ya Buni ni makubwa, na yamekuwa msingi wa kuanzishwa kwa “innovation hubs” (vituo vya ubunifu) nyingi nchini.

Swali: Nini kinakwamisha wanafunzi wa Kitanzania kutosoma masomo ya sayansi, uhandisi, hesabu na Teknolojia (STEM)?

Jibu: Kwanza ni gharama. Masomo ya sayansi yanahitaji maabara, vifaa na walimu waliobobea. Shule nyingi hasa vijijini hazina rasilimali hizo, hivyo wanafunzi wanalazimika kusoma masomo ya sanaa.

Pili ni ukosefu wa walimu. Wakati ninasoma, tulilazimika kwenda shule nyingine kama za pale Mchikichini kutafuta walimu wa fizikia au kemia kwa sababu shuleni kwetu hawakuwepo.

Tatu ni programu maalum. Shule chache kama Ilboru, Mzumbe na Kibaha ndizo zinazotoa programu bora za STEM. Kwa hiyo si rahisi kila mtoto kupata fursa hizo.

Na mwisho, teknolojia kama robotics au Akili Unde zinahitaji uwekezaji mkubwa. Kwa nchi zinazoendelea kama yetu, tunapaswa kuwa wabunifu katika njia zetu za kufundisha badala ya kunakili mifumo ya mataifa tajiri.

Swali: Unaamini ujio wa elimu ya amali, itakuwa chachu ya wahitimu kujiajiri?

Jibu: Naamini sana. Elimu ya amali inaleta mapinduzi makubwa. Inawafanya vijana kuwa wabunifu, kufikiri kwa kina, na kujenga ujuzi wa kufanya kazi kwa vitendo.

Kupitia elimu hii, wanafunzi watajifunza kufanya kazi kwa ushirikiano, kuwa na mawasiliano mazuri, ubunifu na fikra tunduizi.

Hizi ndizo stadi zinazohitajika katika soko la ajira la kisasa. Watu wengi wana GPA (alama za matokeo vyuoni) nzuri lakini hawana uwezo wa kuwasiliana, kubuni au kutatua matatizo. Elimu ya vitendo italeta mabadiliko hayo.

Swali: Ni sahihi teknolojia kuwekwa chini ya Wizara ya Elimu?

Jibu: Kwa mtazamo wangu, hapana. Elimu ni sekta kubwa yenye changamoto zake. Ningependa kuona wizara maalum inayoshughulika na teknolojia, mawasiliano na mageuzi ya kidijitali kama ilivyokuwa zamani. Hiyo ndiyo njia bora ya kusukuma ajenda ya ubunifu na teknolojia mbele kwa kasi.

Swali: Sekta ya Teknolojia inaelezwa kuchechemea kwa kukosa taasisi imara za kuisimamia. Nini maoni yako?

Jibu: Tuna taasisi kama Costech inayojihusisha na utafiti na sasa imepanua majukumu yake hadi ubunifu. Pia kuna Tume ya ICT chini ya wizara husika.

Tatizo si taasisi zenyewe, bali ukosefu wa rasilimali. Tunahitaji kuongeza bajeti zao, kuwawezesha kuajiri wataalamu zaidi, na kutoa fedha za kutosha kufanikisha miradi ya ubunifu na kidigitali.

Kama tukiziimarisha taasisi hizi, tutaona matokeo makubwa katika ubunifu na maendeleo ya teknolojia nchini.

Swali: Unaiona wapi Tanzania kiteknolojia miaka 50 ijayo?

Jibu: Naiona Tanzania ikiwa kitovu cha teknolojia barani Afrika. Serikali inawekeza katika miundombinu ya kidijitali, vyuo vinaongezeka, na vijana wanaopenda teknolojia wanaongezeka.

Miaka 50 ijayo natarajia kuona mamilionea wengi wa Tehama, biashara kubwa za teknolojia, sera bora za ubunifu, na tafiti nyingi kutoka vyuo vyetu. Uwekezaji unaofanyika sasa utazaa matunda makubwa siku zijazo.

Swali: Tueleze kwa ufupi kuhusu elimu yako na maeneo uliyobobea.

Jibu:  Nilisoma Shule ya Msingi Forodhani (sasa St. Joseph), sekondari Azania, na kidato cha sita Loyola. Shahada yangu ya kwanza ni Computer Science and Electronics niliyosoma nchini India, na baadaye Postgraduate Diploma ya ICT Leadership nchini Ireland (DCU). Kwa kifupi, sijawahi kusoma masomo yasiyohusiana na kompyuta.