DB Lioness,  Fox Divas zimemaliza ‘bora liende’

TIMU za DB Lioness na Fox Divas za Tanzania, zimeshindwa kufika mbali katika mashindano ya Kanda ya Tano ya Kikapu Afrika (WBLA), zikiishia njiani kutokana na kutokuwa na maandalizi mazuri.

DB Lioness ambao ni mabingwa wa Ligi ya Kikapu Mkoa kwa Wanawake Dar es Salaam (WBDL), mwaka huu, huku Fox Divas wakiwa wababe mkoani Mara wameshindwa kufanya cha maana katika mashindano hayo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Nyayo Gymnasium uliopo Nairobi, Kenya.

Wababe wa mashindano hayo waliibuka kuwa APR ya Rwanda walioifunga Rwanda Energy Group (REG) kwa pointi 82-71 katika fainali.

APR iliyoundwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kimataifa ilionyesha imejiandaa  vizuri kwa kipindi kirefu pamoja na kusajili nyota wenye ubora mkubwa kutoka nje ya taifa hilo wakiwamo Msenegali Yacine Diop, Italee Lucas (Angola) na Mmarekani A’Lexxus Davis.

Tofauti na DB Lioness na Fox Divas ambazo maandalizi yalionekana ya zimamoto kulinganisha na timu zote zilizoshiriki mashindano hayo, mechi zilikuwa kali na kila timu ilionyesha kuutaka ubingwa.

KIKA 01

DB Lioness ilifanya maandalizi kwa kipindi kifupi na kuonekana imeenda kushiriki mashindano hayo kwa lengo la kupata uzoefu, ilhali Fox Divas ilichelewa kufanya mazoezi ya pamoja kutokana na kukosekana kwa baadhi ya wachezaji wake.    

Timu hiyo iliwakilishwa na wachezaji kutoka timu tofauti ambao ni Noela Uwendameno wa Jeshi Stars, Dina Mussa (Ukonga Queens), Mahewa Matewa (Tausi Royals) na baadhi ya nyota wa kikosi cha Orkweswa.

Fox Divas ilishika nafasi ya tano katika mashindano hayo ni baada ya kuifunga Zetech Sparks kutoka Kenya kwa pointi 67-56.

Akizungumzia ushiriki wa timu hizo katika mashindano hayo, msimamizi wa waamuzi  wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), Prosper Mushi alizitaka timu zinazopata nafasi ya kuwakilisha taifa kujiandaa mapema na kuwa na mkakati wa ushiriki unaoeleweka.

KIKA 02

“Siyo timu inajikusanya, inajipa moyo kwenda kuchukua kikombe. Nachosema ni ngumu kubeba kombe,” amesema Mushi.

Naye Victor Mwoka anayeichezea Dar City alizitaka timu za kikapu za wanawake nchini zisitegemee wachezaji kutoka nje ya nchi kwa kuwa kuna mastaa kibao wenye uwezo mkubwa waliopo katika timu za nyumbani.

“Si umeona wachezaji tegemeo wa kigeni kutoka DB Lioness waliocheza Ligi ya Kikapu ya Wanawake Mkoa wa Dar es Salaam (WBDL), walichezea timu zao katika mashindano hayo,” amesema, akizitahadharisha pia kuwa makini kwani miongoni mwa mastaa wa kike wa Afrika Mashariki inapofikia michuano ya kimataifa huchezea timu zao za asili. 

KIKA 04

KR-ONE YATOA VITISHO LA KWANZA

BAADA ya KR-One kuinyuka Crows kwa pointi 89-35 katika Ligi ya Kikapu ya Daraja la Kwanza Mkoa wa Dar es Salaam, kocha wa timu hiyo, Remy Zilinde ametamba kuziadhibu timu zote itakazokutana nazo.

Ligi hiyo inashirikisha timu 20 ikiwa inafanyika katika Uwanja wa Donbosco, Upanga.

Tambo za kocha huyo zimekuja baada ya ya timu yake kuonyesha kiwango bora katika mchezo huo na kuifanya kuwa na matumaini ya kushinda michezo mingine iwapo itaendeleza ubora iliokuwa nao katika mchezo huo.

Zilinde ajulikanaye kwa jina la Bwax, amesema ushindi huo ulitokana na usikivu wa wachezaji wake katika maelekezo aliyokuwa anawapa katika robo zote nne za mchezo.

“Licha  ya kila timu kutafuta nafasi kati ya tatu kucheza BDL (Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam) mwakani, naamini timu yangu itakuwa ni moja itakayopanda daraja,” amesema kocha huyo.

KIKA 03

KR-One iliongoza katika robo zote nne kwa pointi 28-8, 20-13, 15-14 na 26-20, ambapo mchezaji Felix Vatua wa timu hiyo aliongoza kwa kufunga pointi 23 akifuatiwa na Mohamed Issa aliyetupia 15.

Kwa upande wa Crows alikuwa Danieli Haule aliyefunga pointi 15 akifuatiwa na Hance Kinabo aliyefunga sita. Mchezo huo ni wa pili kwa timu hizo kucheza na katika mchezo wa kwanza KR-One iliifumua Leaders kwa pointi 73-63.

Katika mchezo mwingine uliochezwa uwanjani hapo, Venis iliishinda Kigamboni Heroes kwa pointi 70-43 huku DB VTC ikiifumua Kibada Riders kwa pointi 76-71. Timu tatu zitakazofanya vizuri katika ligi hiyo zitacheza BDL mwakani kuchukua nafasi za KIUT, Polisi na Mgulani JKT zilizoshuka daraja.

KIKA 05

TANGA QUEENS, DEEP SEA WABABE

KUFUATIA Bandari Queens kushindwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Kikapu Mkoa Tanga, kocha  wa timu hiyo, Riziki Mgude amesema kumetokana na kukosa muunganiko mapema katika mashindano hayo mwaka huu.

Bandari Queens ilifungwa na Tanga United Queens kwa pointi 35-29 katika fainali iliyofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani uliopo mjini Tanga.

Mgude aliliambia Mwanaspoti kuwa licha ya kutokuwa na muunganiko bora, pia wachezaji wao walicheza kwa kutofuata maelekezo aliyokuwa anayatoa.

“Niliwambia wacheze kwa mfumo naoutaka hawakunisikiliza. Wakaanza kucheza  wanavyotaka na baadaye timu iliweza kupoteana katika robo zote nne,” amesema Mgude.

Katika mchezo huo Tanga United Queens iliongoza katika robo zote nne kwa pointi 6-4, 10-9, 10-8 na 9-8, huku mchezaji Asha Rashidi akifunga pointi 9 akifuatiwa na Salma Kitunga aliyetupia 6. Kwa upande wa Bandari Queens alikuwa Mary Mwakapasa aliyefunga pointi 8 akifuatiwa na Gaudensia Kilamata aliyefunga 7.

Kwa wanaume Deep Sea ilitwaa ubingwa wa mkoa baada ya kuifunga Ngamiani Kings kwa pointi 57-50. Katika mchezo huo Ngamiani Kings ilianza kuongoza katika robo ya kwanza kwa pointi 18-13 huku Deep Sea ikiongoza zilizofuata kwa pointi 20-15, 14-9 na 10-8.

Mchezaji bora wa mashindano hayo upande wanaume alichaguliwa kuwa Juma Ally wa Deep Sea na upande wanawake alikuwa Asha Saidi wa Tanga Queens. Upande wa chipukizi wanawake alikuwa Salma Kitunga wa Tanga United Queens, huku kwa wanaume ni Brian John wa Ngamiani Kings.