Kocha TMA Stars asikilizia dirisha dogo

KOCHA wa TMA Stars inayoshiriki Ligi ya Championship, Habib Kondo amekiri kuwa kikosi chake kina upungufu baadhi ya maeneo hasa katika safu ya ushambuliaji akisema ndiyo linalompa kazi kubwa zaidi huku akitegemea dirisha dogo kulifanyia marekebisho.

Licha ya timu hiyo kucheza soka la kuvutia, lakini TMA Stars imeendelea kuwa butu mbele ya lango la wapinzani, hali iliyojidhihirisha kwenye kipigo cha bao 1-0 nyumbani dhidi ya Transit Camp kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo jijini Arusha.

Katika mechi tano za Ligi ya Championship ambazo imecheza msimu huu, TMA haijafunga zaidi ya bao moja ikianza na ushindi mechi tatu mfululizo wa 1-0 dhidi ya Bigman FC, Mbeya Kwanza FC na B19 FC, kisha 1-1 dhidi ya KenGold na kipigo cha 1-0 kutoka kwa Transit Camp.

Kondo alieza kuwa alijiunga na timu hiyo ikiwa imesalia wiki moja kabla ya ligi kuanza, hivyo hakupata muda mzuri wa kufanya maandalizi ya kutosha, ambapo alilazimika kuanza na safu ya ulinzi ambayo imezaa matunda kwani katika mechi hizo tano wameruhusu mabao mawili.

“Timu imekuwa na mapungufu mengi sana ambayo nasubiri dirisha dogo niweze kufanyia marekebisho ila kwa sasa nafanya kazi na wachezaji nilionao,”  alisema Kondo.

Alisema wamekuwa wakicheza vizuri, wanatawala mchezo, lakini changamoto kubwa imekuwa ni kubadilisha hizo nafasi kuwa mabao, lakini anaendelea kufanyia kazi eneo hilo la ushambuliaji.

Akizungumzia kipigo kutoka kwa Transit Camp, Kondo alisema kosa la kutocheza kwa umakini kona ndilo lililowagharimu.

“Kupoteza si jambo jema, lakini ni sehemu ya mchezo, tulichelewa kufanya ulinzi wa kutosha kwenye kona wakapata nafasi, baada ya hapo tulitawala mchezo, lakini tukashindwa kutengeneza bao,” alisema kocha huyo.

Kondo ambaye amewahi kuzinoa klabu kadhaa hapa nchini ikiwemo KMC FC na Mtibwa Sugar, anaamini mabadiliko anayofanya yatairudisha timu kwenye ushindi kuanzia mechi ijayo dhidi ya Songea United.

Katika msimamo wa Ligi ya Championship msimu hu, TMA Stars inashika nafasi ya saba ikiwa na alama 10, baada ya kushinda mechi tatu, sare moja na kupoteza moja, ikifunga mabao manne na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili.