BAADA ya kumaliza majukumu yake ndani ya Taifa Stars, kocha Miguel Gamondi ameungana na kikosi cha Singida Black Stars kwa ajili ya kuendelea na maandalizi ya mechi ya kwanza ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CR Belouizdad kutoka Algeria huku akitaja sababu za kuwawahi Waarabu hao.
Singida Black Stars inatarajiwa kuvaana na miamba hiyo ya Algeria Jumamosi, Novemba 22, 2025 kwenye uwanja wa Nelson Mandela huko Baraki, kitongoji cha Jiji la Algiers nchini Algeria huku ikiwa na rekodi ya kushinda mechi tatu dhidi ya Flambeau du Centre na Rayon Sports kati ya nne za hatua ya awali ya michuano hiyo. Moja ikitoka sare na kufuzu makundi kwa mara ya kwanza.
Gamondi, aliyekaimu nafasi ya Kocha Mkuu wa Taifa Stars kwenye mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Kuwait iliyopigwa nchini Misri, mechi ambayo Stars ilipoteza kwa mabao 4-3, alisema hakuna changmoto yoyote ndani ya klabu hiyo kwa kuwa majukumu yake yalikuwa yakisimamiwa na David Ouma.
“Nimefurahi kurejea haraka na kuungana na kikosi. Nilipokuwa nje kwa majukumu ya timu ya taifa, Ouma na benchi la ufundi walikuwa wanaendelea kusimamia programu zetu vizuri. Hakuna kilichoharibika,” alisema kocha huyo na kuongeza:
“Tunajua umuhimu wa mechi hii, ukizingatia ni mechi yetu ya kwanza kwenye hatua ya makundi, tunakutana na timu yenye uzoefu mkubwa Afrika lakini hatupo hapa kujitetea, tupo hapa kwa ajili ya kupambana, kuweka mpango kazi wetu uwanjani na kuonyesha dhamira ya klabu hii.”€
Kikosi cha Singida Black Stars kiliondoka jana Jumanne, kutoka Dar es Salaam kuelekea Istanbul, Uturuki kabla ya kuunganisha safari hadi Algiers kupitia Shirika la Ndege la Uturuki (Turkish Airlines).
Licha ya mechi hiyo kupigwa Novemba 22, benchi la ufundi limeamua kufika mapema Algeria ili kikosi kipate angalau siku tatu za kuzoea hali ya hewa pamoja na mazingira ya uwanja.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya benchi la ufundi la Singida Black Stars, mazoezi ya awali yatafanyika mara tu kikosi kitakapowasili ili kuhakikisha wachezaji wanaingia kwenye utimamu unaohitajika kwa mechi ya ugenini.
Gamondi aliongeza: “Tunataka kuwa tayari mapema. Hali ya hewa ya Algeria ni tofauti na ya kwetu, hivyo ni muhimu kufika mapema ili mwili wa mchezaji uzoee. Hii mechi ni muhimu, tunataka kuanza hatua ya makundi kwa nguvu.”
Singida Black Stars inatarajiwa kufanya mazoezi ya mwisho Ijumaa kwenye uwanja utakaotumika kwa mechi wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 40,784 kabla ya kuvaana na CR Belouizdad inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Sead Ramovic.