CMSA itakavyoboresha mazingira wezeshi, shirikishi

Dar es Salaam. Mamlaka ya Masoko Mitaji na Dhamana (CMSA) imesema itaendelea kuweka mazingira wezeshi na shirikishi ili sekta za umma na binafsi ziweze kutumia masoko ya mitaji kupata fedha za kutekeleza shughuli na miradi ya maendeleo.

Hayo yamesemwa leo Jumanne, Novemba 18, 2025 wakati wa uzinduzi wa iTrust East African Community Large Cap Exchange Traded Fund (IEACLC-ETF), itakayowawezesha wawekezaji wa ndani na nje kupata fursa ya moja kwa moja kumiliki hisa katika kampuni mbalimbali ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

IEACLC-ETF inasimamiwa na CMSA, huku Benki ya NBC ikifanya kazi kama mwangalizi wa mali za wawekezaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Sera, Utafiti na Mipango kutoka CMSA, Alfred Mkombo amesema wamekuwa wakihakikisha shughuli katika masoko hayo zinafanyika kwa kufuata taratibu na miongozo na haki kwa watu wote.

“Masoko ya mitaji huchochea maendeleo ya uchumi kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha na kuimarisha utawala bora katika uendeshaji wa kampuni na taasisi ili zilete tija,” amesema Mkombo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa iTrust Finance, Faiz Arab amesema IEACLC-ETF ni hatua muhimu katika safari ya kukuza na kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

“ETF hii inafungua ukurasa mpya kwa wawekezaji nchini Tanzania. Kwa mara ya kwanza mtu mmoja mmoja ataweza kufikia mfuko wa kikanda unaosimamiwa kitaalamu kupitia bidhaa rahisi na nafuu,” amesema.

Afrika Mashariki ni moja ya kanda zinazokua kwa kasi barani na kama kampuni wanajivunia kuwapa wateja njia rahisi ya kunufaika na ukuaji huo.

“Lengo letu ni kuondoa vikwazo vya uwekezaji ili kila mtu awe mzoefu au anayeanza aweze kushiriki katika mafanikio ya kiuchumi ya ukanda huu. ETF hii ni kwa ajili ya wawekezaji wanaolenga kujenga utajiri wa muda mrefu na walio tayari kuwekeza katika masoko ya hisa kwa kuwekeza kwenye mkusanyiko wa kampuni kubwa na thabiti katika sekta mbalimbali,” amesema.

Amesema mfuko huo unapunguza hatari ya kuegemea upande mmoja na kuongeza nafasi ya kupata faida endelevu kadiri thamani ya hisa inavyoongezeka.

Arab amesema muundo wa mfuko umezingatia uwazi na ulinzi kwa wawekezaji.

Kupitia ETF wawekezaji wataweza kukuza mitaji yao kwa kununua vipande vinavyowakilisha hisa za kampuni kubwa zilizoorodheshwa katika masoko ya hisa ya Dar es Salaam (DSE), Nairobi (NSE), Uganda (USE), na Rwanda (RSE).

Mfuko huu unaongozwa na kielelezo mchanganyiko kinachojumuisha faharisi za masoko yote manne, hivyo kutoa uwekezaji mpana na wa aina mbalimbali kwa ulinganifu wa juu.

Katika kipindi cha Mauzo ya Awali ya Umma (IPO) kilichoanza Novemba 17 na kutarajiwa kufungwa Desemba 12, 2025, wawekezaji wanaweza kushiriki kwa kuanzia kiwango cha chini cha Sh100,000, hatua inayoufanya uwekezaji huu kufikiwa kwa urahisi na wawekezaji wapya pamoja na wenye uzoefu mkubwa.

Baada ya kuorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam, vipande vya ETF vitauzwa na kununuliwa moja kwa moja sokoni kwa bei itakayokuwa inatumika wakati huo.