Moshi. Kampuni ya TPC Limited imeingia katika mageuzi ya kiuchumi kupitia mradi wa kimkakati wa kuongeza mnyororo wa thamani wa zao la miwa, utakaogharimu dola za Marekani 52 milioni (Sh130 bilioni).
Hayo yameelezwa leo Novemba 18, 2025 na Ofisa Mtendaji wa TPC, Jaffari Ally wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huo uliopo Kata ya Arusha Chini, Wilaya ya Moshi, unaotarajiwa kufanyika Novemba 19, 2025.
Ally amesema mradi huo unalenga kubadilisha mfumo wa zamani wa kuuza molases ghafi na badala yake kuichakata kupata bidhaa mbalimbali ambazo zitaongeza ajira, mapato ya kodi, kuchochea uchumi kupitia viwanda, nishati mbadala na uzalishaji wa malighafi muhimu nchini.
Kwa mujibu wa Ally, ujenzi wa mradi huo umefikia zaidi ya asilimia 30 huku vifaa vya ujenzi vikiwa vimewasili kwa asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2026, hatua ambayo itaongeza tija kwa wakulima, pato la kampuni na mapato ya Serikali.
Amesema kwa kukamilika kwa mradi huo, TPC itaanza kuzalisha lita milioni 16.3 za Extra Neutral Alcohol (Ethanol) kwa mwaka, kiwango kitakachofanya kiwanda hicho kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa nchini.
Katika mradi huo, pia watazalisha lita 400,000 za Technical Alcohol kwa mwaka kwa ajili ya matumizi ya majiko poa, hatua inayotarajiwa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.
“Tutakuwa tukizalisha Technical Alcohol, hii ni nishati inayotumika kwa majiko poa. Uwezo wa uzalishaji utafikia lita 400,000 kwa mwaka. Hii itaenda kusaidia upikaji wa vyakula kwa kutumia majiko poa ambayo yatakwenda kuchukua nafasi kubwa na kupunguza matumizi ya kuni na mkaa,” amesema.
Aidha, amesema katika mradi huo, watazalisha tani 8,000 za mbolea ya potasiamu inayotokana na mabaki ya molases, ambayo inayofaa kwa kilimo hai kwa kuwa haina kemikali.
“Pia, tutakuja na uzalishaji wa gesi ya kaboni kwa matumizi ya viwandani, tutazalisha lita 400,000 kwa mwaka na hii inatumika zaidi kwenye viwanda vyetu vya vinywaji. Hivyo, badala ya kuagiza nje ya nchi, itapatikana hapa TPC,” ameeleza Ally.
Kwa upande wake, mwakilishi wa chama cha wafanyakazi wa TPC, Bilali Mchomvu amesema kuanzishwa kwa kiwanda kipya cha kuchakata molasses ni hatua muhimu inayotarajiwa kuongeza thamani ya mazao ya miwa na kupanua wigo wa uzalishaji ndani ya kampuni hiyo.
Ameeleza kuwa kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa mbalimbali zinazotokana na molasses, hatua itakayoiwezesha TPC kuongeza uzalishaji, tija na ushindani katika soko la ndani na nje ya nchi.
Amesema kufunguliwa kwa kiwanda hicho kutaleta maboresho makubwa katika ajira kwani mradi huo unatarajiwa kuongeza nafasi nyingi za kazi na hivyo kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira nchini.
Kwa mujibu wa Mchomvu, kukamilika kwa mradi huo kunaweza kusababisha kuajiriwa kwa wafanyakazi wapya 1,800, jambo litakalokuwa msaada kwa vijana na familia nyingi katika jamii inayozunguka kiwanda hicho na nchini kwa ujumla.
Bilali ameongeza kuwa manufaa ya mradi huo hayataishia kwa wafanyakazi pekee, bali yatachochea pato la Taifa na kuimarisha uchumi wa jamii inayozunguka eneo hilo.
Ameeleza kuwa faida za kampuni zinapoongezeka, huwa ni fursa ya kuboresha masilahi ya wafanyakazi, kuongeza mishahara, na kupanua uwezo wa kampuni kuajiri watu wengi zaidi. Hivyo, mradi huo unaonekana kuwa na mchango chanya kwa uchumi wa ndani, kitaifa na kwa ustawi wa wafanyakazi wenyewe.
Kwa upande mwingine, mbunge mstaafu wa Jimbo la Moshi Mjini, Priscus Tarimo amepongeza hatua za uwekezaji zinazofanywa na TPC akizitaja kuwa ni ubunifu na mfano wa kuigwa katika sekta ya viwanda nchini.