Wauza mkaa wa miti kukiona Songwe

Songwe. Ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yanayotajwa kuchangia kushuka kwa uzalishaji wa zao la kahawa, Serikali mkoani Songwe imepiga marufuku mtu yeyote kujihusisha na shughuli za mkaa unaotokana na miti.

Imesisitiza kuwa bila kuchukua hatua za haraka na makusudi kwa kuoneana aibu, miaka 10 ijayo dunia inaweza kuharibika na kuondoa sekta ya kilimo hicho kutokana na shughuli za kibinadamu.

Akizungumza leo Novemba 18, 2025 wakati wa maadhimisho ya siku ya kahawa duniani iliyofanyika wilayani Mbozi mkoani Songwe, Mkuu wa Mkoa huo, Jabir Makame amesema mkaa unaotokana na miti ni nyara ambayo haipaswi kuonekana na mtu.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabir Makame akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya Kahawa duniani yaliyofanyika leo wilayani Mbozi mkoani humo.

Amesema yeyote atakayekutwa na gunia la mkaa watashughulika naye akibainisha kuwa upo mradi chini ya Shirika la Madini la Taifa (Stamico) wanaozalisha mkaa mbadala na wa mawe ambao ni rafiki kwa matumizi.

“Tumeambiwa hapa uzalishaji wa kahawa umeshuka kwa sababu za mabadiliko ya tabianchi, hii ni kutokana na shughuli za kibinadamu ikiwamo ukataji miti na uchomaji misitu,” amesema na kuongeza;

“Mpango wetu ni kupiga marufuku mkaa katika Mkoa wa Songwe, tunaelekeza Kiwira kusajili wauzaji kila mtaa wauze mkaa mbadala, tutakayemkuta anauza mkaa wa miti tutashughulika naye,” amesema Makame.

Ameongeza kuwa pamoja na juhudi hizo, Serikali imeendelea kuweka juhudi kuboresha sekta ya kilimo kwa kuweka miundombinu bora ikiwamo ya umwagiliaji, kwa kuchimba visima na mabwawa akiwaomba wadau wengine wa kilimo kushirikiana.

Ameongeza kuwa hadi kufikia Oktoba 30 mwaka huu, imeuzwa kilo 3,764,300 za kahawa safi zilizoingiza zaidi ya Sh52.453 bilioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 59 kutoka zaidi ya Sh36.450 bilioni za kwa msimu wa kilimo wa 2024/25.

Kwa upande wake Meneja wa Bodi ya Kahawa nchini (TCB) Nyanda za Juu Kusini, Ezekiel Mwakyoma amesema changamoto kubwa ni mabadiliko ya tabianchi, bei duni ya mazao, fedha, mitaji, idadi ndogo ya miti, ubora mdogo wa kahawa kutokana na maandalizi.

Amesema kuwa katika kukabiliana na changamoto hizo, tayari TCB kwa kushirikiana na wadau wa zao hilo, wameanza utekelezaji wa uchimbaji visima na mabwawa ikiwamo ugawaji miche ya kisasa ‘Mbegu Tacri’.

“Tupo kwenye utekelezaji huo ambapo kitaifa umeanzia hapa Mbozi, tumechimba visima 20 na kati ya hivyo vitano vimekamilika rasmi na vingine mkandarasi anaendelea kufanya usanifu, tunashirikiana sana na wadau.

Baadhi ya wakulima wa zao hilo wakishiriki maadhimisho hayo

“Tunazalisha miche bora na ya kisasa ambayo inakabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Serikali inaendelea kuboresha miundombinu kwa kutumia teknolojia,” amesema Mwakyoma.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Hamad Mbega amesema wilaya hiyo ndio kinara katika uzalishaji wa zao hilo, akieleza kuwa mapato makubwa katika Halmashauri hiyo inategemea sana zao hilo, akieleza kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira mazuri kwa wakulima na ustawi wa mazingira.

“Wakulima kwa kushirikiana na Serikali wamechimba visima 30 na wadau wengine wameendelea kujitolea, Wilaya tumetenga zaidi Sh70 milioni kumalizia miradi ya visima ambavyo havijakamilika,” amesema Mbega.

Mmoja wa wakulima wa zao hilo, Faustine Nsheka amesema pamoja na changamoto zilizopo, lakini Serikali imeendelea kuwa pamoja nao katika kusikiliza na kutatua kero zao kwa wakati.

“Kupitia maadhimisho haya, tunabadilishana mawazo na fikra katika kufikia malengo, kahawa ndilo zao kuu hapa Mbozi na mara kadhaa Serikali imekuwa na sisi, tunashukuru na kuipongeza kutukutanisha, tunaomba bei izidi kupanda kwani tunanufaika sisi na Taifa letu,” amesema Nsheka.