Samia ateua wanane tume ya kuchunguza yaliyotokea Oktoba 29

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameunda Tume Huru ya Uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025.

Sambamba na kuunda tume hiyo, amemteua Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman mwenyekiti wa tume hiyo pamoja na wajumbe saba.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa kile alichoahidi Novemba 14, 2025 alipohutubia na kulizindua Bunge la 13, jijini Dodoma akisema ataunda tume kuchunguza matukio hayo.

“Mimi binafsi nimehuzunishwa sana na tukio lile. Natoa pole kwa familia zote zilizopoteza wapendwa wao, na tunamuomba Mwenyezi Mungu awapumzishe kwa amani. Aidha, kwa majeruhi tunawaombea wapone kwa haraka, na kwa wale waliopoteza mali zao tunawaomba wawe na stahamala na uvumilivu,” alisema Rais Samia na kuongeza:

“Serikali imechukua hatua ya kuunda Tume ya kuchunguza yaliyotokea ili tujue kiini cha tatizo. Taarifa hiyo itatuongoza kujielekeza kwenye mazungumzo ya kuleta maelewano na amani.”

Katika matukio hayo, vurugu zilitokea mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Songwe, Geita, Arusha, Mara na Ruvuma na kusababisha raia kuuawa, wengine kujeruhiwa huku mali za watu binafsi na miundombinu ya umma zikiharibiwa.

Alisema ripoti ya tume hiyo, itaiongoza Serikali kuanza mchakato wa maridhiano kupitia Tume ya Maridhiano na Upatanishi itakayoundwa hapo baadaye.

Taarifa iliyotolewa leo Jumanne Novemba 18, 2025 na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka imeeleza Rais Samia ameiunda tume hiyo kwa mamlaka aliyonayo.

“Kwa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32, ameunda Tume Huru ya kufanya uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea nchini wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 29 Oktoba, 2025,” imeeleza taarifa hiyo.

Wajumbe walioteuliwa kwa mujibu wa taarifa hiyo ni Jaji Mkuu mstaafu, Profesa Ibrahim Juma, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue, Mwanadiplomasia na Balozi Radhia Msuya.

Katika tume hiyo, pia yumo Balozi Paul Meela, Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu, Said Ally Mwema, Balozi David Kapya na Waziri mstaafu wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax.

Jaji Othman ukiacha uzoefu wake wa utumishi katika sekta ya sheria, amewahi kuhudumu nafasi ya uenyekiti katika tume mbalimbali ikiwemo ya karibuni ya kurekebisha mifumo ya haki jinai, iliyoundwa na Rais Samia.

Kwa upande wa Balozi Sefue amewahi kuhudumu katika nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi wakati wa Serikali ya awamu ya nne chini ya Jakaya Kikwete.

Naye, ni miongoni mwa wajumbe walioongozwa na Jaji Chande katika tume ya kurekebisha mifumo ya haki jinai nchini.

Kwa upande wa Profesa Juma, amewahi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Jaji wa Mahakama ya Rufani na hatimaye Jaji Mkuu wa Tanzania.

Balozi Radhia amewahi kuiwakilisha Tanzania nchini Afrika Kusini mwaka 2016 na nafasi nyingine mbalimbali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Balozi Meela amewahi kuiwakilisha Tanzania nchini Jamhuri ya Demokrasi ya Congo na amewahi kuwa Kamanda wa Kikosi cha Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa katika kurejesha amani mjini Darful.

Balozi Meela ni askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na amewahi kuhudumu nafasi za ushauri wa masuala ya ulinzi katika balozi mbalimbali.

Kwa upande wa Said Mwema, amewahi kuhudumu nafasi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania.

Balozi David Kapya amewahi kuwa mshauri mwandamizi na muongozaji wa majadiliano ya Burundi na alikuwa msaidizi maalumu wa Rais wa awamu ya tatu Tanzania, hayati Benjamin Mkapa.

Dk Stergomena Tax yeye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.