Wazungumzia kauli ya ‘Wewe ni mwanaume, jikaze!’ wakiadhimisha siku yao

Dar es Salaam. “Wewe ni mwanaume, jikaze! Mwanaume gani unakuwa legelege! Wanaume huwa hawalii,” hizi na nyingine nyingi ni kauli ambazo wanaume, ambao kesho Novemba 19 wataadhimisha siku yao duniani, wamezieleza namna zinavyowajenga na wakati mwingine kuwaweka kwenye hatari.

Kesho itakuwa mwaka wa 26 kwa wanaume duniani kuadhimisha siku hiyo, iliyoasisiwa mwaka 1999 nchini Trinidad & Tobago. Tanzania, siku hiyo ilianza kuadhimishwa mwaka 2024.

Dk Jerome Teelucksingh, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha West Indies, alipendekeza kuwe na siku maalumu ya kimataifa kwa ajili ya wanaume, baada ya takwimu mbalimbali kuonyesha wanaume hupata vifo vingi kutokana na magonjwa yasiyoambukiza, ajali, na changamoto za kisaikolojia.

Vilevile, shinikizo la kijamii la “kuwa mwanaume” huwazuia wengi kufunguka au kutafuta msaada, hivyo kuanzishwa kwa siku hiyo kulilenga kuwa na majadiliano ya kijamii kuhusu namna inavyoweza kujenga usawa, afya na amani kwa wote.

Wakizungumzia siku hiyo na taswira iliyojenga jamii kuwahusu, baadhi ya wanaume wamekuwa na mtazamo tofauti. Wengine wakiamini kitendo cha kuwa mwanaume kinawafanya wengi kushindwa kuonesha hisia zao, hususan za huzuni, wakihofia kukosolewa na jamii.

Wengine wanashikilia utamaduni wa mwanaume kutakiwa kujikaza na kutoonesha hisia fulani za huzuni. Hali hii huwajengea na kuwaongezea kutokata tamaa huku kukiwaimarisha.

“Hizi kauli za ‘mwanaume hapaswi kuwa hivi’ huonekana ni za kawaida katika jamii, lakini zina athari kubwa kiakili, kijamii na kihisia kwa wanaume,” amesema Tito Ephraim wa Dar es Salaam.

Tito ametolea mfano wa mdogo wake aliyepoteza maisha kwa kushindwa kuelezea hisia zake, akibainisha aliishi katika ndoa yenye maumivu, lakini alishindwa kutoka baada ya familia kumwambia anapaswa kupambana kiume kuinusuru ndoa yake na si kutoa talaka.

“Ilifikia hatua yule ndugu yangu aliishi kwa maumivu, ilipelekea kifo chake, alifanya uamuzi mgumu wa kumuua mkewe na yeye kujimaliza. Ni tukio lililotuhuzunisha, ingawa kwenye familia lilitupa funzo kwamba kabla wazazi wetu waliamini wanaume haruhusiwi kuonesha udhaifu. “Waliamini mwanaume hapaswi kuonesha huzuni, uchungu, kuchoka au kuhitaji msaada, bali anapaswa kuwa jasiri, mkakamavu na asiyehisi maumivu,” amesema.

Mbali na simulizi hiyo ya Tito, kwa Edgar Kabuche, anaamini kuonesha hisia za huzuni kwa wanaume ni unyonge, akisistiza mwanaume anatakiwa kujikaza hata anapoumia au kupitia ugumu wa jambo fulani.

“Katika mila nilizotoka, tunaamini wanaume hawalii, hawakati tamaa, hawakosei, hawasemei shida zao na hawarudi nyuma. Tunaishi katika utamaduni huo, na umekuwa ukituimarisha hata tunapopitia magumu namna gani, tunapambana kiume,” amesema.

Akizungumzia hilo, Mwalimu wa Saikolojia wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Tanga, Modester Kimonga, amesema kuna athari hasi na chanya.

Akifafanua athari chanya, Kimonga amesema kuwa wanaume wanaojikaza kwa usahihi mara nyingi inawaongezea kujiamini na kukabiliana na changamoto badala ya kuzikimbia.

“Pia, inamsaidia kukua kiakili na kimaisha pale anapopitia matatizo na kuwa mbunifu katika kutafuta suluhisho, vilevile inamsaidia kuwa mchapa kazi, mlinzi wa familia au kiongozi bora, na kwa baadhi yao inaweza kupelekea maendeleo makubwa ya kimaisha,” amesema.

Kwa upande wa pili, Kimonga amesema hali hiyo huwa changamoto pale mwanaume anapojikaza bila kuonesha hisia zake au kutafuta msaada pale inapohitajika.

“Wengi huwa wanashindwa kutambua kwamba kuwa mwanaume si lazima kuwa jasiri kila wakati, unapaswa ujikaze bila kujipoteza,” amesema.

Mwanasaikolojia huyo amesema kila binadamu ana hisia bila kujali jinsia yake, japo kwa wanaume wengi wao hujikuta wakizungukwa na kauli za kuwataka wasifanye kitu fulani kwa kuwa tu wao ni wanaume.

“Unapomzuia mtu kuonesha hisia zake, hasa za huzuni, inapelekea ugonjwa, msongo wa mawazo na hata kifo. Mwanaume anaweza kuwa anaumwa, akionesha kuumwa kwa mkewe au mama yake au rafiki zake, wakamwambia ‘usilale lale, wewe ni mwanaume,’ hatoweza tena kuonesha hisia zake,” amesema.

Amesema watoto wadogo wa kiume wanapoishi kwenye jamii yenye utamaduni huo, kutasababisha kupoteza uwezo wa kutoa maoni na hata kujiamini.

“Kutamjengea uoga, anaweza kuwa na tatizo akashindwa kulisema kwa sababu ya mila ambazo amezikuta kwenye jamii iliyomzunguka,” amesema.

Amesema wanaume wengi hawapati nafasi ya kuongea au kuonekana wamedhoofika, huku wakilazimika kutengeneza uso wa ujasiri wakati wakiwa na changamoto za kihisia, jambo ambalo linawaumiza kiakili, kiafya na hata kimwili.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), wanaume hupata vifo vingi kutokana na magonjwa yasiyoambukiza, ajali na changamoto za kisaikolojia.

WHO inasema wanaume huwaona madaktari mara chache zaidi na kuripoti mahitaji zaidi ya huduma ya afya ambayo hayajatimizwa.

Kundi hilo linakabiliwa na hatari kubwa ya kifo cha mapema na ulemavu kutokana na magonjwa na majeraha yanayoweza kuzuilika, mengi ambayo yanaweza kuepukika.

Kwa mujibu wa WHO, wanaume wana uwezekano mkubwa wa kufa mapema kutokana na magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) kama vile magonjwa ya moyo, saratani na kisukari.

“Umri wa kuishi kwa wanaume ni mfupi kuliko wa wanawake karibu kila nchi. Hata kama unajisikia mzima, uchunguzi wa kawaida wa afya kama vile kupima shinikizo la damu, kiwango cha sukari, na uchunguzi wa tezi dume ni muhimu ili kugundua matatizo mapema na kubaki salama kiafya,” ilieleza taarifa ya WHO ya hivi karibuni, ikisisitiza kutafuta usaidizi unapokabiliana na msongo wa mawazo, wasiwasi au mfadhaiko.

Chimbuko la Siku ya Wanaume

Novemba 19 ya kila mwaka, dunia huadhimisha Siku ya Wanaume, yenye lengo la kuangazia mchango, changamoto na nafasi ya wanaume katika jamii.

Siku hiyo ilianza mwaka 1999 nchini Trinidad & Tobago, ikiasisiwa na Dk. Jerome Teelucksingh, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha West Indies, aliyependekeza kuwe na siku maalumu ya kimataifa kwa ajili ya wanaume.

Aliichagua Novemba 19 kwa sababu mbili: kwanza, ilikuwa siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa baba yake, mwanaume aliyemchukulia kama kielelezo cha uadilifu, bidii na uongozi wa familia; pili, ni siku iliyokumbukika kwa umoja wa kitaifa nchini Trinidad baada ya timu ya soka ya wanaume kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa.

Siku hiyo ina malengo sita ambayo ni kuangazia afya ya wanaume na wavulana, ikiwamo afya ya akili ambayo mara nyingi haizungumzwi; kusheherekea wanaume wanaofanya kazi nzuri katika jamii; na kuboresha mahusiano ya kijamii, kifamilia na kijinsia.

Pia, imelenga kukuza usawa wa kijinsia kwa kuhusisha wanaume katika majadiliano, kutambua changamoto zinazowakabili wanaume, kama ajali kazini, msongo wa mawazo na vifo vya kujitoa uhai, na kuchochea amani na usalama katika jamii.

Nchini Tanzania, Siku ya Wanaume ilianzishwa rasmi Aprili 23, 2024, na jumuiya ya Community Development Association (CDA) wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Affirmative Action on Gender Equality Network (AGEN). Wakilenga kuongeza uelewa, kutetea haki za wanaume, na kuwahamasisha wawe waaminifu katika familia na jamii.

Maadhimisho ya kwanza yalifanyika mjini Morogoro, kwenye viwanja vya Shule ya Msingi ya Kiwanja cha Ndege, yakiwa na kauli mbiu “Tanzanian Men, Patriotism, and Responsibility.”