Watano walionusuruka ajali ya moto kujengewa makazi

Mbeya. Familia ya watu watano walionusurika kwenye ajali ya moto na kukosa makazi wamepata matumaini baada ya Taasisi ya Tulia Trust kuanza ujenzi wa nyumba ya kisasa.

Imeelezwa tukio hilo lilitokea Septemba 5, mwaka huu, katika Mtaa wa Mwafute, Kata ya Ilemi kwenye nyumba ya mzee Anyomwisye Mwalyaje (80).

Awali akizungumza na Mwananchi Digital Novemba 17, 2025, Ofisa habari Taasisi ya TuliaTrust, Addi Kalinjila amesema hatua ni sehemu ya kugusa jamii kupitia programu maalumu.

“Tumekuwa na programu maalumu ya ‘Tulia Trust mtaani kwetu’ kwa kusaidia wananchi hususani ujenzi wa makazi kwa kaya maskini, wazee na yatima ambapo kwa mwaka mmoja wamezifikia kaya 22,” amesema.

Katika hatua nyingine amehamasisha jamii na viongozi wa Serikali za mitaa kutoa taarifa za watu wenye mahitaji wakiwepo wazee na kaya maskini ili waweze kuwafikia na kurejesha tabasamu hususani kuwajengea makazi bora na kutoa Bima za Afya bure.

Diwani wa Kata ya Ilemi, Baraka Zambi amesema hatua ya Taasisi hiyo chini ya Dk Tulia kugusa wananchi wenye changamoto ambalo kama jamii inapaswa kuendelea kumuombea.

“Awali baada ya kutokea tukio hilo la makazi ya familia ya Kasemba Mwalyaje (80), kuteketea kwa moto tulitoa taarifa kwa Mbunge wa Uyole Dk Tulia Ackson ambaye  alifika kutoa pole kwa familia na  kuahidi  kujenga haraka kupitia taasisi yake jambo ambalo limetekelezwa kwa vitendo,” amesema.

Wakati huo huo amewataka vijana kuachana na propaganda za mtandaoni na badala yake kugeukia kuchapa kazi kwa maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Mjumbe wa nyumba kumi Mtaa wa Mwafute Kata ya Ilemi, Erasto Clement amesema kuwa kimsingi hatua ya ujenzi wa makazi ya familia hiyo inakwenda kurejesha matumani yaliyo potea kwa kukosa makazi.

“Siku ya tukio nilikuwa mbali kidogo nilipigiwa simu kuwa nyumba ya wazee wetu inateketea kwa moto nililazimika kutoa taarifa kwenye mamlaka husika ambao walifika haraka kuzima licha ya mali na makazi yalikuwa tayari yameharibika,” amesema.

Mmoja wa wanafamilia Nsajingwa Mwalyaje, amesema kimsingi wanamshuru Mungu katika tukio hilo hakuna mtu aliyepata madhara mbali ya uharifu wa mali na makazi.

“Chanzo za kuzuka kwa moto ni kutokana na hitilafu   ya umeme, lakini siku ya tukio ndani  ya nyumba kulikuwa na watu watano wakiwepo baba, mama na wajukuu watatu kikubwa kwa niaba ya familia tunamshukuru  Dk Tulia kwa msaada wa ujenzi wa makazi mapya  ya kisasa,”amesema.