Na Mwandishi wetu- Dodoma
Waziri Mteule wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa amemhakikishia Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu- TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe kushirikiana kikamilifu kwenye eneo la Afya ili kutimiza ndoto ya Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea tabasamu wananchi wa Tanzania kupitia kauli mbiu ya Serikali ya sasa ya Kazi na Utu Tunasonga Mbele.
Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo masaa machache baada ya kuapishwa wakati akikabidhi Ofisi yake ya awali kwa Mhe. Prof. Shemdoe katika Mji wa Kiserikali wa Mtumba jijini Dodoma leo Novemba 18, 2025 huku akisisitiza kuendelea kuimarisha ushirikiano katika utendaji wa kazi.
“Wizara zetu hizi katika eneo la Afya zinahitaji kushirikikiana sana kwa kuwa mwisho wa siku wote tuna lengo moja tu la kumhudumia mwananchi wa Tanzania kama Mheshimiwa Rais wetu anavyotuhimiza katika maagizo yake ya kila baada ya kushinda Mchaguzi Mkuu wa mwaka huu, hivyo hakuna sababu ya kuendelea kutengana” . Amefafanua Mhe. Mchengerwa
Aidha, amesema hana shaka na utendaji na uzoefu wa Waziri Shemdoe katika kuisimamia Wizara hiyo kwa kuwa amekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo hivyo anafahamu maeneo yote kama mtu ambaye amekuwa Mtendaji Mkuu.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Adolf Ndunguru amemshukuru Mhe.Mchengerwa kwa kuisimamia Wizara hiyo kwa mafanikio makubwa katika kipindi chake jambo ambalo amesema ameacha alama nyingi.
Kwa upande wake, Waziri Shemdoe ameitaka Menejimenti ya Wizara yake kuainisha maelekezo yote aliyoyatoa Mhe. Rais na ahadi zinazotakiwa kutekelezwa katika kipindi cha siku mia moja za awamu yake.
“Ndugu zangu siku mia moja za utekelezaji wa ahadi za Mhe. Rais siyo nyingi na kama mnavyotambua tayari siku kumi zimesha katika tumebaki na miezi mitatu ambayo siyo mingi tunatakiwa kwenda kwa spidi tukitambua kuwa hii ndiyo wizara ya kuwaletea furaha watanzania”. Amefafanua Waziri Shemdoe.
