Wachumi: Kauli Samia sawa na kufunga mkanda

Dar es Salaam. Tanzania huenda ikaingia katika kipindi kipya cha ukata wa kifedha na Rais Samia Suluhu Hassan amewataka mawaziri wapya wajipange kukumbana na ugumu huo kufuatia doa ambalo taifa limepata kufuatia matukio ya Oktoba 20, wachumi wameeleza.

Tafsiri ya wasomi hao inafuatia kauli ya Rais Samia kuwa Serikali huenda isipate misaada na mikopo kama ilivyokuwa awamu iliyopita na hivyo akatangaza mkakati mpya wa kutekeleza miradi kwa kutumia rasilimali za ndani.

Kwenye matukio hayo ya wakati na baada ya uchaguzi, mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Songwe, Geita na Arusha iliathirika vurugu zilizopelekea kuuawa kwa raia, wengine kujeruhiwa, pamoja na mali za watu binafsi na za umma kuharibiwa.

Miongoni mwa mali hizo, ni ofisi za serikali, Chama tawala cha CCM, vituo vya polisi, vituo vya mabasi yaendayo haraka ‘mwendokasi’ vituo vya mafuta na nyumba za baadhi ya viongozi.

Matukio hayo, yamesababisha jumuiya za kimataifa ikiwemo Umoja wa Mataifa (UN) kutoa wito wa uchunguzi kufanyika na kutafutwa njia za kudumisha amani nchini, huku Jumuiya ya Madola ikituma ujumbe wa kutafuta mazungumzo ya maridhiano.

Akizungumza baada ya kuwaapisha mawaziri na naibu mawaziri leo Jumanne, Novemba 18, 2025, Rais Samia amesema matukio hayo yameitia doa Tanzania na huenda yakasababisha changamoto ya upatikanaji wa mikopo.

Amewaelekeza watendaji hao kujikita katika matumizi ya rasilimali za ndani kutekeleza miradi iliyopangwa.

“Yaliyotokea nchini kwetu yametutia doa kidogo, kwa hiyo huenda yakatupunguzia sifa ya kupata hiyo mikopo kwa urahisi kama tulivyopata muhula wa kwanza wa awamu hii,” amesema.

Katika muhula wake wa kwanza, amesema Tanzania ilipata mikopo mingi kwa sifa, msimamo na kazi zake, lakini kwa doa lililopo sasa huenda hali ikawa tofauti.

Kutokana na mazingira hayo, amesema ni jukumu lake na viongozi aliowateua kuhakikisha wanafanya kazi ya kutafuta fedha za ndani kupitia rasilimali zilizopo ili kutekeleza miradi inayotarajiwa.

“Muhula wa pili wa awamu ya sita, tutaanza kufanya miradi wenyewe, alafu mashirika yatatukuta njiani tutakwenda nao. Hatutakaa kusubiri, tunauza mradi, tunakwenda kubembeleza mradi unakubaliwa nendeni karekebisheni hili…

“Mradi badala ya kupata uidhinishaji miezi mitatu minne, tunachukua mwaka mzima tunabembeleza mradi mmoja, hadi ruhusa inatoka tuna miaka miwili tunamaliza kipindi chetu, hatutasubiri hayo, tutaanza na watatukuta katikati,” amesema.

Kauli hiyo imewaibua wachumi wakisema mbali na matumizi ya fedha za ndani, hali hiyo itailazimu Serikali kupunguza matumizi, kuanzisha vyanzo vipya vya mapato kama kodi au tozo, jambo litakaloongeza gharama za maisha na maumivu yake yatawagusa zaidi wananchi.

Tahadhari hiyo ya Rais Samia, imeelezwa inawaandaa Watanzania kufunga mkanda, Serikali inapoelekea kujitegemea katika kufanya mambo yake, kama anavyoelezwa Mhadhiri wa Uchumi, Dk Josephat Werema.

Dk Werema amesema Serikali katika hali ya kujitegemea, inapaswa kupunguza gharama za matumizi, mathalan safari za viongozi, misafara inayogharimu fedha, semina kwa watumishi na zaidi hata wingi wa viongozi, likiwemo Baraza la Mawaziri.

Wakati gharama za matumizi zikipunguzwa, amesema kwa upande mwingine Serikali inapaswa kufikiria kuongeza vyanzo vya mapato kwa kuanzisha kodi au tozo katika maeneo mbalimbali, hali ambayo pengine italeta maumivu kwa wananchi.

“Mazingira kama hayo yanapokuja bila kujiandaa, mara nyingi yanasababisha kupanda kwa bei za bidhaa, yanaweza kuleta hali ya ugumu wa upatikanaji fedha na anayeumia katika yote ni mwananchi,” amesisitiza.

Amesema namna yoyote ya kubana matumizi itakayofanywa na Serikali, maana yake inapunguza njia za mapato kwa baadhi ya watu na hivyo, fedha zitapungua mtaani.

“Fikiria kama Serikali itapunguza safari za watumishi wake, maana yake kuna watu watakosa fedha za safari, kama itapunguza vikao, maana yake watu watakosa posho za vikao, fedha lazima zipungue mtaani,” amesema.

Hata hivyo, mwanazuoni huyo amesema mafanikio ya matumizi ya rasilimali za ndani kuendesha mambo ya Serikali, yanapaswa kuanza na uimarishwaji wa mifumo ya ukusanyaji mapato.

Amesema kwa sasa, bado kuna njia nyingi za kuvujisha mapato, hivyo kinachokusanywa si kile kinachopatikana kiuhalisia.

“Mapato yanavuja kwa sababu kuna ulegevu kwenye mifumo kwa kiasi fulani. Jeuri ya kujitegemea inapatikana kwa kuwa na msuli wa kukusanya kwa wingi, hili litawezekana kwanza kama tutaimarisha mifumo,” amesema.

Amependekeza uimarishwaji mifumo hiyo uende sambamba na kusimamia uwajibikaji kwa watumishi wa umma, hasa wanaohusika na ukusanyaji wa mapato hayo.

Amesema wakati mwingine uvujaji wa mapato unatengenezwa na watu kwa masilahi yao, hivyo lazima kuwe na njia za ufuatiliaji wa kina, ili mtu asipate nafasi ya kuvuruga ili akusanye kwa ajili yake binafsi.

“Wapo watu wanatengeneza mazingira ya mfumo uharibike ili wapate mwanya wa kuiba. Ukitaka kujiendesha kwa rasilimali zako za ndani, hakikisha unawasimamia vizuri hawa watu, wakikushinda waondoe,” amesema Dk Werema.

Mbali na hilo, amesema yote hayo ni hatua ya pili, lakini kwanza ni muhimu kutengeneza vitu vitakavyowezesha mapato yapatikane, yaani kutanua wigo wa mapato.

Amesema lazima kuwe na msuli wa maeneo yatakapopatikana mapato nje ya yale yaliyozoeleka.

“Hapo Serikali inatakiwa kurasimisha sekta mbalimbali hasa zisizo rasmi, ili zote ziwe na mchango katika uchumi wa nchi na zichangie mapato. Lakini hilo lisifanywe kwa kuzikandamiza hizo taasisi zikafa kabisa,” amesema.

Dk Werema ametahadharisha hali hiyo isiifanye Serikali kuamua kutafuta vyanzo kwa kuunda kodi kwenye baadhi ya huduma muhimu na hatimaye kuwaumiza wananchi.

Pamoja na yote hayo, amesema kujitegemea kunawezekana iwapo kutakuwa na mawasiliano mazuri kati ya Serikali na wananchi.

Ushauri wa Dk Werema umegusiwa pia na Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi na Biashara wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Dk Felix Nandonde, akisema kinachotakiwa kufanyika ni kuzuia upotevu wa fedha katika vyanzo mbalimbali na kusimamia mapato na matumizi, kama ambavyo amekuwa anashauri Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Amesema jambo jingine ni mawaziri hao kusimamia vyema hilo la kutumia fedha za ndani katika miradi ya maendeleo, akisema wakati wote viongozi wakuu wamekuwa wakihimiza hilo.

“Ni wakati wa kurejea yale maeneo ambayo kwenye ripoti za CAG, zimekuwa zikiainisha kuwa fedha za umma zinapotea au zimetafunwa. Tukidhibiti mambo mengi, tunaweza kufanikiwa,” amesema Dk Nandonde.

Kuhusu kauli hiyo ya Rais Samia, Dk Nandonde amesema: “Nadhani rai ya Rais Samia ni kutwambia kuwa kuna vyanzo vya mapato hatujavitumia au hatujaviibua, lakini kingine ni kusimamia mapato na matumizi.

“Kama tutakuwa tumeonekana hatuna sifa za kukopeshwa au ukopeshwaji wetu unaleta mashaka, basi ni muhimu kwenda kusimamia matumizi na vyanzo vyetu vya mapato,” amesema.

Dk Nandonde amesema kuna wakati Rais Samia aliwahi kueleza kuna maeneo fedha zinapotea, pia hata CAG amekuwa ikibainisha hayo kwenye ripoti zake za ukaguzi.

Akizungumzia hilo, Mhadhiri Mwandamizi na Mchumi Kilimo wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo, Dk Rogers Lumenyela amesema ili kufanikiwa katika hilo, amemshauri Rais Samia kuimarisha amani na umoja, hatua itakayorahisisha ukusanyaji wa kodi.

“Katika hili, Rais Samia asisitize amani, umoja na haki ili Taifa liwe kitu kitu kimoja na lisonge mbele. Ana wajibu huo mkubwa wa kuliweka Taifa katika hali ya umoja,” amesema.

Mbali na hilo, Dk Lumenyela amesema suala la kubana matumizi ambalo ni la muda wote, haliepuki ili kufanikisha mkakati huo utakaotumia rasilimali za ndani kupata fedha za kutekeleza miradi.

Dk Lumenyela amesema miongoni mwa kazi mojawapo ya Serikali ni kuweka mazingira wezeshi ili wananchi wafanye kazi au shughuli mbalimbali za kiuchumi zitakazowezesha kulipa kodi.

“Kuwepo na fursa za kazi, zitengenezwe ili watu wafanye kazi walipe kodi. Kama hakuna kazi, sasa watu watalipaje kodi? amesema.

Mbali na kufunga mkanda, Rais Samia ametumia hotuba yake hiyo kuwataka wateule hao, kuwa hataona shida kufanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri, iwapo watatumia nafasi walizopewa kama fahari badala ya dhamana ya kuwatumikia wananchi.

“Mimi sioni shida kubadilisha na mnanijua na kipindi fulani mlinisema kuwa nabadilisha sana. Na nilisema nabadilisha mpaka nipate yule atakayefanya kazi na mimi kwa moyo mmoja,” amesema.

Amewataka wahakikishe wanawajibika kwa wananchi na Taifa, hasa ukizingatia kuna muda mchache wa kwenda mbio kutekeleza yaliyoahidiwa.

“Aliye mzito akapunguze kilo kidogo tuna kazi ya kwenda mbio na ni mbio hasa, kwa sababu muda mchache, mambo ni mengi,” amesema.

Amesema nafasi za uteuzi ni kupishana, ndiyo maana baadhi ya waliokuwepo hawapo sasa na kuna sura mpya zilizochanganyika na chache za zamani.

Lakini, amesema hata waliokuwepo walifanya kazi nzuri na matokeo yanayoshuhudiwa sasa ni juhudi za bidii zao.

“Lakini kazi hizi ni kupishana. Kwa hiyo wamepishana. Kuna timu mpya na kongwe imechanganyika ili twende tukaendeleze mapambano ya maendeleo kwa wananchi,” amesema.

Katiba baraza Rais Samia amewaacha nje baadhi ya waliokuwa mawaziri akiwamo Dk Doto Biteko, aliyekuwa naibu waziri mkuu na waziri wa nishati.

Wengine na wizara zao kwenye mabano ni Hussein Bashe (Kilimo), Innocent Bashungwa (Mambo ya Ndani), Jenista Mhagama (Afya), Dk Seleman Jafo (Viwanda na Biashara), Dk Pindi Chana (Maliasili na Utalii) na Dk Damas Ndumbaro wa Katiba na Sheria.

Rais Samia amewaambia wateule hao kuwa, kiapo walichokula maana yake wamekubali kubeba majukumu na anaamini wameyabeba kwa moyo mkubwa na wako tayari kwenda kuwatumikia watu.

“Majukumu tuliyopeana leo ni dhamana sio fahari, kwamba na mimi ni waziri ikawa ndio fahari, ulikotoka unakokaa na kwingineko hapana. Tumebeba majukumu ya kwenda kuwatumikia wananchi,” amesema.

Ameeleza kwa kuwa kaulimbiu ni ‘kazi na utu, tunasonga mbel, utu huo unapaswa kuanza na viongozi hao, kisha kuwaonyesha kwa watu wengine na kuuheshimisha.