Pantev afumua maeneo matatu Simba

TAARIFA za ndani kutoka Simba zinasema, klabu hiyo imepanga kuongeza nguvu katika maeneo matatu, ushambuliaji, beki wa kati na kipa kupitia usajili wa dirisha dogo linalotarajia kufunguliwa Desemba 15, 2025 hadi Januari 15, 2026.

Kigogo mmoja wa klabu hiyo, aliliambia Mwanaspoti sababu za kutafuta kipa ni kutokana na Moussa Camara kufanyiwa upasuaji wa goti akitarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya wiki nane hadi 10 baada ya kuumia dhidi ya Gaborone Unite, mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally, amesema jana Jumanne Camara alitarajia kufanyiwa upasuaji nchini Morocco na beki wa kati Abdulrazack Hamza atakwenda nchini humo kwa uangalizi zaidi, kutokana na changamoto ya majeraha yanayomsumbua.

PANT 05

Kuumia kwa Camara iliwalazimu viongozi wa Simba kuanza mchakato wa kuzungumza na makipa kadhaa wa nje akiwemo aliyeng’ara katika michuano ya CHAN 2024 akiwa na timu ya taifa ya Madagascar,  Michel Ramandimbisoa na ilielezwa endapo hilo lingefanikiwa wangempa mkataba wa mwaka mmoja kutokana na umri wake wa miaka 39 kuwa mkubwa.

“Bado tunaendelea kutafuta kipa mzoefu atakayeisaidia timu katika michuano ya CAF na ligi ya ndani kwa kushirikiana na Yakoub Suleiman anayeendelea kuzoea presha ya Simba tofauti na JKT Tanzania alikotokea,” amesema kiongozi huyo.

Kuhusiana na sababu ya kutaka kumsajili beki, kigogo huyo amesema Hamza atachukua muda mrefu kukaa nje, hivyo wanalazimika kutafuta atayesaidiana na Wilsson Nangu, Rushine de Reuck na  Chamou Karaboue.

PANT 02

“Pamoja na Nangu kuanza vizuri, tunatarajia awe na muendelezo wa kiwango chake pia ili mmoja wapo akitokea ameumia kikosi kinakuwa kipana, hiyo ndiyo sababu tunayolazimika kusajili beki wa kati,” amesema kigogo huyo.

Alipotafutwa meneja mkuu wa Simba aliye na taaluma ya ukocha, Dimitar Pantev, amesema: “Desemba tuna uhitaji wa kusajili mshambuliaji wa kati, naheshimu kiwango cha Steven Mukwala aliyemaliza na mabao 13 msimu uliyopita na ni mchezaji mzuri anayejituma, ninachoweza kusisitiza tutaangalia namna mambo yanavyokwenda baina yake na viongozi ambayo napaswa kuyaheshimu pia.”

Japokuwa Pantev hakutaka kufafanua kuhusiana na Mukwala, taarifa za chini ya kapeti zinasema aliyekuwa kocha wa Simba, Fadlu Davids anahitaji kumsajili katika klabu ya Raja Casablanca anayoifundisha.