KLABU ya Al Ahli Tripoli imezidi kuweka presha ya kumtaka kiungo wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’, safari hii ikija na dau jipya, lakini anayekwamisha dili hilo anatajwa ni Kocha Florent Ibenge.
Ikumbukwe, klabu hiyo kutoka Libya iliifuata Azam mara mbili, ikimtaka mchezaji huyo lakini msimu uliopita wakati Waarabu hao wakiwa kwenye harakati hizo, Fei aliongeza mkataba wa mwaka mmoja.
Fei ambaye alisaini mkataba wa miaka mitatu kuitumikia Azam, mwanzoni mwa msimu huu aliongeza tena mwaka mmoja.
Licha ya staa huyo kuwaongezea mlima Waarabu, lakini bado jamaa hawachoki kwani wako radhi kutoa dau lolote ili tu dili hilo likamilike.
Hapo awali, Waarabu hao walishafikia dau la kumnunua mchezaji huyo na walitakiwa kulipa Dola 800,000 (Sh1.9 bilioni za Tanzania), lakini Azam iligoma.
Mwishoni mwa msimu uliopita, kabla ya Fei kuongeza mkataba wa mwaka mmoja, jamaa wakatua tena Azam wakiwa na Dola 1,500,000 (Sh3.6 bilioni za Tanzania), lakini hawakutoboa.
Azam iliendelea kuweka mgomo wa kumwachia kiungo huyo, kwani haikupata mbadala wake bila kusahau kiwango bora alichonacho.
Mwanaspoti linafahamu, kuelekea dirisha dogo la usajili msimu huu, Waarabu hao wamerudi tena na sasa hawataki maneno mengi kwani wameweka mzigo wa kutosha.
Unaambiwa Waarabu wameweka mezani kwa Azam Dola 2,000,000 (Sh4.9 bilioni za Tanzania) ili kuona kama itafanikisha dili hilo la kumng’oa Fei Azam.
Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti, Azam ilishamkubalia Fei watamuuza dirisha dogo la usajili msimu huu.
“Hata Azam ofa hiyo imewapa presha kwani walishamkubalia Fei Toto, kwamba watamuuza dirisha dogo la usajili baada ya kuona kama wangemuuza Agosti mwaka huu ingekuwa ngumu kwao kwenda makundi.”
Azam sasa inashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikijipanga kutua DR Congo kuvaana na AS Maniema Union, huku miongoni mwa mastaa tegemeo ni pamoja na Fei.
Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti, Kocha Ibenge amegoma kabisa kuondoka kwa kiungo huyo kwani anaamini ubora wake utawasaidia sana kimataifa.
“Kocha Ibenge ndiye aliyewaomba mabosi wa Azam kuzuia dili hilo kwa sasa kwani bado hajaona mbadala wa kiungo huyo.
“Lakini kingine kama ataondoka kwenda Al Ahli kwa sasa ni ngumu Azam kupata mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kuwasaidia katika mechi za kimataifa kwani wengi timu walizoko ziko kwenye mashindano hayo.”
Azam itaanzia ugenini Novemba 23, mwaka huu kucheza dhidi ya AS Maniema Union, ikiwa ni mechi ya kwanza Kundi B katika Kombe la Shirikisho Afrika.
