Wapeni watoto wenu mlo wa asubuhi kabla ya kwenda shule

Wazazi na walezi wameaswa kuhakikisha wanawapatia watoto wenye umri wa kwenda shule mlo wa asubuhi kabla hawajaenda shule. Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Mafunzo kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dkt. Eshter Nkuba wakati akizungumza na wazazi na walezi wa shule ya msingi Unubini iliyopo manispaa ya Temeke.

Dkt. Nkuba amesema ni muhimu watoto kupewa mlo wa asubuhi nyumbani ili kumuwezesha asikae na njaa muda mrefu, kwani njaa humpunguzia mtoto umakini wa kusikiliza darasani na hivyo kushidwa kuelewa na kupokea maelekezo atakayopewa na walimu wake.

“Muda wa asubuhi akili ya binadamu hufanya kazi kwa umakini zaidi, ndio maana vipindi vingi vya hesabu shuleni hupangwa muda huo ili kumuwezesha mtoto kupokea na kuelewa kwa urahisi. Lakini mtoto huyo kama atatoka nyumbani asubihi bila ya kula chochote basi atasikia njaa na hivyo ubongo wake kutofanya kazi kwa ufanisi, na matokeo yake mtoto atasinzia darasani ama kukosa umakini wa kumsikiliza mwalimu”

Aidha Dkt. Nkuba amewaomba wazazi pia kuendelea kushirikiana na shule katika kuhakikisha watoto wao wanapata chakula cha mchana shuleni kwani njaa si rafiki wa masomo shuleni.

Kwa Upande wake Afisa Elimu ya Watu Wazima na Nje ya Mfumo Rasmi Manispaa ya Temeke, Mwalimu Donasiana Njuu akimwakilisha Afisa Elimu Manispaa ya Temeke amesema kuwa mpango wa kuwapa watoto chakula cha mchana ni mpango wa kitaifa uliowekwa na Serikali ili kuhakikisha watoto wanapata elimu bora katika mazingira mazuri bila ya kuwepo kwa kizuizi chochote.

“Mpango wa kuwapa watoto chakula cha mchana shuleni si mpango wa Unibini pekee, bali ni mpango wa kitaifa unatekelezwa nchi nzima kupitia waraka wa elimu bure wa mwaka 2016 unaoelezea majukumu ya mzazi ikiwemo kuwanunulia vifaa vya shule kama vile sare za shule na madaftari, lakini pamoja na kuwapatia chakula cha shule”. Amesema Mwalimu Njuu.

Awali wakati akielezea umuhimu wa kuwapa chakula wanafunzi shuleni, Afisa Lishe Mtafiti kutoka TFNC, Eliasaph Mwana amesema kuwa bado kumekuwa na mwitikio mdogo miongoni mwa wazazi katika kuchangia chakula shuleni jambo linalosababisha baadhi ya wanafunzi kukosa chakula. Mwana amesema takwimu zinaonesha kuwa kati ya wanafunzi 100 ni wanafunzi 56 tu ndio wanaopata chakula shuleni.

Mwana amesema kutoka na changamoto hiyo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), pamoja na TFNC wameanzisha mradi wa Afya na Lishe Mashuleni ili kuhakikisha kila mwanafunzo anapata chakula shuleni. Mradi huu unatekelezwa katika shule 15 za msingi katika manispoaa ya Temeke ambazo ni; Lioness Miburani, Unubini, Likwati, Madenge, Charambe, Chemchem, Nzasa, Kilamba, Marten Lumbanga, Amani, Bokorani, Ali Hassan Mwinyi, Mabatini, Umoja na Kibasila

Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Mafunzo ya Lishe, Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dkt. Esther Nkuba akitoa elimu ya lishe kwa wazazi na walezi wa wanafunzi wa shule ya msingi Unubini manispaa ya Temeke ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa  mradi wa Afya na Lishe unaotekelezwa katika shule za msingi 15 za Manispaa ya Temeke.

Mwenyekiti kamati ya wazazi Shule ya Msingi Unubini, Temeke, Albinus Masalu akitoa ahadi ya kuendelea kuhamasisha wazazi na walezi kuchangia huduma ya chakula wanachopewa watoto shuleni mara baada ya kupewa semina elekezi kuhusu umuhimu wa lishe iliyotolewa kwa  wazazi na walezi wa shule hiyo.


Afisa Elimu Watu Wazima Manispaa ya Temeke, Mwalimu Donasiana Njuu akimwakilisha Afisa Elimu Manispaa kufungua semina elekezi kwa wazazi na walezi wa wanafunzi wa shule ya msingi Unubini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa  mradi wa Afya na Lishe unaotekelezwa katika shule za msingi 15 za Manispaa ya Temeke.


Mwenyekiti Serikali ya Mtaa Unubini, Manispaa ya Temeke, Raphael Berege akisisitiza jambo kuhusu umuhimu wa wazazi kuchangia chakula shuleni wakati wa semina elekezi kwa wazazi na walezi wa Shule ya Msingi Unubini inayotolewa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) kupitia mradi wa Afya na Lishe unaotekelezwa katika shule za msingi 15 za Manispaa ya Temeke.
Afisa Lishe Manispaa ya Temeke, Happy Nkunda akielezea umuhimu wanafunzi kupata chakula shuleni kwa wazazi na walezi wa shule ya msingi Unubini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa  mradi wa Afya na Lishe unaotekelezwa katika shule za msingi 15 za Manispaa ya Temeke.

Afisa Lishe Mtafiti  kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Eliasaph Mwana akielezea umuhimu wa watoto wa shule kupewa chakula shuleni  wakati wa semina elekezi iliyofanyika kwa wazazi na walezi wa wanafunzi wa shule ya msingi Unubini manispaa ya Temeke ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa  mradi wa Afya na Lishe unaotekelezwa katika shule za msingi 15 za Manispaa ya Temeke.