Washiriki wa warsha ya mafunzo ya Mfumo wa Kidigitali—Tanzania Chamber Portal (TCP) jijini Arusha wameonyesha mwitikio mkubwa na kutoa pongezi kwa ubunifu wa mfumo huo, wakisema umeleta mwelekeo mpya katika utoaji wa huduma za kibiashara nchini.
Ikiwa ni siku ya pili ya warsha hiyo, iliyoandaliwa na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) na kudhaminiwa na TradeMark Africa, imeendelea kwa mafanikio makubwa huku ikiwakutanisha Maafisa wa Kanda ya Kaskazini pamoja na wadau kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Arusha.
Washiriki wamesisitiza kuwa mfumo wa TCP ni rahisi kutumia, rafiki kwa mtumiaji, na mchango muhimu katika kuboresha huduma za kibiashara nchini. Wameeleza kuwa kupatikana kwa taarifa kwa urahisi, uwazi katika utoaji wa huduma, na kupungua kwa urasimu ni miongoni mwa faida watakazozipata wafanyabiashara pindi mfumo huo utakapotumika kikamilifu.
Aidha, wadau wameutaja mfumo wa TCP kuwa ni hatua ya kimkakati katika safari ya mageuzi ya kidigitali, yenye lengo la kuimarisha mazingira ya biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia sekta binafsi na ushirikiano wa taasisi za serikali.
Warsha inaendelea ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo watumiaji wa mfumo huo ili kuhakikisha kuwa maboresho yanayotarajiwa yanafikiwa na kufikiwa na wafanyabiashara na wadau wote nchini.
*Mwisho*




