FYATU MFYATUZI: Inakuwaje Fyatu mzima anajigeuza au kugeuzwa mdudu?

Kunguni na chawa ni mojawapo ya wadudu wachafu, na hatari bila kusahau wawafugao miongoni mwa viumbe waliolaaniwa tangu walipoumbwa. Ni dhalili, dhalimu, katili, na tegemezi. Hawana akili, aibu, maarifa, wala huruma. Ni hatari, hatarishi, na wabaya hakuna mfano. Hunyonya hata maiti na mizoga.

Ni watumwa wa matumbo yao yasiyoshiba. Huishi kwa kunyonya wengine na kuwasababishia hasara, maradhi, mateso, usumbufu, na vifo. Maumivu ya mirija yao ni makali. Wanaweza kushindana na mbu na funza katika hili. Wanachukiwa na binadamu na wanyama kwa matendo yao ya hovyo na machafu. Ili waishi na kushamiri, wadudu hawa lazima kuwepo na uchafu na watu wachafu wa kuwafuga na kuwalisha kwa faida na sababu wasijuavyo japo ni hatarishi na za hovyo.

Tukiachana na wadudu hawa, kuna mambo wanaweza kutufunza hasa pale binadamu mzima na akili yake anapojigeuza au kugeuzwa mdudu akafanya vitu ambavyo hata wadudu wasingefanya wangekuwa binadamu. Juzi, katika pitapita zangu, nilishuhudia na kusikia mambo ya ajabu.

Mosi, nikiwa mkoa fulani pembezoni mwa kaya, nilimsikia kwa masikio yangu na kumuona kwa macho yangu yote matatu kupe mmoja ajiitaye kiongozi akiongopa mchana kweupe bila aibu wala hofu huku akijigeuza kupe ili kuwashinda chawa. Jamaa, alijitoa kimasomaso na kumpigia kampeni mgombea ‘pinzani’ akagoma kufanya hivyo kwa mgombea wa chama chake. Je, hakujua alichokuwa akifanya? Alihongwa? Alikuwa akijipendekeza ili apewe udohoudoho tena wa aibu? Si rahisi kujibu swali hili na mengine mengi.

 Pili, nilijiuliza bila majibu. Inakuwaje fyatu mzima na akili zake tena mzito kuliko Kabwela anakubali, iwe kwa hiari, kuhongwa, hata kulazimishwa, kujigeuza au kugeuza mdudu. Ili iweje? Kwanini ukubali kuwa mdudu na siyo simba kama unapenda sana kuwa mnyama? Japo wadudu hawafanyi uchangudoa wa kimaadili, kidudu mtu ni changudoa wa kisiasa. Huvi ndiyo njia pekee iliyobaki ya kupata mahitaji, riziki, na ulaji wake? Wewe unamchukuliaje kidudu fyatu huyu? Matumbo yetu yasitufanye tufanyiwe vitu vibaya. Baya zaidi, wanaofanyiwa huu udhalilishaji wana watoi. Sijui wanawafundisha nini watoto wao na wengine?

 Tatu, nilifyatuka na kushangaa, kukasirika, kuhuzunika, na kuudhika. Inakuwaje ‘kiongozi’tena wa chama kinachojiita pinzani, kumwacha mgombea wake, tena baada ya yeye kukacha kugombea urahisi, na kumpigia mgombea pinzani? Hivi hawa siyo wanachamana wa siri wanachojidai kupinga wakati wanaunga? Kweli, huyu anaweza kuaminika hata kwa wanyama?

 Nne, zaidi ya kiongozi huyu muongo ambaye kwake uongozi ni uongo na uroho, ni nini kama siyo kunguni au kupe mtu? Je, anamdanganya nani zaidi ya kujidanganya mwenyewe akidhani anawadanganya mafyatu? Inasikitisha sina mfano kwa ‘kiongozi’ tena mzito kufanya mambo kikunguni na kikupe.

 Tano, tumekuwa tukiwasakama chawa na wale wawafugao tusijue wataibuka hata funza, kunguni, na kupe waje kuturarua na kutuambukiza maradhi kama huyu kupe mtu ninayemjadili leo. Hivi, inakuwaje binadamu mzima mwenye akili timamu, macho, na mikono akatenda kama mdudu na asione aibu wala kuhisi uzito wa dhambi anayojitendea na kuwatendea wengine?

 Sita, kinachogomba na kuuma ni ile hali ya mafyatu kufyatuliwa kuwa uchafu na uchafuzi huu nao ni uchaguzi. Uchaguzi gani usio na wapinzani? Uchaguzi gani ambapo vyama ABCD…Z ‘vinashindana’ vyenyewe. Katika mchezo huu mchafu, kinachoumiza zaidi ni kuunguza na kufyatua njuluku za mafyatu kwa viini macho. Si timu itangaze mteule yake badala ya kupoteza muda na njuluku za mafyatu kapuku? Hata hivyo, nisizoze na kulaumu sana. Hapa, wa kulaumiwa ni mafyatu au wanaowafyatua?

 Saba, japo ni haki ya mtu kuchagua atatakacho, inakuwaje mja anajigeuza mdudu ili ajaze tumbo lisiloshiba asihofie Mungu na kesho? Je, hapa anayewafyatua mafyatu na mafyatu nani alaumiwe? Huku si kukubali kuliwa kwa hiari yao? Je, wakishafanya na kufanyiwa udhalilishaji huu, watakuwa na haki ya kulalamika au kulaumu? Wamlalamikie au kumlaumu nani wakati yote wanasababisha wao wenyewe kwa kukataa kufyatuka na kufyatua kiasi cha kujiruhusu wafyatuliwe hata na wadudu wasio na akili, maarifa, wala nguvu? Jamani, tunamkomoa nani ili iwe nini na kwanini? Kweli, mafyatu na ufyatu wetu tunashindwa hata kuwapondaponda au kuwasafishia mbali hawa wadudu ambao sasa wanaanza kujifanya hawahusiki na mateso yetu? Inakuwaje wadudu wanaonekana kutuzidi akili hadi tunakubali watufyatue tena kirahisi hivi?

 Nashaurini mafyatu kuepuka uchawa, ufunza, ukunguni, ukupe, na ududu kwa gharama zozote. Kwani, mtajikuta pakanga kama kaya. Licha ya kudhalilisha na kuumiza, hali hizi hudumaza ubunifu na uthubutu kiasi cha fyatu mzima kukubali kujigeuza au kugeuzwa jidudu. Shame on you vidudu watu muwe wafugaji au wafugwao. Heri kufa njaa kuliko kukubali aibu, jinai, na shibe hii ya kudhalilishwa na kudhalilisha. Mtaliwa mkijiona. Shauri yenu. Sitaki, siku moja, mseme sikusema wakati nilisema kila mara. Inakuwaje Fyatu mzima anajigeuza au kugeuzwa mdudu?