Mwanamuziki Perer Tosh aliimba kuhusu haki sawa na amani. Alisema kila mtu analilia amani lakini hakuna anayepambania haki. Akaongeza kuwa kutokana na hilo, yeye hahitaji tena amani, bali anachohitaji ni haki sawa. Kwa haraka unaweza kudhani huyu jamaa kachanganyikiwa, lakini ana maana kubwa. Magurudumu ni sehemu ya gari, lakini huwezi kushika gurudumu ukasema una gari.
Haki na amani ni vitu vinavyokwenda sanjari; hakuna amani pasipo haki. Hata kama kuna utulivu kiasi gani, lakini mtu anayekosa haki anaweza kuitafuta na kusababisha aonekane kuwa ni tishio la amani. Ikumbukwe kuwa wapigania uhuru walikuwa wasumbufu kwenye Serikali za kikoloni. Kwa mfano Mandela alionekana msumbufu kwenye nchi huru ya Afrika ya Kusini. Ni kwa sababu aliisaka haki.
Tosh alitoa mfano hai kwamba kila mmoja anapenda kwenda peponi, lakini hakuna mmoja wao anayetamani kufa. Na hakuna binadamu aliyewahi kuingia peponi kama anayekwenda kusalimia ndugu wa mtaa wa pili. Ni lazima afe kwanza ndipo aionje pepo. Na haijalishi ni mtindo upi utakaompelekea kifo; iwe ugonjwa, ajali au usingizi, kila kilichozaliwa ni lazima kife kwanza ndipo kiende peponi.
Watanzania tungali tunaomboleza vifo vya wenzetu vilivyotukia katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu. Kwa watu waliozoea amani kama sisi, huu ni msiba mkubwa sana. Hapa nchini tumezoea kuona hata watu waliogombana wakifarijiana misibani. Kulingana na utamaduni wetu, msiba wa mwanajamii mmoja huwa ni msiba wa jamii nzima. Hiki ndicho kinachothibitisha udugu wetu.
Vijana wa kileo wametajwa zaidi kuhusika na vidonda vilivyotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu. Wengi waliangukia magerezani, huku wenzao wakipatwa na umauti na wengine wakiachwa na ulemavu. Nashukuru mama umelitazama hili kwa ukubwa na kuziagiza mamlaka ziwaangalie upya hawa walio magerezani kwani wamo wanaofanana na mijusi walionasa kwenye mtego wa panya.
Lakini inatupasa kuwatazama vijana hawa kwa macho ya kipekee sana. tukirudi nyuma kidogo, tunaona kuwa wao hawakujipeleka pale walipo sasa, bali ni mifumo ya kidunia ndiyo iliyowafikisha hapa walipo. Wazee wao waliandaliwa masomo yaliyowalinda kwenye uzalendo wa nchi yao hadi walipostaafu. Lakini dunia ilipoingia kwenye utandawazi, hakuna mzazi aliyekubali mwanawe asome vitabu vya “Kibanga ampiga Mkoloni”.
Uzalendo uliachwa kusisitizwa kutoka shuleni hadi makazini. Kulingana na hali yetu ya kiuchumi na tatizo la ajira, utandawazi uliibuka kuwa kimbilio la vijana wengi waliojaribu kujiajiri kwa kutumia mifumo ya ajira isiyo rasmi (ya kuajiriwa Serikalini). Hii ndiyo sababu kubwa iliyopelekea kubadilika kwa mitindo ya maisha kulikosababisha maporomoko ya maadili ya Mtanzania.
Wengi wamefurahishwa na hotuba yako ya kulizindua Bunge, hasa baada ya kusikia nia yako ya kuunda Wizara kamili ya vijana. Ni mpango mzuri sana kwani Waswahili hunena “Kila zama huja na nabii wake”. Vijana wetu wana namna yao ya kufikiri, kuelekezana, kukoseana na hata kusuluhishana. Hivyo hatuwezi tena kuwahukumu kwa mila na tamaduni, tukifanya hivyo tutakuwa tunawaonea.
Kwa maoni yangu Wizara yao ibebwe na vijana wa aina yao. Wenyewe ndio watakaoweza kusikiliza changamoto zao, na kuelewana namna ya kuzimaliza. Mwisho wa siku Waziri wa Vijana atayaleta mezani na itakuwa rahisi kushughulikia utatuzi wake. Hivi sasa ni vigumu kwao kuleta mapendekezo yao bungeni, ni dhahiri hakutakuwa na maelewano baina yao na Bunge.
Nitatoa mfano wa mbwa. Mnyama huyu kama walivyo wanyama wengine wawindaji, huwa na upofu wa rangi. Wao hutambua rangi nyeusi na nyeupe tu. Mchana ataona maumbo meusi na usiku atayaona meupe. Humtambua rafiki au mmiliki na familia inayomtunza kwa harufu zao. Na huyasikia maongezi yao kwa lugha yake tu. Mnapomwambia: “Wewe ni mbwa hodari” yeye husikia “Wuh wuh wuh…”
Nakumbuka siku moja wazazi wangu walikuja kunitembelea kwenye Shule ya Upili. Wakati nikiwatembeza kwenye maeneo ya shule, tulikutana na rafiki tuliyemwita Bisu. Nilimwuliza Bisu imekuwaje akafunga bandeji mkononi, alichojibu kiliwafanya wazazi watazamane kwa mshangao. Alisema: “Ah jana mida ya popo nilikutana na makokoni, wakanipiga ngeta wachukue mapene nikachomoa, si wakanikata kachumbari…”
Ndio maana nasema ni busara kuwaundia vijana Wizara itakayokuwa jukwaa lao la kujadii mustakabali wao. Potelea mbali wasipoeleweka na yeyote zaidi ya waziri, naibu waziri na makatibu, ambao wote ni lazima wawe vijana wenzao. Itafanana kidogo na nafasi maalum iliyobuniwa kwa makundi ambayo hayana nafasi ya kusikika kama wengine.
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi, idadi ya vijana hapa nchini inafika asilimia sitini. Hii ina maana kuwa vijana ndiyo idadi kubwa zaidi ya Watanzania. Hawa ndio nguvukazi ya Taifa, wanapokosa kazi inamaanisha kudorora kwa uchumi. Kwa tafsiri nyepesi, kudorora kwa uchumi wa nchi ndiko kutopea kwenye janga la umasikini kwa nchi yoyote.
Vijana wasiposhirikishwa kwenye mambo yanayowahusu, kuna hatari ya kulichukia Taifa lao hasa ukizingatia kwamba hawakukuzwa kizalendo. Hatari inakuwa kubwa zaidi pale mamluki wanapoweza kuingia kwenye matamanio yao. Hivyo nasisitiza kuwa kuwapatia majukwaa yao lisiwe jambo mzaha, bali wenyewe walione likizingatiwa na kupewa vipaumbele vya kutosha.
