Safari ndefu kwa Zanzibar kusaka maridhiano ya kweli

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, ametangaza Baraza jipya la Mawaziri huku akiacha nafasi nne mahsusi kwa ajili ya Chama cha ACT-Wazalendo, ili kufanikisha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa mara ya nne.

Mfumo huu si zawadi ya kisiasa bali ni matokeo ya mabadiliko ya kikatiba yaliyobarikiwa na kura ya maoni ya Julai 31, 2010, ambapo asilimia 66.4 ya Wazanzibari waliridhia kuanzishwa kwa SUK kama njia ya kudumisha utulivu wa kisiasa.

Kura ya maoni ililenga kuondoa misuguano ya muda mrefu kati ya CCM na CUF, ambayo sasa wengi wa wanachama wake wapo ACT-Wazalendo, migogoro iliyowahi kusababisha vifo, ulemavu, yatima na matukio ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Katika chaguzi za nyuma, kumeshuhudiwa uporaji wa mali, nyumba na magari kuchomwa moto, miundombinu kuharibiwa, pamoja na vitendo vya udhalilishaji kama kuweka kinyesi katika visima na shule.

SUK ilitarajiwa kuwa muundo unaoweza kufungua njia ya maisha yasiyo na ubaguzi, vitisho, au kesi za kubambikiziwa.

Hata hivyo, licha ya Zanzibar kuwa na SUK mara tatu, bado haijapatikana tiba kamili ya janga la siasa za uhasama. ACT-Wazalendo inadai kuwa CCM haijawahi kuwa na dhamira njema katika kuheshimu misingi ya muafaka.

Kauli za viongozi wake, akiwamo Mwenyekiti Othman Masoud Othman, zinatuhumu CCM kuweka mbele ujanja wa kisiasa kuliko maslahi mapana ya nchi.

ACT – Wazalendo inasisitiza kuwa kila kunapojitokeza dalili za maridhiano, CCM huendeleza kile wanachokiita “funika kombe mwana haramu apite,” wakimaanisha kutokuonyesha dhati ya kushirikiana.

Kwa mujibu wa ACT – Wazalendo, mara mbili mchakato wa SUK uliishia njiani na hata muafaka uliopita kabla ya uchaguzi ulionekana kuwa wa kiitikadi tu bila kutekelezwa kwa vitendo.

Miongoni mwa malalamiko yaliyoibuliwa ni pamoja na matumizi mabaya ya madaraka, kutoshirikishwa kwa ACT – Wazalendo kwenye uteuzi wa viongozi, hata katika ngazi ya masheha, kana kwamba nafasi hizo ni za watu wa CCM pekee.

Pia, wamelalamika kuhusu kutotekelezwa kwa makubaliano ya kuwa na tume huru ya uchaguzi na kuondoa kura ya mapema, ambayo wanadai imevunja katiba.

Malalamiko kuhusu kura ya mapema yalisindikizwa na video zilizosambaa mitandaoni zikionyesha makundi ya watu na watoto waliovaa sare zinazofanana na za vikosi vya ulinzi wakipiga kura katika vituo vilivyodaiwa kuvamiwa.

ACT – Wazalendo inadokeza kuwa ilishinda majimbo 32 kati ya 50 na kwamba, hakuna anayeelewa mantiki ya chama hicho kupoteza karibu majimbo yote ya Unguja, eneo ambalo linaonekana wazi kuwa ngome yao.

Aidha, wamehoji sababu ya maafisa wa vikosi vya ulinzi kupiga kura hata katika maeneo yasiyo na kambi za majeshi.

Maswali mengine yanayobaki bila majibu ni kwa nini matokeo ya uchaguzi wa Rais, Wawakilishi na Madiwani yanatofautiana katika baadhi ya vituo, jambo linalojenga shaka kwa kuwa kila mpigakura hupokea karatasi tatu kwenye kituo kimoja.

Pia, hakuna ufafanuzi juu ya video zilizoonyesha makarani wa vituo wakipiga kura tarehe 29 Oktoba badala ya siku iliyotangazwa awali.

Hivi sasa, mjadala wa kuundwa upya kwa SUK umeibuka, lakini ACT – Wazalendo inasisitiza kuwa jambo la msingi kwao si kuingia serikalini bali kupigania kile wanachokiita ushindi wao ulioporwa.

Wanasisitiza kuwa hawamtambui Rais Mwinyi kwa madai kwamba hana ridhaa halali ya wananchi. Hapa ndipo panapoonekana kuwepo pengo kubwa la maelewano ya kisiasa na kitendawili kuhusu nani anaweza kusaidia kufungua njia ya makubaliano ya kweli.

Kwa upande mmoja, CCM inasisitiza umuhimu wa amani, utulivu na umoja kwa maendeleo ya nchi; kwa upande mwingine, ACT – Wazalendo inasema misingi hiyo haiwezi kujengwa bila haki, kwa sababu kukosekana kwa haki kunazaa migogoro na machafuko.

Wananchi wengi wa Zanzibar wanaeleza wasiwasi wao, wakihisi mustakabali wa mbele umefunikwa na mawingu mazito huku wanasiasa wakielekea kwenye mielekeo tofauti.

Hatua yoyote ya kuundwa upya kwa SUK itahitaji kuzingatia dosari zote zilizojitokeza kwenye uchaguzi uliopita na kuhakikisha zinashughulikiwa kisheria.

Hapo ndipo pa kuanzia safari mpya ya maridhiano na kujenga mfumo unaoheshimu haki, uwajibikaji na ushirikishwaji wa kweli. Bila hivyo, jitihada zozote za kuunganisha pande zilizo mbali zitabaki kama kutaka kupunguza chumvi ya maji ya bahari kwa kuongeza sukari.