Geita. Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limekiri kumkamata Dk Kibaba Michael kutokana tuhuma mbalimbali za kijinai ambazo hazijawekwa wazi, ambapo imeelezwa kuwa tayari uchunguzi umekamilika dhidi yake.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatano Novemba 19, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo jeshi hilo limekiri kumshikilia daktari huyo kwa makosa ya kijinai yanayomkabili.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limemkamata na linaendelea kumuhoji Dk Kibaba Michael, mkazi wa Manispaa ya Geita . Sababu za kumkamata ni kutokana na ushahidi uliokuwa umekusanywa kuhusiana na tuhuma mbalimbali za kijinai anazotuhumiwa nazo.’
Taarifa hiyo bila kuwataja watu wengine anaoshirikiana nao katika makosa hayo ya jinai, imeeleza kuwa linakamilisha uchunguzi ili mtuhumiwa huyo achukuliwe hatua za kisheria pamoja na anaoshirikiana nao.
“Uchunguzi uliobakia unakamilishwa ili hatua nyingine za sheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake na anaoshirikiana nao,”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kauli ya jeshi hilo inakuja baada ya kuibuka kwa taarifa katika mitandao ya kijamii ikieleza kuwa Dk Kibaba Furaha anayefanya kazi katika Hospitali ya Manispaa ya Geita akiwa mratibu wa mpango wa kudhibiti Malaria, kudaiwa kutekwa na watu wasiojulikana. Pia ilidaiwa kuwa Dk Kibaba alivamiwa na watu waliokuwa na silaha akiwa katika kibanda chake cha biashara mtaa wa Aziboni na kuondoka naye, huku watu hao wakichukua pia simu yake na kompyuta mpakato aliyokuwa nayo.
Rais wa Chama cha Madaktari nchini, Dk Mugisha Nkoronko akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu amekiri kupokea taarifa hiyo, ambapo amesema kuwa wamekuwa wakifanya ufuatiliaji kupitia Jeshi la Polisi na kulitaka jeshi hilo kumfikisha mahakamani kwa mujibu wa sheria.
‘”Kwa kuwa ni mambo ya kijinai, tunataka Polisi iendelee na shughuli zake kwa uwazi ikiwemo kumfikisha mahakamani kwa mujibu wa sheria, ndiyo tutajua makosa yake yanaangukia kwenye eneo gani.”
“Kwa kuwa taarifa ya Jeshi la Polisi imeeleza inamshikilia, tofauti na hapo nyuma ilivyokuwa, tunashukuru kusikia kuwa ni mzima na tuendelee kuwataka wenzetu wanaotekeleza sheria kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani , Jeshi la Polisi, kukamilisha utaratibu wa kumshtaki rasmi ufuatie,tunaendelea kushirikiana na familia pamoja na wadau wenye nia njema na taaluma ya udaktari kuona haki inatendeka kwa daktari mwenzetu,”amesema Dk Nkoronko.
