RAUNDI ya pili ya Ligi Kuu Soka Wanawake (WPL) itaendelea tena leo Novemba 19, 2025 zikipigwa mechi tatu baada ya raundi ya kwanza kuchezwa idadi kama hiyo, Novemba 14, 2025 ambapo Simba Queens iliichapa Bilo Queens mabao 4-0, Yanga Princess ikiitandika Ruangwa Queens 3-0 na Geita Queens iliyopanda ligi msimu huu ikiondoka na pointi tatu mbele ya Ceasiaa Queens kwa ushindi wa 1-0.
Sasa leo ligi hiyo itaendelea ambapo baada ya Geita kupata ushindi mechi ya kwanza, ina kibarua kingine cha kutafuta alama dhidi ya Fountain Gate Princess, mechi itakayopigwa Uwanja wa Nyankumbu, huku Alliance Girls ikicheza dhidi ya Ceasiaa Queens kwenye Uwanja wa Nyamagana na Simba Queens dhidi ya Bunda Queens, KMC Complex.
Baada ya mechi hizo, ratiba inaonyesha ligi itasimama kwa siku tisa kupisha kalenda ya FIFA kwenye mashindano ya kufuzu michuano ya Futsal na WAFCON itakayoanza Novemba 24 hadi Desemba 2 mwaka huu.
Baada ya michuano hiyo, Desemba 8, 2025 zitamalizwa mechi za viporo JKT Queens iliyokuwa nchini Misri ikishiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake itakipiga na Bunda Queens kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo na Tausi ikiikaribisha Mashujaa Queens Dimba la KMC Complex.
Mechi za raundi ya pili viporo, Tausi itaumana na Yanga Princess, JKT Queens vs Bilo Queens na Ruangwa dhidi ya Mashujaa.
Akizungumzia maandalizi ya mechi kocha wa Alliance Girls, Sultan Juma alisema wanafahamu ugumu wa mechi hiyo lakini malengo yao ni kuchukua pointi tatu.
“Zinapokutana akademi mara nyingi mechi inakuwa ngumu, tunawafahamu Ceasiaa aina yao ya uchezaji, kwetu tunazitaka pointi tatu zisalie nyumbani ingawa haitakuwa rahisi,” alisema Juma.
Kocha msaidizi wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi’ alisema wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaondoka na pointi tatu.
