Dodoma. Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma imeagiza mshtakiwa namba 18 katika kesi ya makosa ya uhaini, Mansoor Omarin, kuendelea kupatiwa matibabu ya jeraha la mguu ili kurejesha afya yake katika hali ya kawaida huku akiendelea kushikiliwa mahabusu.
Omarin na wenzake 17 walifikishwa mahakamani leo, Jumatano Novemba 19, 2025, mbele ya Hakimu Mkazi Getrude Missana kwa ajili ya kutajwa kwa kesi hiyo.
Hata hivyo, upande wa mashtaka ulieleza kuwa upelelezi bado haujakamilika na hivyo wakaomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa shauri hilo.
Waliofikishwa mahakamani leo ni Fabianis Matunda, Hamad Malamila, Shauri Membe, Omary Mweyombwe, Andrea Joseph, Waziri Dafi, Ismail Sweleihe, Saimon Chabazungu, Magohe Wambura, Shafii Magesa, Idd Bakari, Joshua Msihi, Baraka Juma, Yuda Masagati, Amani Stephano, Anord Everian, Hosea Mushi na Mansoor Omarin.
Awali, wakili wa washtakiwa hao Anselm Mwampoma alitaka kujua maendeleo ya afya ya mshtakiwa huyo baada ya kushindwa kusimama wakati kesi yao inatajwa.
“Nataka kujua maendeleo ya mshtakiwa namba 18, Mansoor Omarin anaumwa katika mazingira gani na kama amepata msaada wowote wa matibabu kwa sababu hatujapata muda wa kuzungumza na washtakiwa tujue wanaendeleaje huko mahabusu,” amesema Mwampoma.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Gothard Mwingira aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa huyo yupo chini ya uangalizi wa Jeshi la Magereza na kuiomba mahakama iruhusu askari wa magereza kutoa taarifa kuhusu hali yake.
Ombi hilo lilikubaliwa na mahakama, na askari wa magereza aliyejitambulisha kwa cheo cha Mkaguzi Msaidizi Mkuu aliieleza mahakama kuwa mshtakiwa anaendelea kupatiwa matibabu ya jeraha la mguu akiwa mahabusu.
“Mshtakiwa huyu alipokelewa mahabusu akiwa na jereha hilo mguuni na anaendelea kupata matibabu na hali yake inazidi kuimarika,” amesema askari magereza huyo.
Baada ya maelezo hayo Hakimu Missana aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 3, 2025 kesi hiyo itakapotajwa tena huku washtakiwa wakiendelea kuwa mahabusu.
