Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Masoko na Mahusiano wa benki ya Absa Tanzania, Aron Luhanga amesema benki hiyo inathamini pamoja na kusimamia stori za mafanikio ya wateja wao.
Msingi wa kauli hiyo unatokana na benki hiyo kuwazawadia washindi wa kampeni ya miezi mitatu ya ‘Ujanja ni Kuswipe na Benki ya Absa’ iliyozinduliwa Septemba 30, 2025.
Kampeni hiyo maalumu inayohamasisha matumizi ya huduma za kidijitali na kadi za benki, lengo lake kuu ni kuhimiza Watanzania kutumia zaidi njia za malipo salama, rahisi na za kisasa badala ya kubeba fedha taslimu.
Kampeni hiyo ikiwa na washindi sita wa Sh500,000 kila wiki; mshindi wa Sh3 milioni, Sh5 milioni na Sh10 milioni kila mwezi na mshindi mmoja wa mwisho wa Sh10 milioni ambapo benki hiyo imetenga jumla ya Sh120 milioni kama zawadi kwa washindi watakaopatikana katika kampeni yote.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, leo Jumatano, Novemba 19, 2025, Luhanga amesema tukio hilo linadhihirisha kwa vitendo kauli mbiu ya benki hiyo isemayo ‘Stori yako ina Thamani’ hivyo kwa kuwazawadia washindi hao inaonesha ni jinsi gani Benki ya Absa Tanzania inavyothamini stori za mafanikio ya wateja wao.
Ikumbukwe miongoni mwa faida zake ni bima ya safari za kimataifa, kupata huduma za chakula, vinywaji na mapumziko katika viwanja vya ndege zaidi ya 1,200, bei ya punguzo katika manunuzi, bima ya kufuta tiketi za safari, na udhamini wa bidhaa za muda mrefu.
Mmoja wa washindi wa wiki, Dk Heri Marwa amesema kutokana na kusafiri sana nje ya nchi, kadi ya Absa Infinite Credit imemsaidia kupata huduma zikiwemo manunuzi ndani ya ndege na katika viwanja vya mbalimbali vya ndege, ambapo hapo awali alishindwa kuzipata wakati akitumia kadi za kawaida.
