Watuhumiwa 93 kesi za uchaguzi wafikishwa mahakamani, waangua vilio

Mwanza. Watuhumiwa 93 wamefikishwa mahakamani kwa mara ya pili wakikabiliwa na mashtaka mawili ya kuharibu mali na unyang’anyi wa kutumia silaha, huku upande wa Jamhuri ukitakiwa kukamilisha ushahidi haraka.

Shauri hilo limetajwa kwa mara ya pili mahakamani leo Jumatano, Novemba 19, 2025 katika Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana, Mwanza mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Amani Sumari. Kwa mara ya kwanza ilitajwa Novemba 7, mwaka huu.

Watuhumiwa hao ni miongoni mwa 172 waliofunguliwa mashtaka mbalimbali wilayani Nyamagana kutokana na matukio ya vurugu yaliyotokea baada ya Uchaguzi Mkuu kuanzia Oktoba 29 hadi 31, mwaka huu.

Baadhi ya watuhumiwa wakitoka mahakamani leo baada ya kusomewa kwa mara ya pili kesi inayowakabili katika Mahakama ya wilaya ya Nyamagana, Mwanza. Picha na Damian Masyenene

Upande wa Jamhuri katika shauri hilo umewakilishwa na mawakili Bitunu Msangi na Prince Masawe, huku utetezi ukiwakilishwa na mawakili kutoka Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Duttu Chebwa na Beatus Linda.

Ambapo, wakati wanafikishwa mahakamani mamia ya wananchi wamejitokeza kwa kujua hatima ya ndugu zao, huku wakiwa na matarajio ya kuachiwa kutokana na agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuvitaka vyombo vya dola kuchuja watuhumiwa hao na kuwaachia wale waliotenda makosa kwa kufuata mkumbo.

Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Bitunu Msangi amewasilisha ombi la kubadilisha hati ya mashtaka ili kuongeza washtakiwa wengine sita ambao walikuwa hawajajumuishwa hapo awali.

Amewasilisha maombi hayo kwa mujibu wa kifungu cha 251 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura namba 20 marejeo ya mwaka 2023, huku akiomba muda zaidi (siku 90) wa kufanya upelelezi kwa kuwa bado haujakamilika.

Hata hivyo, upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Duttu Chebwa ulipinga hoja hizo ukiita Jamhuri ieleze bayana ni mashtaka yapi ambayo upelelezi haujakamilika, huku akisisitiza kwamba kosa la kwanza la kuharibu mali maelezo yanataja mali zilizoharibiwa na maeneo lakini anashangazwa kwnini upelelezi haukamiliki.

“Kwenye maelezo ya mashtaka inaeleweka wazi mali zilizoharibiwa ni za halmashauri ya Nyamagana, sasa wanahitaji maelezo mengine yapi kukamilisha ushahidi,” amehoji Chebwa.

Akijibu hoja hiyo, Wakili wa Serikali, Bitunu Msangi amesisitiza kwamba wanaposema ushahidi haujakamilika wanamaanisha makosa yote mawili na siyo kazi nyepesi kama upande wa utetezi unavyotaka iwe.

“Siyo kazi rahisi inapaswa kuwa na maelezo ya kina na ya kutosha kwa sababu ni watu wengi ambao waliharibiwa mali zao, hivyo tunaomba tarehe nyingine tuone tutakuwa tumefikia wapi,” amesema Msangi.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana, Amani Sumari amelikubali ombi la upande wa mashtaka la kurekebisha makosa yote yaliyopo kwenye hati ya mashtaka ili watuhumiwa wasomewe upya kesi hiyo itakapotajwa tena.

Hakimu Sumari ameitaka Jamhuri kukamilisha ushahidi wa kosa la kwanza (Kuharibu mali) kwa kufanya mawasiliano na vyombo vya upelelezi na kufanya marekebisho kwa sababu kwenye hati ya mashtaka imeeleza uharibifu ulifanyika kata ya Isamilo na mali zilizoharibiwa ni za halmashauri ya Nyamagana ambayo kisheria haipo, bali inayotambulika ni Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

“Kosa la kwanza upelelezi ukamilishwe, tunataka tujue upelelezi umefikia wapi. Kosa la pili ni kubwa upelelezi unahitaji muda,” amesema Sumari.

Baada ya maelezo hayo, ameliahirisha shauri hilo hadi Desemba 2, 2015 saa 3:30 asubuhi kwa ajili ya kutajwa tena, ambapo watuhumiwa wataendelea kubaki rumande.

Uamuzi huo wa hakimu ukaibua vilio kwa washtakiwa ambao walikuwa na matumaini ya kuachiwa, huku wakinyoosha mikono ya kutaka kuzungumza kilichopo moyoni ambapo hakimu amewasikiliza huku hoja zao zikiwa ni kwamba wameonewa na kunung’unika kuendelea kusota rumande kwa makosa ambayo hawayajui.

Hata hivyo, Hakimu Sumari amewapa ufafanuzi kwa nini shauri linachukua muda mrefu, huku akiwataka wavute subira wasione kama wanaonewa.