SAFARI ya mafanikio huanza kwa maumivu kwa sababu kila hatua ya ukuaji inahitaji uvumilivu, kujitolea na kupambana na changamoto.
Maumivu hayo ndiyo yanayomtengeneza mtu kuwa imara, kufundisha nidhamu na kumpa thamani ya anachopata baadaye, lakini ndani ya kila uchungu kuna nguvu ya kumuinua, kumtengeneza na kumuandalia ushindi.
Hali hiyo inaikumbusha jamii ya wanamichezo kiungo mshambuliaji wa Azam, Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ ambaye sasa anafanya vizuri akiwa na kikosi hicho pamoja na timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na ile ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’.
Fei hakufika hapo kwa bahati, bali kipaji na uvumilivu wake ndivyo leo vinamfanya atajwe kuwa mmoja wa viungo bora wa ushambuliaji hapa nchini.
Wengi watakuwa wanakumbuka sakata lake akiwa Yanga kwani alipotaka kuhama timu hiyo msimu wa 2022-2023 baada ya kuitumikia tangu mwaka 2018 haikuwa rahisi, lakini mwisho wa siku mambo yakawekwa sawa akahamia Azam kuanzia msimu wa 2023-2024 na hadi sasa.
Ubora wa Fei Toto alionao sasa, ulionwa miaka mingi na kocha Mohamed Salah maarufu Rijkaard ambaye amezungumza na Mwanaspoti mambo mengi kumuhusu kiungo huyo sambamba na maisha yake binafsi.
Kocha huyo ambaye umaarufu wa jina lake umetokana na nyota wa zamani wa Uholanzi, Frank Rijkaard aliyewahi kucheza klabu kadhaa ikiwamo AC Milan sambamba na kuifundisha Barcelona na nyinginezo, anasema Fei Toto anastahili kufika mbali zaidi ya alipo sasa.
Katika mahojiano hayo na Mwanaspoti yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Maisara vilivyopo mjini Unguja, kocha huyo alionekana kutabasamu zaidi aliposikia jina la Fei Toto likitajwa mbele yake huku akiwa na mshangao uliochanganyika na furaha, kicheko na huzuni kwa mbali.
Rijkaard anasema katika kipindi ambacho Fei Toto ana mgogoro na Yanga, alimuaminisha kwamba kuna leo na kesho kwa kumkumbusha anayoyapitia ipo siku yatakwisha wala hapaswi kufa moyo kwa sababu ana safari ndefu ya kuandika historia ya kitabu chake.
“Wakati ule haukuwa mzuri wala wenye afya kwa sababu aliowategemea ndio ambao walimkimbia wakati wa shida. Sikuchoka kusimama naye nikiamini kwamba anastahili kufika mbali zaidi ya alipo,” anasema.
Licha ya yaliyotokea, anasema Fei alikuwa sahihi kuchagua upande ambao una maslahi kwake na familia yake na hakusita kutumia muda huo kumuomba Mungu.
“Hali ilikuwa ngumu kwangu. Sikuwa natembea wala kulala usingizi mnono hadi hali hiyo ilivyotulia, lakini Fei ilikuwa sahihi kuchukua uamuzi huo japokuwa wengi walikaa pembeni na wachache ikiwemo familia yake pekee ndio ilisimama naye,” anasema Rijkaard.
Kocha huyo anasema halikuwa jambo la kushangaza na kufikirisha kwa simu ya Fei kukaa siku nzima bila kuita ingawa hajazoea hilo.
Upepo ulibadilika baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuiomba Yanga imuache Fei ili aweze kucheza mpira na kuachana na mgogoro.
Anasema wakati wanatoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar, hapo simu ndipo ilipoanza kuita na wengi walitamani kutambua mustakabali wake.
“Watu wengi walitaka kumuona Fei akipotea katika ramani ya soka Tanzania kwani walitumia maneno yenye kumchafua na yote hayakusaidia kwani neema ya Mungu ni kubwa kuliko ya binadamu,” anasema kocha huyo.
Mbali ya mgogoro huo, anasema Fei alikuwa akiutumua muda huo kufanya mazoezi ya kutosha kwa kujiweka imara na hakutoa nafasi kumtoa katika mstari wake.
Anaeleza kuwa kila mwezi walikuwa wanakwenda Bara kufanya mazoezi na muda mwingi walifanyia Zanzibar hadi sakata hilo lilipomalizika. Rijkaard anasema suala hilo ni miongoni mwa mambo yaliyompa presha kubwa wakati huo na hatasahau.
Rijkaard anasema: “Fei anapenda zaidi kufurahi na watu akiwa nje ya uwanja, mkweli na anapendelea zaidi kucheza gemu za mpira kwa sababu hapendi kuwa na mawazo.
“Akiwa uwanjani anafanya majukumu yake na nje ya mpira anafurahi na wengine. Umaarufu wake haumzuii kuchangamana na watu wasiokuwa maarufu.
“Kwa sasa anafurahia zaidi jina lake likitajwa vizuri vinywani mwa watu na hayo yote ni matunda ya uvumilivu wake.”
WALIVYOKUTANA Rijkaard anazungumza namna alivyokutana na Fei Toto akisema ni zaidi ya miaka 10 iliyopita.
“Kwa mara ya kwanza nilimuona katika timu za watoto akiwa na umri kati ya miaka 14 hadi 15. Nikavutiwa naye. Kipindi hicho alikuwa anacheza katika timu ya Aston Vila (Zanzibar) na nilivyoenda (kwao) usiku kumchukua nilifukuzwa na mbwa huku wakidai hawawezi kunipatia,” anasema.
Rijkaard anasema bahati nzuri alifanikiwa kumnunua na kuhamia katika timu yake ya Chrisc Zanzibar akiwa na heshima, nidhamu na kujiamini zaidi kwa uchezaji wake.
Kocha huyo anasema kabla ya Fei Toto kujiunga na JKU kulikuwa na timu ya Taifa Jang’ombe ambazo zote zilikuwa zikihitaji huduma yake na hapo ndipo alipomueleza kwamba ikiwa anahitaji mashabiki, basi ajiunge na Taifa Jang’ombe, lakini kama anataka kucheza mpira wenye mafanikio asaini JKU.
Rijkaard anasema sababu ya kumtaka kufanya hivyo alishauona mwelekeo wake na alitambua JKU itamsaidia kutimiza ndoto zake kwa urahisi kwani ni miongoni mwa timu kubwa zinazofanya vizuri Zanzibar na hushiriki mashindano makubwa ya ndani na nje ya nchi.
Anasema anafurahishwa kumuona Fei Toto akiwa katika nafasi nzuri na sasa amekuwa kioo kwa wachezaji wengine Tanzania na imani yake ni kufanya vizuri zaidi.
Akitoa ushauri kwa mchezaji huyo, kocha huyo anamsihi kulinda jina kwani bado anamuombea apate nafasi ya kucheza soka la kimataifa kwa sababu uwezo anao.
Rijkaard anasema kwa sasa anamuona Mohammed Kwacha kuwa mrithi wa Fei, hivyo anamuandaa kijana huyo kuendeleza atakapofika Fei siku za usoni.
Anasema Kwacha ni mchezaji anayemjenga katika misingi ya soka na amefanikiwa kucheza timu ya Taifa ya Zanzibar U17, Azam U15 na sasa Malindi inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar.
Kwa sasa Rijkaard ni kocha msaidizi wa Malindi akionekana kuleta ushindani na hamasa ndani ya Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), kwa mbwembwe na aina mbalimbali za ushangiliaji wake.
Kocha huyo amekuwa kivutio cha mashabiki na wadau wa soka visiwani humo na anajivunia hilo kwa sababu anadai ana mitindo tofauti kulingana na mechi.
Wakati akipiga stori na Mwanaspoti, Rijkaard anasema alianza safari ya ukocha kwa kulipwa Sh1,000 na mmoja wa makocha huko Zanzibar.
Anasema kwa wiki alikuwa anapokea takribani Sh6,000 na aliridhia malipo hayo kwa lengo la kutimiza ndoto zake.
Anasema amekutana na changamoto nyingi katika safari hiyo ambazo hakuzipa nafasi kumuondoa katika mwelekeo wa malengo yake kwani anaamini kwamba mtu akitaka kufika salama safari hapaswi kuziogopa changamoto, hivyo maneno ya watu hayamuathiri na chochote.
Kuhusu jina la Rikaard anasema alipewa na washkaji zake kutokana na kumpenda kocha huyo wakati anafundisha Barcelona na pia alikuwa akivutiwa na naye kuanzia kuvaa hadi anavyokaa katika benchi la ufundi la kikosi chake.
Kabla ya kuwa kocha, kocha huyo aliwahi kucheza soka katika nafasi ya kiungo mchezeshaji akizitumikia timu kadhaa ikiwamo Flamingo, SOS, Real Zanzibar, Black Sailors na Kilimani.
Awali, hakuwahi kufikiria kama ana kipaji cha kufundisha hadi alipopata mtu akamuuma sikio ndipo alipoamua kuacha kucheza mpira na kuwa kocha.
Safari ya kuwa kocha ilianzia kwenye timu ya Toyota na baada kutoka hapo alifundisha Kipago FC, New Generation, Chrisc Zanzibar, Kilimani City, Taifa Jang’ombe, Negro, Gulioni City, Raskazone, Jang’ombe Boys, Riverside, Zimamoto, Azam U20 na sasa Malindi.
Anasema amepitia mikononi mwa makocha wengi, lakini kwake Kocha Ali Shariff anabakia kuwa bora na anayemwamini.
CHANGAMOTO UKOCHA ZANZIBAR
Rijkaard anaeleza kuwa changamoto kubwa iliyopo kwa makocha zanzibar ni kwamba wengi hawapendi kusaidiana, lakinia hiyo anaiona ni fursa ya kujifunza.
Anasema kiuhalisia makocha wengi wa Zanzibar hawapendi kujituma katika mpira wa miguu ili kupata vitu vizuri na kuzungumzwa kwa mazuri wafanyayo.
“Kazi ya mpira inahitaji wasifu mzuri kwani huo ndio utakaokuvusha kutoka sehemu moja kwenda nyengine, fursa ya kufundisha ndani na nje ya Zanzibar. Kwa maana hiyo usipokuwa tayari kujituma huwezi kuyapata hayo.
“Nimejipanga kila timu ambayo nafundisha nifanye kazi kwa weledi kuwafanya mashabiki na wapenzi wangu kuona na kuvutiwa ninachokifanya. Nyuma yangu wapo wanaonitegemea kufanya vizuri nao wafaidike. Nisipofanya hivyo nitawaangusha,” anasema kocha huyo.
Kwa upande wa Zanzibar anataka kufundisha timu ambazo hazijawahi kufaidika naye, lakini Bara anatamani kufundisha timu yoyote na hilo litafanikiwa siku za usoni.
Anatoa wito kwa makocha vijana kutokata tamaa wala kurudishwa nyuma ikiwa wanataka kufikia malengo, akisema: “Wafanye vitu wanavyovipenda na wasipende kusikiliza maoni ya watu kuliko uamuzi wa nafsi zao kwa sababu malengo ni makubwa kuliko ya wanaowahitaji.
“Kitu cha kuzingatia ni kujituma, kujiamini na kutambua wanachopaswa kufanya kwa ajili ya kutengeneza falsafa bora za maisha yao.”
Ukizungumzia soka la vijana Zanzibar, hakika hutaacha kusikia jina lake likitajwa katika vinywa vya mashabiki wa mchezo huo kutokana na uzoefu wake wa kuwatoa vijana wengi wazuri ndani na nje.
Rijkaard amefanikiwa kufundisha timu mbalimbali Zanzibar zilizofanikiwa kutwaa mataji mengi katika ligi ya vijana.
Kwa masuala ya nje ya uwanja kocha huyo anasema ni mfanyabiashara na hivi karibuni atazindua programu ya wachezaji wa Zanzibar kupata tiba.
Kwa kipindi ambacho ligi imesimama Rijkaard anasema anapendelea zaidi kutembelea maeneo ya fukwe na hapendi kujihusisha na shughuli za mpira ili kuifanya akili yake ichangamane na mambo tofauti.
Kocha huyo anaenda mbali zaidi akisema kuwa kama asingekuwa mkufunzi wa soka kwa sasa angekuwa mfanyabiashara mkubwa.
MALINDI TAASISI YA VIPAJI
Safari ya Rijkaard hadi kufika kuifundisha Malindi anaamini kwamba ndoto zake zinakaribia kutimia kwani hiyo ni njia anayoitumia kuvuka kuyafuta mazuri zaidi na hapo alipo hajafika mwisho
Japokuwa timu hiyo anaitumia kama daraja kwake ili kufika mbali zaidi, bado anafurahia kufundisha na anajiona yupo sehemu salama kwa kuwa anapata ushirikiano mzuri kutoka kwa viongozi wa timu na wanaelewa wajibu wao.
Anasema timu hiyo inatoa nafasi kwa wachezaji wenye vipaji kuwaendeleza kimpira na itakuwa mfano ndani ya Zanzibar.