KIUNGO mshambuliaji wa Singida Black Stars, Marouf Tchakei, amesema wanatambua ugumu wanaoenda kukutana nao mbele ya CR Belouizdad ya Algeria katika mechi ya kwanza ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini amewataka mashabiki wasubiri waone kitakachotokea huko.
Tchakei alisema Singida imeenda Algeria ikiwa imara na lengo kuu ni kutaka kuanza mechi hizo za makundi wanayoshiriki kwa mara ya kwanza kwa kufanya vizuri na kuwatoa hofu mashabiki kwamba hawataamini kitakachotokea katika mechi hiyo ya Kundi C.
Singida watakuwa wageni wa CR Belouizdad Jumamosi kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, uliopo Baraki, jijini Algiers huku wakiwa na rekodi ya kushinda mechi tatu dhidi ya Flambeau du Centre na Rayon Sports kati ya nne za hatua ya awali ya michuano hiyo. Moja ilitoka sare na kufuzu makundi kwa mara ya kwanza.
Akizungumza na Mwanaspoti, Tchakei alisema wamefika makundi kwa juhudi na kuwekeza nguvu katika ushindani hivyo matarajio yao keshokutwa ni kuona wanafanya vizuri mechi hiyo ya kwanza ya makundi kabla ya kurudi kucheza nyumbani wiki ijayo.
“Benchi la ufundi, wachezaji na mashabiki wetu wanatambua ugumu wa mchezo huo, tunaendelea kujiweka imara ili kuhakikisha tunatengeneza mazingira mazuri ya kujiweka kwenye nafasi nzuri kusonga hatua inayofuata,” alisema Tchakei, raia ya Togo aliyeongeza;
“Kuna kazi kubwa inahitajika kufanyika kwa wachezaji wenzangu na benchi la ufundi linatambua nini tunatakiwa kukifanya ili kupata ushindi naamini hilo litafanikiwa kutokana na maelekezo ya kiufundi tunayoendelea kupata kutoka kwa kocha mzoefu ambaye pia ameshawahi kukutana na hiyo timu lakini pia kufundisha katika nchi tunayoenda kucheza.
“Malengo yetu ni kusonga hatua inayofuata na hilo naamini litawezekana kama wachezaji wenzangu tutacheza kiushindani, licha ya ugeni wetu kwenye michuano.”