CRDB yaorodhesha Sukuk ya Kiislamu soko la hisa Dar

Dar es Salaam. Benki ya CRDB imetangaza mafanikio ya kihistoria baada ya kuiorodhesha rasmi hatifungani yake inayofuata misingi ya Sharia ya Kiislamu, CRDB Al Barakah Sukuk, katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE). Hatifungani hiyo imevunja rekodi kwa kukusanya Sh125.4 bilioni sawa na asilimia 418 ya lengo, pamoja na Dola 32.3 milioni za Marekani (Sh78.16 bilioni) sawa na asilimia 646, hatua inayochochea ukuaji wa masoko ya mitaji nchini.

Akizungumza katika hafla ya kutangaza matokeo na kuorodheshwa kwa hatifungani hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk Elijah Mwandumbya ameipongeza CRDB kwa mafanikio hayo akisema ni msingi muhimu kwa maendeleo ya taifa.

“Utendaji huu wa kipekee wa Sukuk unaonyesha kukua kwa masoko ya mitaji nchini na shauku ya wawekezaji kwa bidhaa bunifu,” amesema.

Dk Mwandumbya amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji, ikiwamo kukamilisha sheria maalumu za kusimamia huduma za fedha zinazofuata misingi ya Kiislamu.

Amesema sheria hizo zitaimarisha ulinzi wa wawekezaji, kuongeza uwazi na kuiweka Tanzania katika nafasi ya ushindani katika huduma za fedha za Kiislamu barani Afrika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema matokeo ya mauzo ya hatifungani hiyo yamevuka matarajio katika sarafu zote mbili zilizoruhusiwa.

Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa zaidi ya wawekezaji 1,000 kutoka Tanzania na mataifa zaidi ya saba wameshiriki, wakiwamo watu binafsi, taasisi, makundi ya kidini na wawekezaji wa kimataifa.

“Kukusanya Sh125.4 bilioni na Dola 32.3 milioni si ushindi pekee kwa CRDB, bali ni kielelezo cha kuongezeka kwa imani kwa Tanzania,” amesema Nsekela.

Amesema zaidi ya Sh70 bilioni zilitoka kwa Watanzania binafsi, jambo linaloonyesha uelewa mpana wa masuala ya kifedha, huku zaidi ya Sh50 bilioni zikitoka kwa wawekezaji wa kimataifa, ishara ya kuvutiwa na soko la Tanzania.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Exaud Julius amesema mafanikio ya mauzo ya Sukuk hiyo, yamechangiwa na sera endelevu za kuboresha mazingira ya uwekezaji.

 Amesema hatua hiyo imeongeza imani ya wananchi kuwekeza katika hatifungani za kampuni na kuongeza thamani ya soko kutoka Sh13.5 trilioni hadi Sh13.7 trilioni.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa DSE, Peter Nalitolela amepongeza mafanikio hayo akisema kiwango kikubwa cha mauzo kinadhihirisha uimara wa mifumo ya udhibiti nchini.

“Kuorodheshwa kwa Sukuk kutaimarisha ukwasi na kuongeza ushiriki wa wawekezaji na kuiweka Tanzania kwenye ramani ya masoko ya fedha za Kiislamu kama Kuala Lumpur, Dubai, Riyadh na Manama,” amesema.

Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB, Profesa Neema Mori amesema matokeo hayo ni chachu ya kuendeleza ubunifu na utawala bora.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Sharia ya Al Barakah, Abdul Van Mohammed, akizungumza katika hafla hiyo, amesema mpango wa Serikali kuanzisha sheria maalumu za fedha za Kiislamu utafungua milango ya ushirikiano na masoko yenye ukwasi mkubwa, hasa kutoka nchi za Ghuba.

Tangu kuanzishwa mwaka 2021, CRDB Al Barakah imeendelea kukua kwa kasi ikiwa na zaidi ya wateja 400,000, amana za zaidi ya Sh350 bilioni na uwezeshaji wa Sh287 bilioni  katika miradi inayofuata misingi ya sharia.

Mafanikio haya yanaashiria mwanzo wa zama mpya za huduma za fedha za Kiislamu nchini.