Mavitu ya Mangalo yamkosha Mkenya

KOCHA wa Pamba Jiji, Mkenya Francis Baraza amesifu kiwango kinachoonyeshwa na beki wa kati wa kikosi hicho, Abdulmajid Mangalo tangu ajiunge na timu hiyo Agosti 7, 2025 licha ya kukaa nje ya uwanja kwa msimu mzima akiuguza majeraha yake.

Beki huyo amerejea tena baada ya kukaa nje ya uwanja kwa msimu mzima, kufuatia majeraha ya goti kipindi akiwa na Singida Fountain Gate, jambo linalomfanya Baraza kusifu kiwango alichokionyesha hadi sasa kikosini.

Akizungumza na Mwanaspoti, Baraza alisema Mangalo ni miongoni mwa wachezaji wazuri na wanaojua kujitunza kwa sababu si rahisi kukaa nje kwa muda mrefu bila ya kucheza mechi za ushindani, kisha ukarejea tena katika kiwango bora kwa haraka.

“Mchezaji aliyekaa nje kwa msimu mzima tena akiuguza majeraha ni lazima anaporejea aanze taratibu lakini kwa Mangalo ni tofauti sana, anavyocheza utafikiri msimu uliopita alikuwa na timu, hii inaonyesha amekomaa kiakili,” alisema Baraza.

Baraza alisema hata kama asingeingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza kwa haraka, hana shaka na uwezo wa beki huyo kwa sababu ameshafanya naye kazi kabla ya kuungana naye tena akiwa Pamba, hivyo, hajutii usajili wake.

Hii ni mara ya pili kwa Baraza kufanya kazi na Mangalo, kwa sababu wawili hao walikuwa pamoja Biashara United misimu minne iliyopita, ambapo beki huyo ndiye aliyekuwa nahodha mkuu wa ‘Wanajeshi wa Mpakani’, wanaoshiriki First League msimu huu.

Tangu Mangalo amejiunga na Pamba inayoshiriki Ligi Kuu kwa msimu wa pili sasa tangu ipande daraja msimu wa 2023-2024, ametengeneza pacha kali na beki, Brian Eshihanda aliyesajiliwa pia msimu huu akitokea Kakamega Homeboyz ya kwao Kenya.