BEKI wa kimataifa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Kelvin Yondani anayekipiga kwa sasa New King iliyopo Ligi Kuu ya Zanzibar (ZPL) amefichua sababu zilizomfanya aibukie huko kuwa ni kutaka kubadili mazingira kutokana na kushindwa kutoka nje ya nchi enzi zake akiwa katika ubora.
Nahodha huyo wa zamani wa Jangwani, aliyewahi pia kukipiga Polisi Tanzania na Geita Gold kabla ya msimu uliopita kuitumikia KenGold iliyoshuka daraja, tayari amecheza katika ligi za madaraja yote nchini na sasa yupo ZPL aliyoitaja kufurahishwa na mazingira yalivyo visiwani Zanzibar.
Akizungumza na Mwanaspoti, Yondani alisema amefanya kila kitu akiwa Ligi Kuu Bara ila hakupata bahati ya kutoka kwenda kucheza soka nje ya nchi akiwa katika ubora wake, hivyo amefanya uamuzi wa kucheza Zanzibar kabla ya kuamua kustaafu mpira.
“Soka ni mchezo wa wazi kila mmoja ameona kile nilichokifanya, bara nilipata ofa nyingi lakini machaguo yangu ni Zanzibar kwani ni sehemu ambayo nimecheza katika mashindano ya muda mfupi (Mapinduzi Cup na kadhalika) sasa nacheza kwa msimu mzima,” alisema Yondani na kuongeza;
“Nafurahia mazingira ya huku kuna vipaji vingi vikubwa ubora wa ligi yao hauendani na Bara sababu ni uwekezaji lakini wana vipaji vikubwa sana.”
Akizungumzia msimu wa kwanza ndani ya ligi hiyo alisema ni mapema sana kutaja ushindani ulivyo lakini ameshuhudia vipaji vikubwa na anaamini atakuwa na msimu mzuri.
“Nafurahia mazingira, ni mapema sana kuzungumzia ugumu lakini kuhusu utofauti kuna utofauti mkubwa. Bara kuna ushindani kwa sababu kuna uwekezaji mkubwa tofauti na huku, huku kuna vipaji vikubwa.”
Beki alianza kufahamika akiwa jijini Mwanza miaka ya mwanzoni mwa 2000 akiwa na Mwanza United kabla ya kusajiliwa na Simba 2006 aliyoichezea hadi 2012 na kuhamia Yanga alikokaa hadi mwaka 2020 kabla ya kutua Polisi Tanzania 2021 kisha kuzitumikia Geita Gold na Ken Gold.