Dar City yaizamisha Bravehearts ikitinga nusu fainali ‘road to BAL’

TIMU ya mpira wa kikapu ya Dar City kutoka Tanzania, inaendelea kufanya kweli katika mbio za kufuzu hatua ya nusu fainali, baada ya kupata ushindi wa pili mfululizo kwenye michuano ya Elite 16 Kanda ya Mashariki, ikiifunga Bravehearts ya Malawi kwa alama 93–75. Ushindi huu unaiweka karibu zaidi na nafasi ya kucheza Nusu Fainali katika safari yao ya BAL kwa mara ya kwanza.

Katika mechi ya leo Jumatano Novemba 19, 2025 iliyochezwa Uwanja wa Ndani wa Kasarani jijini Nairobi nchini Kenya, Nisre Zouzoua aliongoza mashambulizi kwa kufunga pointi 28, zikiwa nyingi kuliko mchezaji yeyote katika mechi hiyo na kuongeza rebound saba pamoja na kupokonya mipira mitatu, akipewa maksi 29 kwa kiwango chake. Wachezaji wengine watatu pia walifunga pointi za ‘double digits’, na kuifanya Dar City kupata ushindi wa pili bila kupoteza baada ya awali kuichapa Matero Magic 85-78.

Wakati Zouzoua akionyesha kiwango kikubwa, Solo Diabaté naye alifanya kweli kwa kutoa pasi za mwisho 14, huku mfungaji bora wa mechi, Deng Angok Yak Deng, akiweka pointi 17, moja zaidi ya Youssou Ndoye aliyeingia kutokea benchi. Raphael Putney aliongeza pointi 15.

Tofauti na mechi ya ufunguzi ambapo Dar City ilianza taratibu licha ya kushinda, safari hii kikosi hicho cha kocha Mamadou Gueye raia wa Ivory Coast kilianza kwa kasi, kikiongoza 10–4 mapema. Putney alifunga pointi 8 katika robo ya kwanza waliyoshinda 23–15.

Ndoye aliuwasha moto katika robo ya pili, huku Zouzoua aliyefunga pointi tano katika robo ya kwanza akifika pointi 10 ndani ya dakika za mwanzo za kipindi hicho na kuwapeleka Dar City hadi 32–20.

Mchezaji huyo wa kimataifa kutoka Ivory Coast, aliongeza pointi nyingine 10 kabla ya kipindi kumalizika na kufanya matokeo kuwa 46–30, ingawa Vincent Masiyano aliipunguzia Bravehearts kwa mkwaju wa mwisho wa pembeni uliofanya nusu ya mchezo kumalizika 46–33.

Bravehearts walishindwa kuhimili kasi ya timu hiyo kutoka Tanzania katika robo ya tatu. Kikosi cha Gueye kiliongeza presha zaidi, na Diabaté akiwafikisha Dar City kwenye alama 50.

Zouzoua alifunga tena kwa mbali kufanya matokeo yawe 53–34, tofauti kubwa zaidi hadi wakati huo. Mashuti manne zaidi ya nje ya mstari wa pointi tatu yaliimaliza kabisa Bravehearts, huku Dar City ikitawala robo hiyo kwa 32–10.

Katika robo ya mwisho, kocha Gueye aliwapa nafasi wachezaji wake wa akiba, jambo lililowapa ujasiri Wamalawi kucheza kwa nguvu na kushinda robo hiyo 32–15, lakini tayari mchezo ulikuwa umekwishaamuliwa.

“Tunafurahia ushindi huu wa pili mfululizo lakini bado tuna kazi ya kufanya ili kupata muunganiko mzuri zaidi uwanjani. Tumekuwa na mwanzo bora kuliko jana, tumetekeleza mipango kwa pamoja na kutumia nafasi zetu kujiweka mbele zaidi tulipoweza. Tutadumisha kasi hii kuelekea mchezo wa mwisho wa kundi, tukileta nguvu na moyo ule ule,” amesema Nisre Zouzoua wa Dar City.

Dar City ipo Nairobi nchini Kenya ikishiriki mashindano ya Elite 16 Kanda ya Mashariki ikiwa imepangwa Kundi B na timu za Bravehearts BC ya Malawi, Matero Magic (Zambia) na Ferroviario Da Beira (Msumbiji).

Kesho Alhamisi, Novemba 20, 2025, Dar City itakabiliana na Ferroviario da Beira majira ya saa 9:30 alasiri ikiwa ni mechi ya mwisho hatua ya makundi.