Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kuwa kitaisimamia kikamilifu Serikali ili kuhakikisha utekelezaji wa ilani na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, unakwenda sambamba na matarajio ya wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano, Novemba 19, 2025, jijini Dodoma, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Kenani Kihongosi, amesema ni wajibu wa Chama kuisimamia Serikali kwa kuwa ndicho kilichopewa dhamana ya kuomba kura, kuunda serikali na kuhakikisha ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni zinatimia.
Kihongosi amesema chama hakitasita kuchukua hatua kali dhidi ya kiongozi yeyote wa serikali, aliyechaguliwa au kuteuliwa, atakayebainika kufanya kazi kwa maslahi binafsi badala ya kutumikia wananchi. Amesisitiza kuwa mawaziri, manaibu waziri, pamoja na viongozi wengine waliopewa dhamana wanatakiwa kwenda kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na weledi.
Aidha, amewataka viongozi katika ngazi za mikoa, wilaya, halmashauri na kada nyingine za utendaji kufanya kazi kwa kasi na ufanisi ili kuhakikisha matarajio ya Rais Samia yanatekelezwa kama ilivyoainishwa. Ameonya kuwa chama hakitavumilia viongozi wanaoonyesha uzembe, uvivu au rushwa, akibainisha kuwa hatua zitachukuliwa mara moja dhidi ya watakaokiuka maadili ya utumishi wa umma.
Akifafanua zaidi, Kihongosi amesema CCM itaanzisha mfumo wa vipimo vya utendaji kazi kwa viongozi wa serikali. Amesema utendaji wao utachekechwa kulingana na vigezo ambavyo chama kitaweka, na kwamba kiongozi atakayeshindwa kufikia viwango hivyo atachukuliwa hatua bila kusubiri muda mrefu. Kwa upande mwingine, viongozi watakaofanya kazi kwa ufanisi na matokeo mazuri watapewa ulinzi na kuungwa mkono na chama.
