Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amewateua waliowahi kuwa Wakurugenzi watendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) Bakari Machumu na Tido Mhando kwenye ofisi yake ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu.
Uteuzi huo uliofanyika leo Jumatano, Novemba 19, 2025, umemtaja Bakari Machumu ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, akichukua nafasi ya Sharifa Nyanga ambaye atapangiwa majukumu mengine.
Rais pia amemteua Tido ambaye ni mwanahabari mkongwe nchini, kuwa Mshauri wa Rais, Habari na Mawasiliano.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka imeeleza kuwa Rais Samia amemteua pia Lazaro Nyalandu kuwa Balozi.
Nyalandu ambaye aliwahi kuhudumu kwenye nafasi ya uwaziri katika Serikali ya awamu ya nne iliyokuwa ikiongozwa na Rais Jakaya Kikwete na wizara yake ya mwisho kuhudumu ilikuwa ya maliasili na utalii.
Pia amewahi kuwa mmoja wa washauri wa aliyekuwa mke wa Rais wa awamu ya tatu, Mama Anna Mkapa katika uendeshaji wa Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF).
Kwa upande wa Machumu na Tido wote kwa nyakati tofauti, wamewahi kufanya kazi MCL wakihudumu katika wadhifa wa ukurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo.
Tido amehudumu kwenye nafasi hiyo ya Ukurugenzi Mtendaji kuanzia mwaka 2011 mpaka 2013 huku Machumu akihudumu kuanzia 2021 mpaka alipostaafu 2024.
Itakumbukwa kuwa Machumu aliitumikia MCL kwa miaka 17 kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa huo, akimrithi Francis Nanai.
Mbali na hilo, wawili hao wote ni wajumbe wa kamati ya watu tisa wanaofanya kazi ya kutathimini hali ya uchumi katika vyombo vya habari nchini. Kamati hiyo inaongozwa na Tido.
Akizungumzia uteuzi huo alipozungumza kwa simu leo, mwanahabari mkongwe nchini, Absalom Kibanda amesema kwa mara ya kwanza, Rais Samia amefanya uteuzi mzuri kwenye ofisi yake ya Mawasiliano Ikulu kwa kuwaweka watu ambao wanaifahamu tasnia ya habari kwa undani zaidi
“Kuanzia kwenye uteuzi wa masuala ya habari na mkurugenzi wa mawasiliano, wote hawa ni wazoefu. Kwa uzoefu wa kitaifa na kimataifa kwa Tido Mhando, atakuwa mshauri sahihi wa Rais Samia na atamuongoza vizuri Machumu.
“Hawa ni watu ambao kwa pamoja wamewahi kufanya kazi Mwananchi, lakini si hilo tu, bali wamekuwa wote kwa muda mrefu katika tasnia ya habari. Sekta ya habari ya Ikulu imepata timu sahihi, kulikuwa na kupwaya kidogo kwenye mawasiliano kwa umma, Rais ameamua kuongeza nguvu,”amesema Kibanda.
Mwanahabari mkongwe, pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).
Machumu amekuwa MCL, kuanzia mwaka 2004 akianzia nafasi ya Mhariri wa Biashara katika Gazeti la The Citizen kwa miaka miwili baadaye akateuliwa kuwa Mhariri Mtendaji wa gazeti hilo.
Mwaka 2012, Machumu aliteuliwa kuwa Mhariri Mtendaji Mkuu wa MCL akisimamia magazeti yanayochapishwa na kampuni hiyo ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti pamoja na majukwaa ya mtandaoni.
Kabla ya kujiunga na MCL mwaka 2004, Machumu alifanya kazi na Kampuni ya Business Times Ltd iliyokuwa inachapisha magazeti ya Majira, Business Times, Daily Times na Dar Leo kwa miaka sita na katika kipindi hicho, alikuwa mwandishi wa habari za biashara na mhariri wa makala.
Lakini pia aliwahi kuwa Mhariri wa Habari wa gazeti la Daily Times. Kitaaluma, Machumu ana Shahada ya Kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), alikohitimu mwaka 1998.
Miaka 20 baadaye, alihitimu shahada ya uzamili katika usimamizi wa biashara (MBA) kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Uongozi ya chuo cha Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika (Esami).
Pia, Machumu amesomea shahada ya uzamili katika uongozi wa vyombo vya habari na ubunifu katika Chuo Kikuu cha Aga Khan, Nairobi nchini Kenya.
Kuhusu Tido ni mwanahabari mkongwe aliyewahi kufanya kazi na Shirika la Utangazaji la BBC, London Idhaa ya Kiswahili.
Pia amewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), kabla ya kuhamia MCL.
Pia, Tido amewahi kuwa Naibu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam, baadaye Mtendaji Mkuu Azam Media Group, sambamba na hilo, mwanahabari huyo ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB).
