…………..
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limempongeza Bakari Steven Machumu kwa kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu.
Machumu ambaye hadi uteuzi wake alikuwa Makamu Mwenyekiti wa TEF ni mchapa kazi, anajituma, ana ujuzi, uzoefu na weledi wa hali ya juu katika tasnia ya habari.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Deodatus Balile kupitia taarifa yake leo amesema TEF inaamini kuteuliwa kwake atakuwa kiungo mzuri kati ya Ikulu na sekta ya habari nchini.
“TEF inampongeza pia Tido Mhando, kwa kuteuliwa kuwa Mshauri wa Rais, Habari na Mawasiliano, ambaye ni mwanahabari mkongwe na mwenye ujuzi mkubwa unaohitajika katika nyakati zenye changamoto kuu ya mawasiliano duniani kwa sasa. Tumaamini kwa uzoefu wa wawili hawa, tutashuhudia mabadiliko makubwa ya kufikisha habari za serikali kwa wananchi.”
Tunawatakia kila la heri katika majukumu yao mapya. Mungu ibariki Tanzania.
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
Deodatus Balile
Mwenyekiti
Novemba 19, 2025