Fiston Mayele ametawazwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa Klabu za Wanaume katika Tuzo za CAF 2025, akihitimisha msimu wake bora zaidi uliomfanya mshambuliaji huyo wa DR Congo kuwa mmoja wa wachezaji wasiozuilika kirahisi barani Afrika.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa DR Congo ametoa mchango wa hali ya juu kwa klabu ya Pyramids iliyotwaa mataji matatu makubwa ambayo ni Ligi ya Mabingwa Afrika, CAF Super Cup na Kombe la FIFA la African-Asian-Pacific.
Mayele amekabidhiwa tuzo hiyo kwenye hafla iliyofanyika leo Jumatano Novemba 19, 2025 katika Chuo Kikuu cha Mohammed VI Polytechnic (UM6P) kilichopo Rabat nchini Morocco.
Mbali na mchango wake wa kubeba mataji hayo, nyota huyo amemaliza msimu wa 2024-2025 akiwa mfungaji kinara kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika akifunga mabao sita yaliyokuwa na mchango mkubwa katika kuiwezesha Pyramids kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza katika historia yao.
Pia Mayele alifunga mabao matatu yaliyoiwezesha Pyramids kutwaa ubingwa wa Kombe la FIFA la African-Asian-Pacific katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Al Ahli ya Saudi Arabia, Septemba 25, 2025.
Oktoba 18, 2025, akafunga bao pekee katika ushindi wa 1-0 ilioupata Pyramids mbele ya RS Berkane na kubeba taji la CAF Super Cup.
Mayele amemshinda mchezaji mwenzake wa Pyramids, Mohamed Chibi raia wa Morocco ambaye ni beki wa kulia. Mwingine ni mshambuliaji wa RS Berkane na timu ya taifa ya Morocco, Oussama Lamlioui ambaye alifunga mabao matano yaliyoisaidia RS Berkane kutwaa Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2024-2025. Pia alikuwa na mchango wa kuisaidia RS Berkane kushinda taji lao la kwanza la Botola Pro 2024-2025.
Katika hatua nyingine, Lamlioui aliiwezesha Morocco kutwaa taji la CHAN 2024, akiibuka pia mfungaji bora wa mashindano hayo akipachika mabao sita.