Maiga azindua mahema ya kuboresha biashara kwa vijana na wanawake mpaka wa Mutukula.

Na Mwandishi Wetu

Mkuu wa Wilaya ya Misenyi Hamisi Mayamba Maiga, amezindua rasmi mahema maalumu ya kuboresha mazingira ya biashara kwa vijana na wanawake katika mpaka wa Mutukula, mkoani Kagera. Mradi huo unatekelezwa na TCCIA kwa ushirikiano na AGRA, ukiwa na lengo la kukuza biashara za mpakani na kuongeza usalama wa shughuli za kiuchumi.

‎Uzinduzi huo ni mwendelezo wa utekelezaji wa mradi unaoendelea katika mikoa mbalimbali nchini, ambapo tayari umefanyika Kigoma na sasa umefika Kagera.

‎Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhe. Maiga aliipongeza TCCIA na AGRA kwa juhudi za kuwawezesha wafanyabiashara wadogo, hususan vijana wanaojishughulisha na biashara za mazao, mboga mboga na matunda katika maeneo ya mipakani.

‎“Kwanza nitoe pongezi sana kwa TCCIA na AGRA kwa kuandaa mradi huu na kuutekeleza kwa viwango. Hii ni fursa kubwa kwa vijana wetu, hasa hawa wa mpakani,” alisema.

‎“Serikali inaunga mkono jitihada hizi; endeleeni kuzifikisha katika mipaka yote nchini.”

‎Aidha, aliwataka vijana na wafanyabiashara kutumia mahema hayo kama jukwaa muhimu la kupata taarifa za masoko, kuripoti changamoto zisizo za kikodi, na kuongeza ufanisi wa biashara zao.‎

‎“Tumieni platform hii kutafuta taarifa, kutangaza bidhaa na kuripoti vitendo kandamizi ili mfanye biashara vizuri na mchangie ukuaji wa uchumi wetu,” aliongeza.

‎Uzinduzi huo uliambatana na mafunzo ya Whistle Blowing kwa wafanyabiashara wa Mutukula, yaliyolenga kupambana na vizuizi visivyo vya kikodi (NTBs), kuripoti changamoto kwa njia za kidigitali, kuboresha ubora wa bidhaa na kutumia mitandao ya kijamii kupanua masoko.

‎Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa TCCIA Kagera, Bw. Rwechungura Mali, alisema chemba hiyo itaendelea kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati kupitia mafunzo na kuwaunganisha na mitandao ya kibiashara. Aliwahimiza wafanyabiashara kujiunga na TCCIA ili kufungua fursa zaidi za ukuaji.‎

‎Mradi huo unatarajiwa kuongeza ufanisi wa biashara mpakani, kuimarisha usalama wa bidhaa, kupunguza rushwa na gharama za uendeshaji, pamoja na kukuza uchumi wa vijana na wanawake. Utekelezaji wake katika mikoa ya Kigoma na Kagera tayari umeanza kuleta matokeo chanya.