SIMBA inaendelea kujifua kwa sasa ikijiandaa kwa pambano la kwanza la Kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro Atletico ya Angola, lakini kuna jambo linafanywa kwa kipa wa timu hiyo, Yakoub Suleiman, kuhakikisha anakuwa bora zaidi ili awabebe wekundu.
Kazi hiyo ya kumweka sawa kipa huyo namba moja wa Simba na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inafanywa na kaka yake, aitwaye Mohamed Seif Belo, ikiwa ni siku chache tangu Yakoub ageuke gumzo kutokana na kipigo cha Stars cha mabao 4-3 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Kuwait.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Novemba 15, 2025 jijini Cairo, Misri, Yakoub aliruhusu mabao yaliyoonekana kama ya uzembe binafsi na wa mabeki wa Stars na kushambuliwa mtandaoni, kitu kilichomfanya kaka mtu kuamua kuingilia kati na kufichua alivyoanza kumpa mbinu za kumbeba.
Belo ambaye kitaaluma ni kipa, ameiambia Mwanaspoti, tatizo kubwa la mdogo wake ni kushindwa kuitumia miguu (footwork) kwa ufanisi na ameshazungumza naye ili kulifanyia kazi mazoezini kumfanya aweze kuokoa mpira kwa miguu, kwani maeneo mengine yupo freshi.
Kabla majeraha hayajamstaafisha kucheza soka, Belo alikuwa anacheza nafasi ya kipa katika timu mbalimbali ikiwamo Polisi Tanzania ilipokuwa Ligi Kuu kabla ya kushuka daraja na sasa inashiriki Ligi ya Championship.
Belo amesema ana uelewa na nafasi hiyo ndiyo maana alibaini upungufu, hivyo Yakoub kuna vitu baadhi anatakiwa kuvifanyia kazi.
Amesema alikuwa anaifuatilia mechi ya kirafiki ya kimataifa ya Stars dhidi ya Kuwait na kupoteza kwa mabao 4-3 ambayo Yakoub alisimama langoni, hivyo akaona ni kitu gani anapaswa kukifanyia kazi na yupo tayari kumsaidia.
“Kwanza baada ya mechi nilimpigia simu na kumuuliza kwa nini anashindwa kucheza kwa kutumia miguu, alinijibu alipokuwa mapumziko hakufanyia mazoezi ya kutosha kuhusiana na hilo, nikamwambia akirudi awamu hii ahakikishe anafanya mazoezi ya ndani ya uwanja,” amesema Belo na kuongeza;
“Jambo lingine la msingi nililomwambia kuhusiana na kinachoendelea katika mitandao ya kijamii, anapaswa kuwa na mtazamo wenye nguvu wa kujiboresha zaidi ili kiwango chake kiwe na mabadiliko uwanjani na siyo kitu kingine.
“Presha ya Simba na JKT Tanzania ni vitu viwili tofauti, kila kitu atakachokifanya kitatazamwa kwa ukubwa lazima ajue jinsi ya kukabiliana na kila kitu.”
Belo aliyewahi kuzichezea timu za Amani Fresh, Sharp Boys, Polisi Zanzibar, timu ya Taifa ya Zanzibar ya watoto kuanzia umri wa miaka sita na Polisi Tanzania, amesema kila anachokifanya mdogo wake anakifuatilia ili kumjenga awe bora zaidi.
Katika hatua nyingine, Yakoub ametegua mtego wa kwanza kati ya miwili anayotakiwa aikwepe katika kipindi ambacho mwenzake, Moussa Camara akiwa anajiuguza baada ya kufanyiwa upasuaji huko Morocco.
Mtego ambao Yakoub ameushinda hivi sasa, ni wa adhabu ya kukosa mechi kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya kujilinda kutopata mjumuisho wa kadi za njano katika mechi mbili zilizopita ambao zingemuweka katika hatari ya kukosa mchezo mmoja kati ya miwili ya hatua ya makundi ambayo Simba itacheza katika kipindi ambacho Camara atakuwa nje ya uwanja.
Katika mechi mbili zilizopita dhidi ya Nsingizini Hotspurs ambazo Yakoub alicheza, kipa huyo alimaliza bila kuonyeshwa kadi ya njano, jambo linalompa uhakika wa kucheza mechi mbili zijazo dhidi ya Petro Luanda na Stade Malien.
Kwa mujibu wa kanuni ya 5(i) ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, mchezaji atakosa mchezo unaofuata baada ya kutimiza kadi tatu za njano.
“Mchezaji anayefikisha kadi ya njano ya tatu, atasimamishwa moja kwa moja kucheza katika mechi inayofuata ya mashindano ya Klabu ya CAF. Sekretarieti inapaswa kuwasiliana na Chama husika juu ya kusimamishwa huko,” inafafanua kanuni hiyo.
Kama Yakoub angeonyeshwa kadi za njano mbili katika mechi hizo za nyuma, maana yake kadi ya njano katika mechi inayofuata dhidi ya Petro Atletico ingemkosesha mechi dhidi ya Stade Malien na hivyo ingeifanya Simba kubaki na kipa mmoja tu mwenye angalau uzoefu ambaye ni Hussein Abel.
Ukiondoa hilo, Simba na Yakoub mwenyewe wanapaswa kuombea kipa huyo aruke kiunzi cha majeraha ili mzigo wa kulinda lango la timu hiyo usibakie kwa Abel pekee ambaye amekuwa hatumiki kikosini kwa muda mrefu.
Kipa wa zamani wa Simba, Idd Pazi ‘Father’ amesema anaamini Yakoub atalilinda vyema lango la Simba katika mechi atakazosimama langoni kipindi ambacho Camara hatakuwapo.
“Ni kipa mzuri watu wawe na imani naye tu. Hizi timu kubwa zina presha, lakini ndani ya muda mfupi anaonekana ameweza kukabiliana nayo. Watu hawapaswi kuwa na wasiwasi naye na naamini atafanya vizuri tu,” amesema Pazi.
Nyota wa zamani wa Simba, Dua Said amesema; “Michuano mikubwa anayokwenda kucheza isimfanye apate presha, anatakiwa acheze kama anavyocheza mechi za kawaida, hapo ataona matokeo. Yakoub anatakiwa acheze kwa kujiamini, akiwaza kwamba yuko pekee yake anaweza kujihurumia na kujikuta anaruhusu mabao kizembe.
“Simba iko mikononi mwake hivyo mashabiki tunaamini kwenye uwezo wake ambao unatakiwa kudhihirika katika michuano hiyo.”
Mchambuzi wa Soka na kiungo wa zamani wa Yanga na Simba, Amri Kiemba amesema Yakoub anatakiwa kujiamini na kuhakikisha anaifanikisha timu hatua ya makundi, kwani yeye ndiye tegemeo.
