Tanzania kuwa lango kuu la kuzifikia nchi nyingine za Afrika ya Mashariki na kusini mwa Afrika ndiyo moja ya malengo ya Serikali ya awamu ya sita katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Jambo hili linaweka ulazima wa kuwekeza kwenye miundombinu ya usafiri na usafirishaji ili kuweza kuzihudumia vyema nchi jirani ambazo hazikupata bahati ya kuwa na milango ya kuingia na kutoka kwa njia ya bahari.
Haya yamewekwa bayana na Rais Samia Suluhu Hassan wakati akifungua Bunge la 13 katika awamu ya pili ya uongozi wake tangu alipochaguliwa Oktoba 29, 2025 kuongoza nchi kwa kipindi kingine.
Akihutubia kwa mara ya kwanza tangu kuapishwa kushika nafasi hiyo kwa muhula wa pili, Rais Samia alisema hiyo itasaidia nchi kuweza kunufaika na fursa ya kijiografia iliyonayo na kukuza uchumi wa taifa.
“Ni kwa msingi huo, tunaendeleza uwekezaji kwenye ujenzi wa reli ya kisasa ya (SGR) ya ushoroba wa kati kwa kukamilisha vipande vilivyosalia, yaani Makutupora-Tabora; Tabora-Isaka; Isaka-Mwanza; na Tabora-Kigoma, na vilevile, kipande kinachoenda Burundi cha Uvinza-Musongati. Tutakuja na mkakati wa kuhakikisha reli inatengeneza ushoroba wa uchumi, biashara na uwekezaji,” anasema.
Pia ameweka bayana kuwa kama nchi inajipanga kujenga reli ya SGR kutoka Tanga hadi Musoma na kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay (Ruvuma) inayofika pia Mchuchuma na Liganga sambamba na kusimamia maboresho ya reli zilizopo ikiwamo reli ya Tanzania – Zambia.
“Ninafurahi kuwataarifu kuwa hivi karibuni kutafanyika hafla ya kuweka jiwe la msingi la Mradi wa Ukarabati wa Reli ya TAZARA itakayofanyika nchini Zambia. Pia kwa reli ya zamani ya Meter Gauge (MGR) tutafanya ukarabati wa vipande vya Tabora – Kigoma, Kaliua – Mpanda; Tanga – Arusha; Ruvu – Mruazi; ili nayo itumike kuchochea uchumi,” anasema.
Suala hili halijaicha mbali sekta binafsi kwani watasimamia ujio wa waendeshaji binafsi kwenye reli zinazojengwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC).
Anasema kwa kuanzia tutakuwa na mwendeshaji binafsi kwenye reli ya Tazara, hatua hii itazidi kupunguza gharama za usafirishaji kwa wafanyabiashara.
Wakati foleni ikiwa ni moja ya jambo linalochukua muda mwingi wa kazi kwa wakazi wa kwenye majiji, Serikali imeweka bayana kusudi lake la kujenga treni za mijini za kisasa katika miji ya Dar es Salaam na Dodoma ili kuboresha usafiri kwenye majiji haya yanayokua kwa kasi.
Hili linafanyika wakati ambao Dar es Salaam inatarajiwa kuwa na wakazi milioni 10 ifikapo mwaka 2030, hivyo kurahisisha njia za usafiri ni kurahisisha shughuli za kiuchumi.
Katika upande wa uchukuzi anasema mwelekeo wa kisera ni kujenga Mfumo Fungamanishi, ambao utahakikisha kuwa bandari viwanja vyote vya ndege na vituo vya reli vina muunganiko wa usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo kwa njia mbalimbali.
Hili linafanyika wakati ambao takwimu zinaonyesha kuwa maboresho ya miundo mbinu na mifumo ya uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam yaliyofanyika yamefanya gharama za uendeshaji wa bandari zimepungua ambapo zaidi ya Sh258 bilioni kwa mwaka zimeokolewa.
“Kuelekea mwaka 2030, tutasimamia maboresho zaidi kwenye bandari zetu nchini. Tutaongeza gati 10 kwenye Bandari ya Dar es Salaam ambayo kwa sasa ina Gati 12. Tutakamilisha kuunganisha reli ya SGR na bandari ili mizigo isafirishwe kwa reli hadi Bandari Kavu ya Kwala ambapo magari ya mizigo (malori) yatafanya kazi ya usafirishaji kuanzia hapo,” anasema.
Pia bandari za Bahari ya Hindi ikiwamo Tanga ambayo itaunganishwa kwa reli na Bandari ya Musoma kule Mara zitaboreshwa sambamba na kufanya upanuzi na maboresho kwenye Bandari ya Mtwara ambayo inakusudiwa kuunganishwa kwa reli na bandari inayojengwa Mbambabay kule Nyasa, Ruvuma.
Kadhalika bandari mpya itakayojengwa Bagamoyo itaunganishwa na Bandari kavu ya Kwala.
Serikali pia inakusudia kuendeleza bandari za maziwa makuu za Mwanza, Kigoma na Kalema kule Tanganyika na tutakamilisha ukarabati na ujenzi wa meli za abiria na mizigo zitakazotoa huduma kupitia bandari hizo ikiwemo MV Mwanza ambayo imeshaanza kutoa huduma za usafirishaji kule Kanda ya Ziwa.
“Tutakamilisha upatikanaji wa meli kubwa itakayotoa huduma katika Bahari ya Hindi. Kwa upande wa usafiri wa anga, pamoja na mambo mengine, tumepanga kuwa ifikapo mwaka 2030 tuliimarishe zaidi Shirika letu la Ndege la Tanzania kwa kuongeza ndege mpya 8 kuliwezesha shirika kuongeza miruko ndani na nje ya nchi,” anasema Samia.
“Mwelekeo wetu ni kufungua nchi pamoja na kukifanya kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere kuwa kiungo (hub) cha safari za ndege kimataifa.
Akizungumzia suala hilo, mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Abel Kinyondo anasema miundombinu ni kitu muhimu kwani kinaweza kuchochea uchumi kwa kuwezesha kusafirisha bidhaa, mali na watu kutoka sehemu moja hadi nyingine.
Alitolea mfano wa mkulima wa nyanya aliye Kibondo asiyekuwa na mfumo wa utunzaji bidhaa zake ambazo akikaa nazo kwa siku nne zinaweza kuoza lakini ikiwepo treni ya kisasa anaweza kufikia masoko ambayo yana bei nzuri badala ya kuuza shambani kwake kwa bei ya hasara na badala yake anafuata soko kubwa kama Kariakoo na akapata bei kubwa anayopata mtu wa kati.
“Suala hili lina uwezo wa kunyanyua watu kutoka katika kiwango cha uchumi walichokuwapo hata hivyo mtandao huu unapaswa kuunganishwa na maboresho mengine kama mazingira ya uwekezaji ikiwemo viwanda ili mtu anayeuza nyanya badala ya kwenda moja kwa moja jikoni iongezewe thamani,” anasema Profesa Kinyondo.
Hii itafanya kuongeza tija kwenye kilimo kwa sababu itasaidia si kufikia soko la Kariakoo bali pia katika nchi jirani kwa sababu soko limepanuka.
“Hii itafanya bidhaa zisindikwe nyingi zaidi na ili uzalishaji uongezeke lazima mbolea ipatikane, tozo zipungue kwa sekta zote hivyo nini kifanyike tuangalie uwekezaji ikiwemo kwenye nishati kwani viwanda vinahitaji viwango vya uhakika maji ya uhakika ukitaka faida kubwa isizungumzwe tu miundombinu kwani inaweza kufanya Mkenya auze bidhaa za viwanda kwako kuliko wewe,” anasema.
Kama nchi inataka faida ya kweli ni vyema kuangalia uchumi unajengwaje ili kuhakikisha faida za miundombinu hii zinawanufaisha watanzania badala ya kufanya watu wasiwe na uwezo wa kununua zaidi kutoka nchi Jirani.
“Ni vyema kuangalia ni kitu gani ambacho tunaweza kufanya huku ili kusaidia vijana wetu kupata ajira, watu kufanya uzalishaji,” anasema.
Katika hilo Dk Lutengano Mwinuka kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) anasema miundombinu ni muhimu katika ukuaji wa uchumi kwani bidhaa zitaweza kusafirishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine jambo litakalochochea ukuaji wa uchumi wa watu kupitia kufungua fursa mbalimbali kama kilimo, viwanda na utalii.
“Hivyo lazima tuendelee kuunganisha miji kwani miundombinu ni uwezeshaji lakini kuwekeza katika maeneo mengine hakukwepeki ikiwamo kugusa wakulima, kuwekeza katika masoko, maghala, viwanda kwa ajili ya kuongeza thamani ya bidhaa za kilimo na kuongeza thamani kwa wananchi,” anasema na kuongeza kuwa ni vyema kuhakikisha sekta nyingi zinaguswa ili kufungamanisha uwekezaji huo.
Mtaalamu wa Uchumi, Oscar Mkude anasema uwekezaji huu ni mwelekeo wa kimkakati na kama ikitekelezwa itasaidia na kurahisisha uchukuzi na biashara.
Anasema suala hilo linapaswa kwenda sambamba na uwepo wa mizigo ili kuweza kupata matokeo katika uwekezaji uliofanyika huku akitaka sekta mbalimbali kuwezeshwa kama ambavyo vipaumbele vya Chama cha Mapinduzi (CCM) vilivyotajwa.
Alitolea mfano wa sekta ya kilimo ambavyo watanzania wengi wamejiajiri akisema katika mwaka mzima wanafanya kazi kwa miezi mitatu au minne pekee jambo ambalo si zuri kwa sababu wanalima kwa kutegemea mvua hali inayofanya wasifanikiwe kwa kiasi kikubwa.
Jambo hilo ndiyo huwafanya kutafuta shughuli nyingine ya kujiingizia kipato ikiwemo kuchoma mkaa huku akisema uwekezaji katika kilimo cha umwagiliaji inaweza kukomesha jambo hilo ili kuhakikisha wanakuwa na shughuli za kufanya miezi yote.
“Mimi ningependa kuona namna gani tunamzungumzia mkulima si kwa wale walio karibu tu na skimu za umwagiliaji bali wote hata walio mbali na skimu kwa sababu tunazungumzia kuongeza tija kwenye kilimo na kuwa mwekezaji hivyo ni vyema kuhakikisha wanatumia siku zote za mwaka vizuri katika shughuli zake za kila siku,” anasema.
