Mume adaiwa kumuua mkewe naye ajiua kwa sumu Geita

Geita. Mwanamke aliyefahamika kwa jina la Maria Salvatory mkazi wa Kitongoji cha Bugoma,Kijiji cha Kilombero,Kata ya Lwamgasa Wilaya ya Geita amefariki baada ya kudaiwa  kushambuliwa na mumewe Mayala Juma, kwa kitu butu kichwani na kuchomwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa katika mitandao ya Jeshi la Polisi jana Jumatano Novemba 19,2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita,Safia Jongo,imeelezwa kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 17,2025 saa 1:00 asubuhi ambapo baada ya Mayala kumuuwa mkewe, naye alijifungia ndani na kunywa sumu.

‘’Baada ya kufanya mauaji,Mayala Juma alijifungia chumbani na kunywa sumu aina ya synom crown pamoja na dawa nyingine katika jaribio la kujiua.Aliwahishwa Hospitali ya Wilaya ya Geita ili kuokoa maisha yake lakini alfajiri ya Novemba 18,2025 alifariki dunia.’’ imeeleza taarifa hiyo.

Katika taarifa hiyo imeelezwa kuwa,chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi,baada ya mume kumtuhumu mkewe kuwa na uhusiano na wanaume wengine.Miili ya marehemu imefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa ndugu kwa taratibu za mazishi.