Chippo akomalia nidhamu Mtibwa Sugar

BAADA ya uongozi wa Mtibwa Sugar kumtambulisha Mkenya Yusuf Chippo kwa ajili ya kukiongoza kikosi hicho kwa msimu huu wa 2025-2026, kocha huyo amekutana na kuzungumza na wachezaji wote wa timu hiyo, huku akiwataka kuzingatia zaidi nidhamu.

Chippo aliyeachana na Murang’a SEAL ya kwao Kenya tangu Agosti 21, 2025, amejiunga na timu hiyo kwa ajili ya kuiongoza kwa msimu huu, akishirikiana na Awadh Juma ‘Maniche’ aliyeipandisha daraja kwenda Ligi Kuu, ambaye amekuwa msaidizi wake.

Akizungumza na Mwanaspoti, Chippo amesema amefurahia mapokezi makubwa na mazuri aliyoyapata baada ya kukutana na uongozi na wachezaji wa kikosi hicho kizima, huku miongoni mwa mambo waliyozungumza aliwataka kuheshimiana wenyewe kwa wenyewe.

CHIP 01

“Baada ya kukutana nao na kuzungumza nao niliwasihi tufanye kazi kwa nidhamu, kila mmoja amuheshimu mwenzake bila kujali umri na uzoefu alionao, kwa sababu ili tufanikiwe sote ni lazima tuzingatie hilo kwa mustakabali wetu,” amesema Chippo.

Kocha huyo amesema mbali na kuzungumza na wachezaji ila aliushukuru uongozi wa timu hiyo kwa kumwamini na kumpa nafasi hiyo muhimu ya kukiongoza kikosi hicho na miongoni mwa mambo waliyojadiliana ni pamoja na usajili wa dirisha dogo.

“Tumezungumza mambo mengi hususan kuboresha kikosi katika dirisha dogo lijalo, hilo lote tutaliangalia kwa kina muda mwafaka ukifika, japo kwa sasa tunapambana kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye mechi zetu zijazo,” amesema Chippo.

CHIP 02

Kwa msimu wa 2025-2026, Maniche aliiongoza Mtibwa katika mechi tano za mwanzo za Ligi Kuu na kati ya hizo alishinda moja tu, akitoa sare miwili na kupoteza pia miwili, ikishika nafasi ya 13, baada ya kukusanya jumla ya pointi zake tano.

Chippo anakumbukwa na mashabiki wengi hasa baada ya kukiongoza kikosi cha Ulinzi Stars kutwaa mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu ya Kenya ‘KPL’ kati ya 2003 na 2005 na kuhudumu akiwa kocha msaidizi wa Harambee Stars kuanzia 2008 hadi 2011.

Kibarua cha kwanza kwa Chippo aliyezifundisha pia timu mbalimbali za Tanzania zikiwemo za Pamba Jiji, Coastal Union na TRA United zamani Tabora United, kitakuwa dhidi ya KMC, mechi itayopigwa Uwanja wa KMC Complex, Novemba 25, 2025.