Mchechu: Ushirikiano wa serikali na TPC umezaa matunda, wachangia zaidi ya Sh75 bilioni kwenye mapato

Moshi. Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu amesema mafanikio yaliyopatikana ndani ya miaka 25 tangu ubinafsishaji wa TPC Limited yametokana na ushirikiano thabiti kati ya serikali na sekta binafsi, hatua iliyolibadilisha shirika hilo kutoka kiwanda kilichokuwa kinafifia hadi kuwa mmoja wa wazalishaji bora wa sukari barani Afrika.

Kwa sasa, TPC inatoa gawio la Sh16.5 bilioni kwa Serikali, huku mchango wake wa jumla katika mapato ya Serikali ukifikia zaidi ya Sh75 bilioni.

Mbali na mapato, uzalishaji wa sukari umeongezeka kutoka tani 36,000 zilizokuwa zinazalisha mwaka 2000 na kufikia Tani 120,000 kwa sasa.

Akizungumza jana usiku, Novemba 19, katika maadhimisho ya miaka 25 ya ushirikiano huo, ambayo yalitanguliwa na uwekaji wa jiwe la msingi la mradi mpya wa kimkakati wa kiwanda cha kuchakata molases (TPC Distillery) chenye thamani ya Sh130 bilioni, Mchechu amesema uamuzi wa Serikali kuuza asilimia 75 ya hisa za TPC kwa sekta binafsi mwaka 1999 ulikuwa hatua muhimu ya kuanzisha mageuzi ya kiutendaji na kiuchumi.

Mchechu amesema TPC imekuwa mfano bora wa mafanikio ya ubia baina ya sekta ya umma na binafsi, ikiwamo kulipa gawio la kila mwaka ambapo Mwaka 2023 pekee, Serikali ilipokea Sh16.5 bilioni kama gawio.

“Uwekezaji huu umetupa maslahi makubwa. Mbali na gawio la Sh16.5 bilioni, TPC inachangia zaidi ya Sh75 bilioni kwenye mapato ya Serikali kiwango kinachoonyesha ufanisi wake na tija ya uwekezaji huu,” amesema Mchechu.

Kwa upande wa kijamii, Mchechu amesema zaidi ya Watanzania 4,000 wamenufaika na ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, huku TPC ikiendelea kuwekeza katika elimu, afya na miundombinu ya jamii, jambo linaloimarisha ustawi wa wananchi.

Amesema zaidi ya Sh265 bilioni zimeshatumika kuboresha miundombinu, mashamba na teknolojia, hatua iliyowezesha kampuni hiyo kufikia uzalishaji wa wastani wa tani 150 za miwa kwa hekta kiwango kinachotambuliwa kama miongoni mwa bora Afrika na duniani.

Akizungumzia mradi mpya wa TPC Distillery Limited, Mchechu amesema mradi huo ni mwendelezo wa ushirikiano wa kimkakati, ambapo Serikali na TPC wanamiliki asilimia 85 ya hisa, wakati mwekezaji mpya, Isautier Drinks Africa, akimiliki asilimia 15.

Amesema hatua hiyo inaonyesha kuongezeka kwa imani ya wawekezaji wa kimataifa katika uthabiti wa uchumi wa Tanzania.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Miwa Group, Arnaud Lagesse, amesema historia ya miaka 25 ya TPC ni ushahidi wa maono, ustahimilivu na kazi ya pamoja.

Amebainisha kuwa licha ya changamoto za ukame, misukosuko ya soko na mabadiliko ya kiuchumi, kampuni imeendelea kukuwa na kufikia uzalishaji wa rekodi mwaka 2025.

Lagesse amesema ujenzi wa kiwanda kipya cha kuchakata molases ni sehemu ya mkakati mpana wa kupanua minyororo ya thamani na kuimarisha uthabiti wa kimazingira.

Ameongeza kuwa “Dira ya TPC ni kuendelea kuwa kinara wa ubora barani Afrika kupitia uzalishaji wa sukari, ethanol na bidhaa nyingine, sambamba na kuimarisha mchango wake katika jamii na Taifa kwa ujumla,” amesema.

Ameipongeza Serikali kwa kujenga mazingira bora ya uwekezaji, akisema hatua hiyo imeiwezesha TPC kukua na kuwa mfano halisi wa ushirikiano wenye tija kati ya sekta ya umma na binafsi huku akisisitiza kuwa mafanikio ya TPC ni uthibitisho kuwa Tanzania ni eneo sahihi kwa uwekezaji endelevu.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa, ameipongeza TPC kwa mchango wake mkubwa katika uchumi wa mkoa huo, hususan kupitia mradi wa kiwanda kipya cha kuchakata molases ambacho alikitaja kuwa kielelezo cha uwekezaji endelevu.

“Mradi huu unafaida kubwa kwani ni utaongeza ajira mpya, utaongeza mapato yanayotokana na kodi lakinj pia utaongeza thamani katika sekta za sukari na nishati, na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika soko la kikanda,” amesema Nzowa.

Mradi huo unaendana na dira ya Serikali ya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, kukuza viwanda na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi, hivyo kuonyesha dhamira ya TPC katika ubunifu, uendelevu na uwezeshaji wa jamii.

Maadhimisho hayo yalitoa wito wa kuendelea kuimarisha ubunifu, kuongeza uzalishaji na kuifanya TPC kuwa kitovu cha maendeleo ya Kilimanjaro na mhimili muhimu wa uchumi wa Taifa.