Zimamoto yakiri kuchelewa eneo la tukio ajali moto, sababu yatajwa

Shinyanga. Kaimu Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Shinyanga, Mrakibu Msaidizi Stanley Luhwago, ameeleza sababu za gari la zimamoto kuchelewa kufika eneo la tukio, akisema kuwa gari hilo lilipata hitilafu njiani.

Amesema tukio la moto lilitokea Novemba 19, 2025 majira ya saa 11 jioni, na mara baada ya kupigiwa simu waliwahi kuanza safari kuelekea eneo la tukio. Hata hivyo, wakiwa njiani bomba la upepo la gari lilipasuka, jambo lililosababisha ucheleweshaji.

Akizungumza leo Novemba 20, 2025 kwa njia ya simu, Luhwago amesema walifanikiwa kurekebisha hitilafu hiyo na kufika eneo la tukio, ambapo zoezi la uokoaji lilikuwa tayari limeanza kwa jitihada za wananchi.

“Ni kweli tulipigiwa simu mida ya saa 11 jioni kuwa kuna moto unateketeza nyumba, lakini tulipokuwa barabarani kuelekea eneo la tukio bomba la upepo la gari lilipasuka kitu kilichopelekea kuchelewa kufika, tulifanikiwa kutatua tatizo hilo na kufika eneo la tukio, lakini chanzo cha moto bado hakijajulikana tunaendelea na uchunguzi,” amesema Luhwago.

Tukio la ajali lilivyokuwa

Novemba 19, 2025, majira ya saa 11 jioni, nyumba yenye makazi ya watu na shughuli za biashara iliyopo maeneo ya Mnara wa Voda iliteketea kwa moto.

Wananchi walifanikiwa kuuzima moto huo kabla ya askari wa zimamoto kufika, huku wakilalamikia ucheleweshaji wa gari la zimamoto.

Kufuatia hasira hizo, baadhi ya wananchi walilishambulia gari la zimamoto kwa mawe mara lilipowasili eneo la tukio.

Baadhi ya mashuhuda na waathirika, akiwamo Zainab Shaban, walieleza kusikitishwa na kitendo cha polisi kuwatawanya wananchi, wakidai kuwa wananchi hao ndiyo waliotoa msaada mkubwa katika kuokoa mali zilizokuwa ndani ya nyumba wakati jeshi la zimamoto halijafika licha ya kupigiwa simu mapema.

Hali hiyo ilitulizwa baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Shinyanga, ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya Julius Mtatiro, pamoja na Jeshi la Polisi chini ya Kamanda Janeth Magomi, kufika eneo la tukio na kudhibiti vurugu zilizokuwa zimeanza kujitokeza.