Dare es Salaam. Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Dar es Salaam imewapa siku 14 wakazi wawili wa Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, kufungua maombi ya mapitio ya mahakama dhidi ya taasisi tano za Serikali.
Kibali hicho kimetolewa jana Jumatano, Novemba 19, 2025 na Jaji Anorld Kirekiano wakati akitoa uamuzi wake wa maombi namba 23799 ya 2025 ambayo wananchi hao wakazi wa kiwanja namba 344 na 346 wanataka kufungua maombi hayo.
Kiini cha wananchi hao, Ernest Mbuli na Kimonge kufungua shauri hilo ni madai kuwa baa ya Dove Nest Garden Events Bar and Grill ya jijini Dar es Salaam inasababisha kelele nyingi za muziki, kero na athari mbaya kwa afya na mazingira yao.
Maombi hayo ni dhidi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, kama wajibu maombi wa 1,2 na 3 mtawalia.
Katika shauri hilo, wananchi hao wamewaunganisha Kamanda wa Polisi wa mkoa (RPC), mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Waombaji hao, wameeleza kupitia viapo vyao kuwa nyumba zao zipo jirani na kiwanja namba 616 kitalu K ambacho mjibu maombi wa tatu (mkurugenzi Manispaa ya Konondoni), ameipa leseni baa hiyo.
Wanadai kwamba hawafurahishwi na kutolewa kwa leseni hiyo kwa kuwa uendeshaji wa baa na matukio yanayofanyika hapo, vinasababisha uchafuzi wa mazingira kwa kelele nyingi, kero na athari mbaya kwa afya na mazingira yao.
Waombaji hao wanadai wamestahimili hali hiyo, lakini tatizo limeongezeka siku za hivi karibuni, kuanzia Juni 2025 hadi Agosti 2025 na kwamba malalamiko yao (waombaji) kwa wajibu maombi namba 1, 2, 3 na 4 yameonekana hayana maana.
Kwa hivyo waombaji wameamua kufungua shauri kwamba wajibu maombi wanayo mamlaka ya kisheria ya kuhakikisha kelele zinadhibitiwa, kupigwa marufuku na wahusika kuadhibiwa lakini wamepuuza kutekeleza majukumu yao.
Hivyo waliiomba mahakama iwape kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya mahakama ili kuwalazimisha wajibu maombi kutimiza wajibu wao na kuizuia baa hiyo kuendelea kusababisha uchafuzi wa mazingira kutokana na kelele.
Walieleza kelele hizo zinavuruga hali ya ukimya na amani na wao na familia zao kushindwa kufurahia kuishi katika nyumba zao kutokana na kelele.
Kwa mujibu wa viapo hivyo, waliwasiliana na mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na kuwasilisha malalamiko yao lakini hawakupata majibu yoyote na kwamba mkurugenzi hakuwashirikisha katika mabadiliko ya matumizi ya ardhi yaliyosababisha hali hiyo.
Katika usikilizwaji wa maombi hayo, waleta maombi waliwakilishwa na kampuni ya mawakili ya Nyanduga Law Chamber Advocates wakati wajibu maombi wote waliwakilishwa kortini na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Ayoub Sanga.
Wakati wa mchakato wa usikilizwaji wa awali wa maombi hayo, wajibu maombi walipewa muda wa kuwasilisha kiapo kinzani, na baadaye wakili Sanga aliieleza mahakama kuwa hawana kipingamizi dhidi ya maombi ikiwa wahusika wamekidhi vigezo.
Jaji amesema katika kutoa kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya mahakama, mambo matatu huzingatiwa ambayo ni pamoja na kama waombaji wana uwezo wa kuyafungua, yamefunguliwa kwa wakati na wamejenga msingi wa kesi.
Kulingana na Jaji Kirekiano, baada ya kupitia maombi hayo pamoja na viapo vya waombaji, kigezo cha kwanza kimetimizwa kwa kuwa waombaji hao wana masilahi na maombi hayo kwa kuwa ni wakazi wa eneo linalolalamikiwa.
Jaji alisema waombaji wanaishi jirani na baa inayolalamikiwa kufanya uchafuzi wa mazingira kwa njia ya kelele na hiyo inathibitishwa na hati za umiliki wa viwanja vyao ambavyo vipo jirani na baa hiyo, hivyo wana masilahi na suala hilo.
Kuhusu kama maombi hayo yalifunguliwa ndani ya muda, viapo vya waombaji vinaeleza kuwa hali ya uchafuzi wa mazingira imekuwa mbaya zaidi kuanzia Juni 2025 hadi Agosti 2025 na kuna mawasiliano yaliyofanyika ndani ya miezi sita.
Jaji alisema kisheria, mtu hatapewa kibali cha kufungua maombi ya kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya mahakama isipokuwa tu kama maombi hayo yanafanyika ndani ya miezi sita tangu jambo linalolalamikiwa kutendeka.
“Ninaona wamefungua maombi ndani ya muda wa miezi sita kisheria,” alisema.
Kuhusu hoja kama kuna kesi yenye mashiko, Jaji alisema viapo vya waombaji vinaonyesha wajibu maombi ndio wanawajibika kusimamia masuala ya mazingira na sheria zake hapa Tanzania na NEMC imepewa mamlaka hayo kisheria.
Jaji alisema wajibu maombi wa tatu ambaye ni mkurugenzi wa Halmashauri na wa nne ambaye ni AG wana wajibu kwa umma wa kuhakikisha waombaji wanaishi kwa amani katika maeneo yao na bila kusumbuliwa na aina yoyote ya usumbufu.
“Inaonyesha waombaji wamejaribu kuwabana wajibu maombi watimize wajibu wao wa kisheria lakini hakuna kilichofanyika. Sasa kama hawakutimiza wajibu wao au walitimiza hayo yatazungumzwa katika maombi ya msingi,” alisema Jaji.
Jaji alisema pamoja na waombaji kuiomba mahakama itoe amri kwa Waziri, NEMC na RPC Kinondoni kuizuia mara moja baa ya Dove Nest Garden kuendelea kuchafua mazingira kwa njia ya sauti, katika hatua ya sasa hawezi kutoa amri hiyo.
Kulingana na Jaji, hatua ambayo mahakama ilikuwa inaifanya ni kupima kama maombi hayo ya kibali yamekidhi vigezo vya kisheria ili waweze kupewa kibali cha kuwaruhusu kufungua maombi ya mapitio ya mahakama juu ya suala hilo.
Jaji alisema kushughulikia ombi hilo itakuwa ni sawa na kusikiliza maombi ya msingi na sio sehemu yake hivyo akatoa siku 14 kwa waombaji kuwasilisha maombi yao ya mapitio kutaka uwajibikaji kwa wajibu maombi.
