Dar es Salaam. Taasisi za Kiislamu 27 nchini likiwamo Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), zimeazimia mambo 17 yatakayorejesha amani na utulivu nchini, huku zikikisisitiza njia ya maridhiano.
Mambo hayo yameazimiwa leo Alhamisi Novemba 20, 2025 na Amiri wa Baraza Kuu na Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Mussa Kundecha katika tamko alilolitoa mbele ya wanahabari, wakurugenzi wa taasisi za Kiislamu katika ofisi za makao makuu ya Bakwata Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Kabla ya Sheikh Kundecha kutoa tamko hilo, aliwaeleza wanahabari, viongozi waandamizi wa Bakwata, wenyeviti na wakurugenzi wa taasisi za Kiislamu kuwa, walifanya ibada ya Itikaf katika Msikiti wa Mfalme Mohamed VI.
Amiri wa Baraza Kuu na Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Mussa Kundecha akisoma tamko la Baraza na taasisi za kiislamu mbele ya wanahabari,katika ofisi za makao makuu ya Bakwata Kinondoni jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga
Itikaf ni ibada maalumu inayofanyika ndani ya msikiti kwa kujitenga na mengine yote ili kujikurubisha kwa Mungu, kutafuta radhi zake.
“Ibada hii hutumiwa na waumini kufikisha vilio na dua zao kwa Mungu wao asiyeshindwa na jambo lolote. Tumeona ni muhimu kuwa na ibada hii ya Itikafu baada ya matukio yaliyoikumba nchi yetu Oktoba 29,” amesema Sheikh Kundecha.
Oktoba 29 kulitokea matukio yaliyohusisha vurugu na uvunjifu wa amani ikiwamo kusababisha vifo, majeruhu, kuharibu miundombinu na kuchoma vituo vya polisi, ofisi za Serikali za mitaa, vituo vya mabasi yaendayo haraka, vituo vya mafuta mafuta, maduka na magari.
Kabla ya kueleza mambo hayo 17, Sheikh Kundecha amesema taasisi hizo zinalaani matukio hayo yaliyosababisha vifo vya majeruhi na vifo vya wananchi.
Akianza kutaja mambo hayo 17, Sheikh Kundecha amesema baada ya kutafakari kwa kina katika ibada hiyo, taasisi hizo zimeazimia kuunga mkono kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan, aliyoitoa katika uzinduzi wa Bunge la 13, jijini Dodoma Novemba 14 2025.
“Tunaunga mkono hatua ya Rais Samia kuunda Tume Huru ya Uchunguzi wa matukio ya uvunjivu wa amani yaliyotokea Oktoba 29,” amesema Sheikh Kundecha.
Mapema leo Alhamisi Novemba 20, 2025 Rais Samia amezindua tume hiyo inayoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Othman Chande na wajumbe wengine wanane, wakiwamo mabalozi wastaafu.
Pia, Sheikh Kundecha amesema taasisi hizo, zinaunga mkono mchakato wa maridhiano ya kitaifa uliopendekezwa na Rais Samia, akisema wapo tayari kushiriki na kutoa mchango wao.
“Msingi wa maridhiano hayo lazima ujikite kwenye uadilifu na dhamira njema, na sio juu ya vuguvugu la muda mfupi, au mashinikizo ya kisiasa au uanaharakati.
“Tuko tayari kuwa daraja la kuunganisha Watanzania,tunapendekeza uwepo uchunguzi wa kina, usiopendelea upande wowote, ili kubaini watu waliochochea, waliopanga, na kuratibu uhalifu uliotokea,” amesema Sheikh Kundecha.
Pia, amesema maridhiano yasiwe kichaka cha kuficha uhalifu, bali wenye hatia wajulikane, wasio na hatia walindwe na haki isimame sawa bila kupindishwa.
“Mchakato wa maridhiano, pamoja na umuhimu na ulazima wake, kamwe usituzibe macho tukashindwa kuun’goa mzizi wa fitina uliozaa maafa haya yaliyolitia doa Taifa letu,” amesema Sheikh Kundecha.
Sambamba na hilo, Sheikh Kundecha ameitaka Serikali kuangalia kwa jicho la huruma wale wote waliopoteza nafsi za ndugu zao, kuharibika kwa mali na biashara zao.
“Tunaipongeza Serikali kwa kutambua miongoni mwa waliokamatwa kulikuwa na vijana na wananchi waliofuata mkumbo bila dhamira mbaya.
“Juhudi za kuwatambua na kuwarejesha katika familia zao ni hatua ya uadilifu tunayoiunga mkono,” ameeleza.
Wakati akizundua Bunge hilo, Rais Samia alivielekeza vyombo vya sheria ikiwamo ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuangalia kiwango cha makosa yaliyofanywa na vijana hao.
“Kwa wale wanaoonekana wamefuata mkumbo, lakini hawakuonekana na dhamira ya kufanya uahalifu, wawafutie makosa yao. Pia, walioonekana kufuata mkumbo, lakini hawakudhamiria kufanya uhalifu, wafutiwe makosa,” alisema Rais Samia.
Katika hatua nyingine, Sheikh Kundecha amesema dini zote za Tanzania zinapinga uhalifu, chuki uharibifu wa mali na machafuko, hivyo viongozi wa kiroho wanapaswa kuikanya jamii hii dhidi ya uovu huo na kuhimiza kusameheana.
“Tunawataka Waislamu na Watanzania wote kwa jumla, pale wanapolazimika kudai haki zao, iwe ni serikalini au popote pale katika nchi yetu, wafuate taratibu na sheria zilizowekwa,”amesema.
“Tunayaagiza madawati mbalimbali ya dini yetu yanayotuunganisha na wenzetu wa dini nyingine, kufanya haraka kuratibu mkutano wa viongozi wakuu wa dini kwa lengo la kuinusuru nchi yetu na kuirejeshea amani yake.”
Sheikh Kundecha ametumia nafasi hiyo, kuwaomba Watanzania kutokubali kuchochewa na mijadala inayoendelea katika mitandao ya kijamii na majukwaa mengine yanayopandikiza chuki za kidini, kikabila, kikanda au ubaguzi wa aina ya yoyote.
“Tunawaasa vijana wetu kuitumia Desemba 9 kukaa nyumbani na wazazi wao, kuliombea Taifa letu, kufanya ibada kama sehemu ya kudumisha amani na utulivu wa nchi.
“Tumebaini kuwepo kwa hila za kupandikiza katika jamii yetu chuki, uhasama na majaribio ya kutugombanisha na kutugawa kwa misingi ya dini,” amesema Sheikh Kundecha.
Kutokana na hilo, amewaasa viongozi wa dini zote kuzikataa hila hizo na kuwaelimisha waumini wao kuhusu hatari zake kwa umoja na mshikamano wa Taifa.
“Tunawaagiza Waislamu wote katika misikiti yao, madrasa zao, vyuo vyao na katika kila mkusanyiko wao na kila mmoja wetu katika ibada zake kumuomba Mungu arejeshe na kuidumisha amani yetu iliyotetereka,” amesema.
Katika tamko hilo, Sheikh Kundecha amewasihi viongozi na Waislamu wote kuepuka kauli na matamshi yanayochochea na kuhamasisha mpasuko katika jamii.
“Mufti (Abubakar Zubeir) anatoa rai, tutumie maneno na kauli za kujenga, kuleta umoja na kuwa daraja kati ya Waislamu na baina yetu na Watanzania wengine wote.
“Tanzania ndiyo nchi yetu, hatuna nyingine, tusiruhusu amani yetu ijaribiwe au kuchezewa. Sisi taasisi za Kiislamu tutailinda amani hiyo kwa gharama yoyote ile,” amesema Sheikh Kundecha.
Awali, Katibu Mkuu wa Bakwata, Sheikh Nuhu Mruma amesema mkutano huo umeshirikisha takribani taasisi za Kiislamu 30 ikiwamo Jumuiya ya Maimamu Tanzania, sambamba na masheikh wa mikoa 19.
