Kibarua kinachomsubiri Simbachawene | Mwananchi

Dar es Salaam. Baada ya George Simbachawene kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, anakabiliwa na jukumu la kuhakikisha usalama wa raia, utulivu na utawala wa sheria vinaendelea kudumishwa nchini.

Hata hivyo, wadau wa sekta ya usalama wanasema mafanikio yake yataongezeka endapo vyombo vilivyo chini ya wizara hiyo vitakuwa karibu zaidi na wananchi ili kutoa huduma bora na zinazojibu mahitaji ya jamii, kwa kuzingatia kwamba wananchi wana uelewa mpana kuhusu changamoto na fursa zilizopo katika wizara hiyo.

Novemba 17, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alimteua Simbachawene kuongoza wizara hiyo nyeti inayogusa maisha ya Watanzania moja kwa moja, akisaidiwa na naibu wake, Denis Londo.

Wizara hiyo inahusika na usimamizi wa vyombo vya ulinzi na usalama, kuratibu masuala ya dharura na majanga, pamoja na kuhakikisha utawala bora katika taasisi zilizo chini yake.

Kushika kwake wadhifa huo, Simbachawene anakabiliwa na jukumu la kuimarisha utendaji wa Jeshi la Polisi, hasa katika kukabiliana na ongezeko la vitendo vya uhalifu na utekaji, lakini pia kitendo cha Jeshi la Polisi kujichunguza kwa baadhi ya matukio wanayohusika.

Jukumu lingine ni kurejesha na kuimarisha imani ya wananchi kwa jeshi hilo, kusukuma mageuzi ya mifumo ya kiusalama na kuhakikisha teknolojia mpya zinatumika katika kupambana na uhalifu wa kimtandao unaozidi kukua.

Aidha, anahitajika kusimamia maboresho ya huduma na utekelezaji wa majukumu katika vyombo vilivyo chini ya wizara yake ikiwemo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Jeshi la Magereza na Idara ya Uhamiaji ili kukuza uwajibikaji na kuongeza ufanisi wa utendaji.

Kwa upande wa uhalifu wa ndani, matukio kama uporaji, utekaji, uhalifu mtandaoni na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia yameendelea kuibua hofu miongoni mwa wananchi.

Changamoto hizi zinahitaji mbinu mpya za kiintelijensia, uwekezaji katika miundombinu ya kiusalama na matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuyadhibiti kikamilifu.

Wizara hiyo inakabiliwa na kazi ya kusimamia usalama katika mipaka ya nchi, kuhakikisha udhibiti madhubuti wa wahamiaji haramu na kukabiliana na magenge ya biashara za dawa za kulevya, vitendo vinavyozidi kuathiri jamii na uchumi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi, wadau hao akiwemo Kamishna Msaidizi Mwandamizi (mstaafu) wa Polisi (SACP), Jamal Rwambow, wamesema wananchi wanajua mengi kuhusiana na yote katika wizara hiyo.

“Kuna wakati wizara hiyo ilifanikiwa katika idara zake kuwa karibu na watu, walipotea wapi hadi sasa watu wanaviangalia hivyo vyombo tofauti, hilo sijui. Vyombo viwe karibu na watu,” amesema.

Kwa mujibu wa Rwambow, jamii haiwezi kuwa karibu na vyombo hivyo ikiwa havitekelezi majukumu yake kwa kuzingatia utu, vikigeuka vya kibabe haviwezi kufika kokote.

“Anatakiwa kuwa na jicho la kusikiliza, awasikilize watu maeneo mbalimbali. Ana hazina kubwa ya watu wa kumsaidia kama atawatumia. Vile vyombo kabla ya hao waliopo kulikuwa na watu walioviendesha, si vibaya kupata maoni yao waliotangulia,” amesema.

Rwambow amesema ikiwa ataomba ushauri watamsaidia, lakini ikiwa atataka kujifungia na kuwatumia walipo katika nafasi hizo, kuna wakati atadanganywa.

“Unajua hivyo vyombo vinatazamwa kunuka kwa rushwa. Ili akonge nyoyo za wananchi anatakiwa kupambana na rushwa, kuna rushwa ndani ya Polisi na ndani ya vyombo vingine. Sasa akipuuzia itakuwa hakuna kitu,” amesema.

Amesema anatakiwa kuonesha kukataa na kukemea rushwa na kuchukua hatua kwa watuhumiwa wote wa rushwa bila kujali nafasi zao, kuanzia wa ngazi ya chini hadi juu, akifanikiwa hilo atasaidiwa.

“Watu wana taarifa nyingi, lakini huwezi kuzipata ikiwa utajifungia milango,” amesema Rwambow.

Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Flugence Massawe, amesema kuna matukio ambayo Jeshi la Polisi limekuwa likilalamikiwa na wananchi, hivyo waziri anatakiwa kulisimamia jeshi hilo lifanye kazi kwa weledi.

“Akilisimamia jeshi kwa weledi, itapunguza malalamiko na manung’uniko ya wananchi kupitia utendaji wake. Kumekuwa na tatizo la watu wasiojulikana, na yakitokea matukio ya kutisha polisi wanatoa majibu rahisi watu wasiojulikana,” amesema.

Kwa mujibu wa Massawe, jeshi hilo limeshindwa kuchunguza na kuwaambia wananchi asiyejulikana ni nani, tafsiri yake nchi imebaki bila ulinzi.

“Huwezi kusema ‘watu wasiojulikana’ basi. Inatutia wasiwas, watu wanatekwa ni kesi ambazo zinaogofya na zinaacha maswali kwa wananchi. Kwa hiyo suala la usalama wa raia limekuwa changamoto,” amesema.

Amesema weledi unahitajika katika chombo hicho huku akieleza uzuri wake ni kwamba si mgeni katika wizara hiyo, alishawahi kushika wadhifa huo, lakini huenda halikuwa kama ilivyo sasa.

Makamu Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi–Bara, Joseph Selasini, amesema waziri anatakiwa kurudisha imani ya wananchi kwa Jeshi la Polisi kwa kuwa limekuwa likionea watu.

“Watu wanateseka kwa kubambikiziwa kesi, kushikiliwa mahabusu kwa muda mrefu bila kupewa dhamana; hayo ni mateso. Jeshi la Polisi limejipa nguvu ya kimahakama—linakamata, linasikiliza ushahidi na linaukumu,” amesema.

Selasini amesema hiyo si kazi ya polisi, anatarajia waziri abadili mtindo huo kwani chombo hicho kazi yake ni kukamata, lakini kukaa na mtu muda mrefu ni kuingiza chuki katika jamii.

Katika kuchangia maoni hayo, baadhi ya wadau walikuwa wanakinzana akiwemo Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, aliyedai suala linalohusu utu na usalama wa raia ni saratani isiyo na tiba.

“Ni lazima tukate mguu, tukatafute mguu wa raia ili tupate mabadiliko. Kweli ni lazima mitaala ya Jeshi la Polisi ifumuliwe upya na ihaririwe tupate muundo mpya na kuligeuza Jeshi la Polisi kuwa huduma na si kutumia nguvu,” amesema.

Amesema kwa sasa jeshi hilo limejikita kwenye usalama wa viongozi na si raia, lakini kusema waziri huyo atafanya lolote haiwezekani labda kumpa kibogoyo atafune mifupa.

“Waziri hawezi kufanya lolote kulingana na mfumo wa kikatiba, kisheria na kisera labda kama nchi ingeandika Katiba kwanza, tuanze upya. Lakini kuja kwa waziri huyo tusitegemee mapya,” amesema.

Kabla ya kuteuliwa kuongoza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Simbachawene ambaye ni mbunge wa Kibakwe, alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Amechukua nafasi hiyo kutoka kwa Innocent Bashungwa aliyeiongoza kuanzia Desemba 10, 2024 hadi sasa, ingawa naye alikalia nafasi hiyo kutoka kwa Hamad Yusuf Masauni.