WAZIRI KAPINGA AHIMIZA KUKUA KWA BIASHARA ILI KUWAWEZESHA VIJANA

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, akizungumza mara baada ya kukabidhiwa Ofisi na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo Dkt.Selemani Jafo,hafla iliyofanyika leo Novemba 20,2025 katika Ofisi za Wizara zilizopo Mtumba jijini Dodoma.

Na.Alex Sonna-DODOMA

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha Watanzania, hususan vijana, wanapata maendeleo kupitia ukuaji wa sekta za viwanda na biashara, na amewataka watumishi wa wizara hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano ili kufanikisha malengo hayo.

Akizungumza leo Novemba 20,2025 wakati wa makabidhiano ya ofisi, Waziri Kapinga amesema  kuwa kufanikisha maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kunahitaji mshikamano wa watumishi katika kutekeleza majukumu, hasa ikizingatiwa sekta hizo ndizo zinazoibeba ajira na uchumi wa wananchi.

“Ushirikiano ni muhimu katika kutimiza malengo na maono ya Rais Samia, ambaye mara zote amesisitiza kuhakikisha biashara inaendelea kukua. Ni sekta inayochagiza maendeleo kwa Watanzania, hususani vijana, ambao katika muhula wake wa pili ameyaweka macho yake zaidi,” amesema Mhe.Kapinga

Kapinga amesema kuwa ana imani kubwa na rasilimali watu iliyopo katika wizara hiyo na akawataka watumishi kuwa tayari kutekeleza majukumu kwa ufanisi ili kuhakikisha matokeo chanya kwa wananchi.

Aidha, ametoa shukrani kwa watangulizi wake kwa mchango wao katika kuendeleza sekta hizo na kuwasihi watumishi kuendelea kujifunza kutoka kwao.

“Muhula wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Sita umeleta matokeo makubwa katika sekta ya viwanda na biashara. Kazi hiyo isingekamilika bila wasaidizi ambao Rais alikuwa nao, akiwamo kaka yangu Dk. Selemani Jafo. Namupongeza kwa kazi kubwa iliyofanyika, na tukiwa na uhitaji wa ushauri, tutaendelea kugonga mlango wake,” amesema Mhe.Kapinga

Kwa upande wake, Waziri aliyemaliza muda wake, Dk. Selemani Jafo, amewataka watumishi wa wizara hiyo kutoa ushirikiano kwa viongozi wapya na kuendelea kuchapakazi kwa bidii.

“Nawaomba muwape ushirikiano viongozi wapya. Endeleeni kuchapa kazi ili wizara iendelee kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi,” amesema Dk.Jafo.

Aidha, amewasihi watumishi kuendelea kumwombea Rais Samia Suluhu Hassan ili aweze kutekeleza majukumu yake na kuiendeleza nchi kwa amani.

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, akizungumza mara baada ya kukabidhiwa Ofisi na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo Dkt.Selemani Jafo,hafla iliyofanyika leo Novemba 20,2025 katika Ofisi za Wizara zilizopo Mtumba jijini Dodoma.

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga,akimsikiliza aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo Dkt.Selemani Jafo  akizungumza mara baada ya kukabidhiwa Ofisi hiyo  leo Novemba 20,2025 katika Ofisi za Wizara zilizopo Mtumba jijini Dodoma.

 

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga,akikabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo Dkt.Selemani Jafo,hafla iliyofanyika leo Novemba 20,2025 katika Ofisi za Wizara zilizopo Mtumba jijini Dodoma.